02 August 2013

MAJANGA

  • GHOROFA LINGINE TISHIO HILI HAPA
  • WAHUSIKA WAZIDI KUPIGA CHENGA

Na Goodluck Hongo
BAADHI ya maghorofa yaliyojengwa jijini Dar es Salaam yamezidi kubainika kuwa ni tishio kwa wakazi wanayoyatumia, wapita njia na majirani kutokana na kuwa na nyufa zinazoashiria kuwa yanaweza kuanguka wakati wowote, huku mengine yakifikia hatua ya kuanza kuegemeana.

Uchunguzi wa Majira jijini Dar es Salaam umefanikiwa kubaini ghorofa lingine ambalo ni tishio kwa maisha ya wananchi, lakini cha kushangaza mamlaka husika zimeendelea kukwepa kutoa ushirikiano, licha ya gazeti hili hivi karibuni kuchapisha habari kuhusiana na hali ya ghorofa la Golden Plaza lililopo kwenye mtaa wa Agrrey na Indira- Ghand.
Jengo hilo la ghorofa takriban 10 lipo mtaa wa Zanaki na Libya, jijini Dar es Salaam ambalo limeyumba kiasi cha kugusana na ghorofa lingine.
Mmoja wa maofisa katika Serikali ya Mtaa wa Kisutu, jijini Dar es Salaam ambaye jengo hilo lipo kwenye eneo lake la kiutawala, (jina tunalo) alisema hali ya jengo hilo wanaifahamu siku nyingi, lakini wahusika ni Manispaa ya Ilala.
Alikiri kuwa analifahamu jengo hilo, lakini kitaalamu mhandisi wa Manispaaa ndiye anayeweza kulitolea ufafanuzi zaidi ni kwa nini lipo katika hali hiyo.
Baadhi ya wananchi wanaoishi eneo hilo, walisema kwa muda mrefu jengo hilo wamekuwa wakililalamikia lakini hakuna mamlaka husika ambazo zimeweza kuonesha ushirikiano.
"Unajua tatizo letu hapa ni uwajibikaji wa viongozi, watu wanasubiri hadi madhara yatokee ndipo wawajibike, tumelalamika muda mrefu, lakini hatujaona uwajibikaji," alisema na kuongeza;
"Majengo haya tunayafahamu muda mrefu yalikuwa yameachana lakini sasa yamefikia hatua ya kulaliana maana yake ni kwamba kama kusingekuwepo na jengo hilo (lililolaliwa) maafa yangetokea."
Gazeti hili, lilishuhuda hali ya jengo hilo huku maisha yakiendelea kama kawaida miongoni mwa wapangaji wa jengo hilo, bila kujali hatari iliyopo mbele yao.
Diwani wa Kata ya Kisutu ambaye ni Naibu Meya wa Manispsaa ya Ilala, Khery Kessy, alipoulizwa kuhusiana na hali ya jengo hilo, alisema wao sio wataalamu wa majengo bali wahusika wapo.
Alisema analijua suala hilo tangu miaka minne iliyopita, lakini hadi
 sasa hakuna kitu kilichofanyika kwani kwa sasa hakuna mamlaka ya moja kwa moja ya kushughulikia suala hilo.
"Zamani jiji ndiyo lilikuwa linashughulika na kila kitu hata ambapo wao ndio wanunuzi na waamuzi katika manispaa zao na hilo lilikuwa rahisi hata kuwadhibiti watu ambao wanafanya makosa, lakini kwa sasa hivi ni vigumu kwani kuna mamlaka nyingi zinazoshughulika na kitu kimoja na matokeo yake ndiyo mengine yanajitokeza," alisema Diwani Kessy.
Alisema ni vyema kila manispaa ziwe na mamlaka kamili ya kuiwezesha kudhibiti majengo ya aina hiyo. Alitolea mfano hali ya chemba moja ya maji taka ambayo imeziba na kumwaga vinyesi barabarani karibu na mitaa hiyo.
Alisema kila walipofuatilia wahusika wanatupiana mpira, kila mtu anasema hahusiki, lakini kama Jiji lingekuwa na mamlaka kama zamani hali hiyo isingekuwepo na mara moja hatua zingechukuliwa.
B a a d h i y a wa s imami z i wa majengo ya maghorofa waliozungumza na gazeti hili walisema mara nyingine hali hiyo inatokana na kuchakachuliwa kwa ukubwa wa nondo au wakati wa kuchanganya kokoto, saruji na mchanga (zege).
Walisema ujenzi wa ghorofa ambalo baadaye linaenda upande husababishwa na kiti cha ghorofa kujengwa katika sehemu ambayo haina mwamba mgumu.
"Kabla hujajenga nguzo za ghorofa lazima kwanza uchimbe chini hadi ukutane na mwamba mgumu na hapo ndipo uanze kujenga, lakini ukianza ujenzi katika eneo ambalo halina mwamba mgumu, basi lazima jengo litaelemea upande mmoja na hatima yake ni kuanguka," alisema mzee Mohamed Musa ambaye ni msimamizi wa ujenzi wa ghorofa nane.
Alisema ghorofa linaweza kuwa na nyufa katika beem na likakaa kwa muda mrefu bila kuanguka lakini hiyo yote inatokana na ujenzi ambao haukufuata viwango vinavyotakiwa.
Alisema mara nyingi nguzo zinazoshikilia ghorofa lazima ziwe na nondo kuanzia milimita 25 na ziedelee hivyo hadi sakafu ya mwisho, lakini ikiwemo nguzo moja kuwa na nondo 10 lakini wengine huweka hadi milimita 16 hadi 20 na nondo nane katika beem moja na matokeo yake ni kutokea ufa na wakati mwingine kuanguka.
"Mfano msikiti wa ...(anataja jina) una ufa katika beem na mimi
 huo tangu miaka 10 iliyopita, lakini hadi leo unaendelea kutumika na sio hilo tu bali kuna majengo mengi sana hapa Kariakoo." alisema.
Gazeti hili lilifanya jitihada za kuwasiliana na Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) Injinia Steven Mlote, ili kuzungumzia suala hilo lakini ilishindikana kutokana na Katibu Muhtasi kusema kwamba siku hiyo asingeweza kuzungumza na mwandishi wa habari hii.
"Hautaweza kuzungumza naye kwani haikuandikwa kwenye kitabu cha kumbukumbu (Kitabu cha watu wanaotakiwa kumuona siku hiyo,) alisema Katibu Muhutasi huyo.
Awali gazeti hili liliwasiliana na Injinia Mlote kwa njia ya simu ambapo alimtaka mwandishi aende ofisini kwake ili azungumzie suala hilo, lakini alipoenda hakuweza kuonana naye.
Pamoja na Katibu Muhutasi kuelezwa hivyo, bado aliendelea kushikilia msimamo kuwa wanaoingia kumuona ni wale wenye miadi naye.
Gazeti hili lilipomtafuta Mhandisi wa Manispaa ya Ilala ili kuzungumzia suala hilo kila wakati alikuwa akidai yupo kwenye shughuli zingine au kwenye vikao

 


2 comments:

  1. Majanga haya yatatuandama daima kama wahusika hawatachukuliwa hatua za kisheria - inaonekana kuwa kuna ulaji mkubwa baina ya NHC, maafisa wa serikali na wale wanaojiita wawekezaji - matokeo yake majengo haya yataporomoka na kuwaua wengi - Ndo maana waziri anatoa amri ya kubomolewa lakini hakuna anayejali

    ReplyDelete
  2. Tanzania tuna kazi kubwa sana kufikia maendeleo endelevu,hakuna uwajibikaji kwa wahusika,kila kitu ni vululu vululu tu,sijui hadi wafe wajmba zao wa damu ndo wawajibike, hivi sie aliyeturoga kafa nini ndo maan kila sehemu hakuna kinachowezekana kufanikiwa,Serikali kazi yake ni nini,watendaji nao kazi zao ni nini,mbona majangaa,loh!!

    ReplyDelete