05 August 2013

WAZIRI KIGODA AFUFUA MATUMAINI YA VIWANDA


Na John Gagarini, Kibaha
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda amesema kuwa uchumi wa Tanzania hauwezi kutegemea kilimo pekee bali viwanda ndivyo vinaweza kuinua uchumi na kuifanya nchi kuwa ya viwanda ifikapo mwaka 2025.


Aliyasema hayo juzi kwenye Mtaa wa Zegereni wilayani Kibaha mkoani Pwani, wakati akizindua kiwanda cha kutengenezea 'Gypsum' cha Kampuni ya Sun Shine Gypsum Limited Group kutka China na kusema kuwa viwanda ndiyo moja ya vyanzo vya mapato nchini.
Dkt. Kigoda alisema kuwa hata nchi zilizoendela zilianza na viwanda vidogo na viwanda vya kati hadi vikafikia kuwa na utajiri mkubwa walionao sasa ambapo China ni moja wapo ya nchi zilizoanza kwa utaratibu huo lakini kwa sasa iko mbali kiuchumi.
"Viwanda vinachangia asilimia 30 ya pato la Taifa huku asilimia 40 ya wananchi wakiwa wameajiriwa kwenye sekta ya viwanda hapa nchini na kufanya uchumi kutegemewa kwa kiasi kikubwa kupitia sekta hiyo ambayo kwa sasa inaendelea kukua licha ya baadhi ya watu wakidai kuwa eti Tanzania haina viwanda vingi jambo ambalo si kweli," alisema Dkt. Kigoda.
Aidha alisema kuwa hata wajasiriamali wa Tanzania wanaweza kuungana kujenga viwanda kama hivi ambavyo ni vya daraja la kati hasa ikizingatiwa malighafi za kutengenezea bidhaa hiyo zote zinapatikana hapa hapa nchini.
"Mnapaswa kutoa kipaumbele cha ajira kwa wakazi wa Kibaha ili nao wafaidi matunda ya uwepo wa kiwanda hiki na msaidie huduma za kijamii na kujenga uhusiano mzuri pia mzingatie viwango ili bidhaa hizi ziweze kuwa na soko ndani na nje ya nchi," alisema Dkt. Kigoda.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, Silvestry Koka aliipongeza kampuni hiyo na kusema kuwa dhana ya kurudisha uchumi kwa wananchi sasa imeanza kuonekana kwani baadhi ya wakazi wa hapa wamepata ujuzi na ajira.
Koka alisema kuwa kampuni hiyo imezingatia suala la ajira kwani hadi sasa watu 60 wamepata ajira huku baadhi yao wakipewa kazi za umeneja na si kuwa zile za ufagizi tu kwani hayo ndiyo yanayopaswa kufanywa na viwanda vingine ili kuweka usawa wa utendaji kazi.
"Mji uliamua eneo hilo la Kata ya Visiga kuwa eneo la viwanda hivyo wajasiriamali na watu mbalimbali wananafasi kubwa ya kuweka viwanda vyao hapa na si kung'ang'ania kujenga Dar es Salaam pekee ambapo hadi sasa tayari kuna viwanda vinne vingine vikiwa ni cha kusafishia mafuta, madini na nondo, vimeshajengwa kwenye eneo hilo," alisema Koka.
Kiwanda hicho kilianzishwa mwaka jana na kina thamani ya dola za Marekani milioni tatu na kimeajiri watu 60 na tayari kimeanza uzalishaji ambapo bidhaa zake zinauzwa ndani na nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment