02 August 2013

PINDA ABURUTWA MAHAKAMANI


 • MWANASHERIA MKUU SERIKALINI NAYE YUMO
 • MAWAKILI ZAIDI YA 20 WAMEJIPANGA KUMKABILI
Na Mariam Mziwanda

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimemfungulia mashtaka Mahakama Kuu ya Tanzania, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutokana na kauli yake aliyoitoa bungeni ya kuruhusu vyombo vya usalama kuwapiga watu wanaokataa kutii sheria zinazotolewa na vyombo hivyo.


Mashtaka dhidi ya Waziri Pinda, yaliwasilishwa mahakamani hapo jana na wanasheria wa LHRC, TLS wakisindikizwa na taasisi inayofuatilia mwenendo wa bunge na wananchi.

Katika shauri hilo LHRC inawakilishwa na mawakili zaidi ya 20.Mbali na Pinda mwingine aliyeunganishwa katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Waziri Pinda, anakabiliwa na tuhuma za kudaiwa kuvunja katiba ya nchi kwa kuruhusu askari kuwapiga wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasilisha hati ya mashtaka dhidi ya Waziri Pinda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mwenyekiti wa Bodi ya LHRC, Dkt. Ringo Tenga, alisema watu wenye mamlaka inapotokea wakakiuka katiba ya nchi, mahakama ndiyo mwamuzi pekee, hivyo kituo hicho kimefikisha suala hilo mahakamani kutafuta suluhu.

"Katiba ipo wazi, Waziri Mkuu amevunja katiba hivyo ni sahihi kumpeleka mahakamani, ndiyo sehemu pekee atakayoeleza uhalali wa polisi kupiga wananchi," alisema na kuongeza kuwa anashukuru wananchi zaidi ya 3,000 ambao wamesaini hati ya makubaliano ya kumfikisha Waziri Pinda mahakamani.

Alifafanua kwamba wao wana imani na mahakama, hivyo wanasubiri taratibu za kesi hiyo kupangiwa jaji baada ya washtakiwa hao kupelekewa hati ya kuitwa mahakamani.

Naye Mkurugenzi wa LHRC, Dkt. Hellen Kijo-Bisimba, alisema kauli ya mwanasheria mkuu kuwa Waziri Pinda, hawezi kushtakiwa kutokana na kulindwa na kanuni za bunge, alidai hizo ni kauli za kisiasa.

Alisema mwanasheria mkuu amejisahau kwani hata yeye ameona athari za polisi kuwapa nafasi za kupiga wananchi.

Alisema mwanasheria mkuu anachotakiwa ni kuipa kinga Katiba ya nchi kwa mujibu wa Ibara ya 100 na sio kumpa kinga mtu. Alisema Ibara ya 100 ya Katiba inaeleza kuwa kinga ni kwa ajili ya Katiba, hivyo Waziri Pinda ametoka nje ya mipaka ya Katiba, hivyo kinga ya mwanasheria mkuu na wabunge haimsaidii, waache mahakama ione maamuzi dhidi yake.

Kutokana na hali hiyo, alisema ndiyo maana LHRC imeona haja ya kupeleka mashauri mawili mahakamani hapo,ambalo moja linahusu kauli ya pinda na lingine mwanasheria mkuu juu ya kinga za bunge zinapoingilia haki za binadamu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi inayofuatilia mwenendo wa Bunge, Marcossy Albanie, alisema wanaunga mkono uamuzi huo, kwani tamko la Pinda ni kubwa lililovunja katiba na bado wanaamini kuwa ni tamko la Serikali.

Alisema mbali na shtaka hilo dhidi ya Waziri Mkuu, taasisi yake ina shtaka lingine dhidi ya Pinda kutokana na kauli yake anayoitoa mara kwa mara bungeni kuwa amechoka.

Alisema watamshtaki kwa wananchi kwani kauli hiyo ni msisitizo kuwa Pinda na Serikali yake inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete, wamechoka kuwaongoza wananchi, hivyo hawezi kuendelea kuwavumilia.

Katika kikao cha Bunge lililopita wakati wa maswali ya papo kwa papo Waziri Mkuu Pinda alisema;

"Ukifanya fujo na umeambiwa usifanye hiki na wewe ukaamua ukakaidi utapigwa tu, maana hakuna namna nyingine...ehee maana wote tukubaliane nchi inaongozwa kwa misingi ya kisheria, sasa kama wewe umekaidi, hutaki, unaona wewe ni imara zaidi, wewe ndiyo jeuri zaidi watakupiga tu na mimi nasema muwapige kwa sababu hakuna namna nyingine maana tumechoka sasa."

13 comments:

 1. Hii kesi haina maana yoyote.Mngetetea wanyonge wasiojua sheria nza ardhi,wanauawa ktk ajali bila fidia na wajane wanaodhulumiwa.Vyombo vya dola vya ulinzi lazima vitishe wakorofi katika jamii.Lakini sio kuuwa.Mtu akiandamana kuingia nyumbani kwako kwa nguvu utamtisha kwa bastola akivunja mlango utamvunja mguu(diable) ili uweze kumtuliza umpeleke mahakamani.Mjane wa Jaji Uzia alivamiwa saiti yake juzi,ilibidi jeshi lije litishe ndo wakakimbia.

  ReplyDelete
 2. Ndyo. Takwimu zao tu zinawasuta. Kwa wale wanaofuatilia mambo kwa makini katika TV walisema serikali ilisababisha vifo katika ishirini, na wananchi wenyewe kwa wenyewe katika miatatu. Wapi na wapi? Waziri mkuu naye atishwe ili kisiwe na serikali. Mshikemshike uanze. Wao wana bastola za kujikinga, je sisi wanyonge tusiotembea hata na visu?

  Jamani wananchi wenzangu tulitafakari hili jambo kwa makini bila ushabiki wa upande wowote. Hawa wasomi wanatuingiza katika janga lingine. Someni lama za nyakati!

  ReplyDelete
 3. Hongera sana LHRC kwa kulivalia njuga suala hili - Je hao waojiita wanahakati nao wako wapi ? Mbona kimya ? Au mnaogopa kupigwa?

  ReplyDelete
 4. Wanaharakati! Hongera Pinda kwa kua tayari kuwajibika kwa kusimamia usalama wetu. Tujihurumie wenyewe lakini sio Pinda, kama Pinda atapelekwa jela. Watanzania wote tuungane tuondoe tofauti zetu za kisiasa tumuombee waziri mkuu

  ReplyDelete
 5. kauli ni kitu kizuri lakini kibaya sana kinaposhindwa kueleweka,inabidi hasa wakubwa kuchunga sana hilo fro salum danford

  ReplyDelete
  Replies
  1. Pole sana Danford. Itabidi uchunge ulimi hata ukiongea na wanao maanake watakuburuta kotini. Mtekelezaji wa serikali achunge ulimi ili asitoe amri halai. Huoni wahuni walivyofta, mbona hawakujitokeza baada ya kauli ya Pinda. Kauli ilielweka vizuri kwa walengwa! Wasioielewa sio walengwa, hivyo sio tatizo. Wajitokeze wapigwe! Hakuna cha mdav wa kuchezeana wakati tunapoteza mali zetu kwa ajili ya watu wenye malengo ya kujinufaisha binafsi bila kujali majali ya wengine. Hongera Pinda!

   Delete
 6. Hata hao waliofungua kesi huko mahakamani wamekurupuka sana kwani wamesahau kuwa mbunge akiongea bungeni anakinga.Hao mawakili wenzangu wamepotoka.

  ReplyDelete
 7. Waache tu wanatetea ajira zao. Watatoa taarifa gani kwa wafadhili wao wa hizo NGO zao? Wewe hujui wabongo nini? hapo ndio wako kazini hasaa! Si wanatengeneza pesa hata kwa kutumia majina ya albino, yatima na wakimwi ili mradi tu wana NGO zinazowatajirisha

  ReplyDelete
 8. PM Pinda ametangaza vita na Wananchi anopaswa kuwaongoza na siyo kuwatawala. Anaongea lugha ya baba aliyepitwa na wakati: "Nyie watoto mtaniona nikikuta mnachezea gari langu".
  Alipaswa ajiudhuru mapema. Au Rais angemfukuza kazi mara moja.

  ReplyDelete
  Replies
  1. Hafukuzwi kazi wala haiuzulu mpaka muda wake utakofikia ukomo. Ukivunja kanuni za nchi utapigwa tu. Nchi ni ya amani na upendo. Usjione kuwa wewe tu ndiye mwenye haki ya kuishi nchi hii na kutenda utakavyo. Kuna wananchi wengi wanaohitaji ulinzi wa dola. Hakuna serikali yoyote ile hata kama itaundwa na mtu mpole kiasi gani itakayoacha mambo yaende hatakavyo yenyewe. Pole sana Pinda. Tupo pamoja!

   Delete
 9. Mizengo Peter Pinda, amechemsha kwani hawezi kusema mimi na wewe tupigwe tu. Hajua kuwa anaowangoza ni watu tena wengine wame mchangua yeye akawa mbunge wao na leo amewageuka wapigwe tu.


  Hii yote kwa sababu yeye ameshakuwa waziri na anaona yupo juu ya sheria.mimi naipongeza sana kituo cha haki ya binadamu LHRC na TLS kwa kutuongoza watanzania kumpeleka mahakani Pinda ili ajue kuwa cheo ni dhamana.

  ReplyDelete
 10. kiongozi huyu PINDA hatufai kabisa katika wakati huu wa kujali haki za binadamu.pia hafai kabisa kuitwa kiongozi katika TANZANIA ya sasa maana anakauli tata sana na hakuna kabisa jambo alilosimamia yeye kwa jamii ya watanzania likawa na sura ya kitaifa;
  1.MGOGORO WA MADAKTARI
  2.MGOGORO WA KUCHINJA(geita)
  3.MGOGORO WA GESI
  migogoro yote hii imepoteza maisha ya watanzania wenzetu wengi sana na yeye ni chanzo cha vifo hivyo. alishindwa kushawishi na kutatua mgomo wa madaktari na kusababisha vifo.
  alishindwa kutatua tatizo hili na kuliacha hewa mpaka kifo cha mchungaji kikatokea na hadi sasa wakristo wanadai haki yao kuchinja akiwa waziri mkuu anasema watu waendelee na utaratibu wa zamani, wakati nchi inaongozwa kwa sheria na sio mazoea
  Gesi ya mtwara; na DAMU ya waliouawa hiwe juu yake maana aliwaambia watanzania ametatua suala la gesi wakati si kweli anaendelea kusema uongo kuhusu viwanda kule mtwara wakati hakuna hata kiwanda kimoja wakati amenadi katika vyombo vya habari vipo viwanda 45 vitajengwa. kauli zake ni kupinda pinda kama jina lake lilivyo. kweli ana haki ya kupelekwa mahakamani kwa mdomo wake.

  ReplyDelete
 11. Mnatengeneza migogoro ili mhurumiwe. Hakuna, hakuna! Hakuna hiyo.

  ReplyDelete