17 July 2013

WIZI WA UMEME TANESCO: KWAWAKA


 SIKU moja baada ya gazeti la hili toleo la jana kuibua hujuma za wizi wa umeme kwenye minara ya simu za mkononi, Serikali imeiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na menejimenti ya shirika hilo, kushughulikia haraka suala hilo na kupelekewa majibu haraka.
Wakati Serikali ikitoa agizo hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, Jenerali Mstaafu Robert Mboma, amethibitisha kuwepo kwa vitendo vya wizi kupitia minara ya simu ambao ameshuhudia mwenyewe.
Akizungumza na Majira kwa njia ya simu jana, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema wizara imeiagiza Bodi na Menejimenti kufuatilia na kutoa taarifa Serikalini.

"Tumeielekeza Bodi ifuatilie suala hilo na baadaye itatupa majibu," alisema Profesa Muhongo. Alipoulizwa kuhusu taarifa kwamba kuna ofisa mmoja wa TANESCO amesimamishwa kazi kutokana na kadhia hiyo, Profesa Muhongo, alisema yeye kwa upande wake hizo taarifa hana Kwa upande wake Jenerali Mstaafu Mboma, alisema ni kweli wizi upo kupitia minara ya simu kwa kuondoa seal (alama) na kuweka zingine na wakaguzi wa TANESCO wakienda wanaona umeme unatumika kama kawaida. "Ni kweli TANESCO inaibiwa kwa kutumia njia za kuondoa seal," alisema na kuongeza; "Katika ofisi zetu seal namba 34 ilitakiwa iwe stoo, lakini tayari amekamatwa nayo mtu mmoja akiikodisha." Aliongeza kuwa katika stoo ya shirika zimepotea Playa Power 1,700 pamoja na waya ndogo ndogo 11 zinazotumika kuunganisha umeme, hivyo wanaendelea kufanya uchunguzi kubaini wahusika. Jenerali Mstaafu Mboma alisema tayari wamefanya ukaguzi katika baadhi ya minara ya Gongo la mboto na kubaini kuwepo kwa wizi huo, hivyo uchunguzi zaidi unaendelea. "Ni mapema mno kutaja kampuni ambazo tumebaini hadi uchunguzi kamili ukakamilike na sisi kutoa taarifa," alisema. Al i p o u l i zwa k ama k u n a wafanyakazi wamechukuliwa hatua kuhusiana na sakata hilo, Jenerali Mstaafu Mboma alisema kwa sasa ni mapema mno kuzungumzia hilo,lakini watakaobainika kuhusika kwa namna moja au nyingine hatua za kisheria zitachukuliwa. Alisema kwa sasa wanaendelea na ukaguzi wa kina kwenye minara.
Uchunguzi uliofanywa na Majira umebaini kuwa shirika hilo limekuwa likipoteza mabilioni ya fedha kupitia minara ya simu za mkononi. Wizi huo wa fedha umekuwa ukifanyika kupitia minara inayomilikiwa na kampuni binafsi (jina tunalo) isiyopungua 1,470 nchi nzima kutokana na kuwa na mfumo usio wa kawaida wa kusoma umeme. Minara hiyo ambayo hutumika kuwaunganisha Watanzania nchi nzima, inadaiwa kutumia umeme unaogharimu zaidi ya sh. milioni 70 kwa mwezi kwa kila mnara, lakini TANESCO imekuwa ikilipwa sh. milioni 1.5 hadi 2 tu.

1 comment:

  1. mashirika mengi ya umma yanajiendesha kifisadi,mwisho wa siku yanapata hasara na kufa. kwa TANESCO huwa wanakimbilia kuongeza gharama za umeme BADALA YA KUFA wakisema kwamba wanapata hasara kumbe wanajiibia wenyewe. kuanzia sasa hatutakubali ongezeko lolote la gharama za umeme mpaka hapo mtakapotuthibitishia na pia tutakapojiridhisha kwamba watumishi wa TANESCO wameacha kuiba umeme WANAOZALISHA NA KUUSAMBAZA.

    ReplyDelete