Na Livinus Feruzi, Bukoba
WAFANYAKAZI wa
Serikali Kuu na Afya kote nchini, wametakiwa kuacha tabia ya kuomba na kupokea
rushwa mahala pa kazi na badala yake watekeleze wajibu wao kwa kufuata kanuni,
taratibu na sheria za kazi.
Kauli hiyo
ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya
Tanzania (TUGHE), taifa Bw. Ally Kiwenge wakati akizungumza na viongozi wa
chama hicho na wafanyakazi wa idara ya afya, katika ziara yake ya siku moja
aliyoifanya kwenye Wilaya za Muleba na Bukoba.
Bw.Kiwenge alisema
kuwa w a n a c h a m a w a TUGHE wakiwamo watumishi wa hospitali, mahakamani,
magerezani na polisi wanalalamikiwa kwa kula rushwa mahala pa kazi na kuwa
tatizo hilo litasimamiwa na chama hicho ili kuondoa aibu iliyopo hivi sasa.
"TUGHE
haiwezi kuwa kichaka cha kuficha walarushwa, wazembe kazini, makatibu wa mikoa
simamieni hili kuanzia ngazi za matawi hakuna anayeweza kujificha kwa kula
rushwa asitambuliwe," alisema katibu huyo wa TUGHE taifa.
Alisema kuwa,
pamoja na kuwa wanawahimiza waajiri kuwalipa waajiriwa stahili zao, lakini pia
lazima waajiriwa watimize wajibu wao kwa mujibu wa taratibu na kuwa TUGHE haipo
kwa ajili ya kuchochea migogoro kazini, bali kuleta maelewano kwa pande zote.
Akizungumza na ujumbe wa TUGHE ofisini
kwake, katibu tawala wa Mkoa wa Kagera, Bw. Nassor Mnambila alikiri kuwepo kwa
malalamiko ya wananchi kuombwa rushwa na watumishi na kuwa serikali inajitahidi
kukabiliana na kero hiyo.
Bw. Mnambila alisema kuwa mbali na hilo
pia kuna baadhi ya viongozi wa vyama vya wafanyakazi ambao wanajifanya kama
viongozi wa vyama vya siasa na kusababisha uchochezi wa migororo mahala pa
kazi, ambapo aliwataka kubadilika.
Awali, akisoma taarifa ya TUGHE, katibu wa
chama hicho Mkoa wa Kagera, Bw. Mwisa Edward alisema kuwa, wanakabiliwa na
tatizo la kutokuwa na vitabu vya sheria na migogoro baina ya wafanyakazi na
waajiri inayotokana na kuchelewesha stahili zao.
Alisema kuwa, kwa sasa TUGHE Kagera
ina wanachama 2,285 na kuwaomba watumishi wa Serikali Kuu na Afya ambao bado
hawajajiunga na chama hicho kujiunga ili kuwa na sauti ya pamoja katika kudai
masilahi yao.
No comments:
Post a Comment