17 December 2012
Kauli ya Rais Kikwete itekelezwe kwa vitendo
Na Rose Itono
IMEKUWA ni jambo la kawaida kwa taasisi za fedha kutoa mikopo kwa riba kubwa na kufanya wananchi wa kipato cha chini kushindwa kumudu.
Hii ni kutokana na mikopo mingi inayotolewa na taasisi hizo kuwa na riba kubwa kiasi cha kufanya wananchi wa hali ya kawaida kushindwa kuzitumia fursa hizo.
Hali hii imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa kuongeza umaskini kwa wananchi wengi kwa kushindwa kuzitumia nafasi wanazopata katika kuchukua mikopo na kujiendeleza katika biashara kutokana na kuwa na riba kubwa.
Kutokana na hali hiyo hali ya umaskini katika nchi umekuwa ukiendelea kuwepo na kufanya watu kuendelea kudidimia kiuchumi kwa kushindwa kuendeleza biashara zao kwa kukosa mitaji.
Kutokana na hali hiyo ni lazima taasisi za fedha zikazingatia hali halisi ya kipato cha wananchi wa kawaida na kupanga kiasi cha riba ambacho kitawezesha kuisaidia jamii kubwa kunufaika na fursa za mikopo na kuwezesha kukua kiuchumi.
Hivi karibuni tumeshuhudia Rais wa Jakaya Kikwete akizitolea uvivu taasisi zote za fedha nchini zinazotoa mikopo yenye riba kubwa kutoa mikopo kwa riba nafuu kwani riba ya asilimia 18 inayotolewa na taasisi hizo ni kubwa na inawafanya walalahoi kushindwa kutumia fursa hizo.
Alitoa kauli hiyo wakati akizindua mradi wa nyumba za gharama nafuu zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika eneo la Kibada jijini Dar es Salaam.
Anasema kupunguza riba katika mikopo kutasaidia kupunguza rushwa katika maeneo yao ya kazi ili kupata fedha za kufanyia maendeleo.
Kwa kuliona hilo nampongeza Rais Kikwete na kusisitiza kuzitaka taasisi zote kulifanyia kazi agizo hilo ili kuweza kuinua uchumi wa watanzania wengi.
Mbali na kuinua uchumi huo pia kupungua kwa riba kutawawezesha wananchi hata wale wanaofanya biashara za kuuza maandazi kuongeza mitaji ikiwa ni pamoja na kuanzisha biashara nyingine zitakazowasaidia kukuza kipato chao.
Rais alisema haridhishwi na kasi ya benki katika utoaji mikopo na kusema hadhani kama zinakopesha watu wa hali ya chini na ndiyo maana watu hawakopi kutokana na kutojua.
Nionavyo ni kweli kwani asilimia kubwa ya wananchi wa kipato cha chini wamekuwa wakishindwa kuzitumia fursa za mikopo zinazotolewa na benki kutokana na masharti magumu ya ukopaji.
Ni ukweli usiopingika asilimia kubwa ya mabenki hukopesha watu kwa kutumia dhamana za mali zisizohamishika zikiwemo hati za nyumba mashamba na viwanja kitu ambacho walalahoi si nafasi yao kufika huko.
Kwa mabenki kufanya hivyo ni wazi kuwa wapo nchini kwa ajili ya kuneemesha wachache wenye uwezo na kuendelea kuwaacha maskini wakihangaika pasipo kujua kwa kukimbilia.
Hii imekuwa ikisababisha watu wa kipato cha chini kutofikiria hata siku moja kukopa benki kutokana na kushindwa kumudu vigezo vya ukopaji ambavyo hutolewa na mabenki mengi.
Hii ni ukweli kuwa umaskini umekuwa ukiendelea kuwakumba wananchi wa kipato cha chini kutokana na kulazimika kukopa pesa kutoka kwa watu binafsi tena kwa riba kubwa.
Nionavyo tabia ya baadhi ya watu wenye fedha kutoa mkopo wa 100,000 kwa 150,000 mpaka 200,000 kwa mwezi ni sawa na kumuongezea mkopaji mzigo ambao humfanya kuendelea kubaki maskini.
Ifike wakati sasa kwa wananchi wenye uwezo kuona ipo kila sababu ya kusaidiana na kukopeshana kwa riba ndogo ili kila mtu aweze kuinua kipato chake na kuweza kupata fedha za kukuza mtaji wake.
Nionavyo kupungua kwa riba katika tasisi zinazojishughulisha na utoaji mikopo kutawezesha watu wengi kuzitumia fursa hizo na kuendesha biashara na kujiongezea kipato.
Hivyo pamoja na yote ni vema pia wananchi wakabadilika na kuitumia mikopo wanayopata kwa ajili ya kundeshea biasahara na si vinginevyo kwani kuna baadhi huchukua mikopo na kufanyia mambo .
0655930221
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Katika uhalisia utaona ni asilimia 18 lakini ukweli ni kwamba kuna taasisi ambayo riba ni asilimia 27 kiasia ambacho ni kikubwa sana,mfano NMB Unapojaza fomu inaonekana asilimia 18 lakini ukifanya hesabu za kifedha ni asilimia 27 kiwango kinachoonesha wananchi wasiojua hesabu za kifedha wanaibiwa kwa kuwekewa mzigo wa riba
ReplyDelete