15 January 2013

Diwani CCM afikishwa kortini akihusishwa na mauaji MusomaNa Raphael Okello, Musoma

WATU wanne akiwemo Diwani wa Kata ya Mugango, kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Wandwi Kunju (34), mkazi wa Mugango, Wilaya ya Butiama, mkoani Mara, jana wamefikishwa mahakamani akidaiwa kujihusisha na mauaji ya mtu mmoja.


Bw. Kunju alifikishwa katika Mahakama ya Mkoa huo, mbele ya Hakimu Faisal Kahamba, ambapo Mwendesha Mashtaka Jonas Kaijage, alidai kuwa mtuhumiwa ambaye pia ni mfanyabishara katika Mtaa wa Rwamlimi, Manispaa ya Musoma na wenzake watatu walifanya mauaji hayo Desemba 2,2012.

Aliwataja watuhumiwa wengine kuwa ni Ndalo Mabuse, kwa jina maarufu 'Amir Lonaldo' (27), ambaye ni mkulima wa Kijiji cha Kwibara, wilayani Butiama, Msiba Maregesi (50), mkazi wa Kwibara Mugango na Abeid Kazimili (41), mkulima wa Mugango.

Aliongeza kuwa, watuhumiwa wote walifanya mauaji hayo usiku katika Kijiji cha Kwibara wilayani Butiama nyumbani kwa Tabu Makanya.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya mauaji hivyo iliahirishwa hadi Januari 28 mwaka huu, wakati upelelezi ukiendelea.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Tarime-Rorya, linamshikilia mkazi wa Mtaa wa Nyamisangura, mjini Tarime Bi. Prisca Mwita (22), akituhumiwa kumuua mtoto wake mchanga Happy Anthony kwa kunyofoa baadhi ya viungo vyake.

Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Justus Kamugisha, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo Januari 11 mwaka huu, saa mbili asubuhi nyumbani kwa mwanamke huyo Tarime Mjini.

Alisema mtoto Anthony alikuwa na umri wa miezi 11 na alipoteza maisha baada ya kukatwa sikio la kushoto, kunyofolewa nywele upande wa kushoto, nyusi za jicho la kushoto na kumchuna
ngozi ya kichwa sehemu ya kushoto.

“Majirani ndio waliogundua unyama huo na kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, mtuhumiwa amefikishwa mahakamani jana...baadhi ya wananachi wamelihusisha
tukio hili na imani za kishirikina,” alisema.

Katika tukio jingine, mkazi wa Bunda Mjini, Makuru Laurent (18), amejeruhiwa vibaya mdomoni, kupoteza  baadhi ya meno, kipande cha ulimi baada ya kulipukiwa na baruti ambayo inadaiwa aliitengeneza mwenyewe.

Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Abisalom Mwakyoma, alisema tukio hilo lilitokea juzi, saa 3:00 asubuhi katika eneo Bunda Stoo, wakati Bw. Laurent akiwa nyumbani kwao.

“Baruti hii aliitengeneza kwa kutumia spoku za baiskeli, unga wa njiti za kibiriti na kuunganisha kwenye betri ya pikipiki ambayo alikuwa nayo nyumbani,” alisema Kamanda Mwakyoma.

No comments:

Post a Comment