11 March 2013

Vigogo 6 polisi wasimamishwa *Dkt. Nchimbi afichua tuhuma nzito dhidi yao *Wadaiwa kupokea rushwa, kubambikia kesi *Wengine wabadili vidhibiti dawa za kulevya


Na Rehema Maigala

WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imewasimamisha kazi maofisa sita wa Jeshi la Polisi nchini kwa tuhuma mbalimbali
za ukiukwaji wa maadili na taratibu za jeshi hilo.


Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Emmanuel Nchimbi, alisema mwaka 2012, Wizara hiyo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, waliunda timu iliyokuwa ikichunguza mambo maovu waliyokuwa wakiyafanya.

Alisema tuhuma zinazowakabili maofisa hao ni kubadili kidhibiti cha dawa za kulevya zilizokamatwa mjini Tunduma, mkoani Mbeya, kuwapiga na kuwabambikia wananchi kesi zisizo na dhamana baada ya kupewa rushwa na kujipatia fedha ili kutoa ajira za polisi.

Tuhuma nyingine ni kungia katika Hifadhi ya Wanyama Serengeti, mkoani Mara na kupanga njama za kuchimba madini ya dhahabu ndani ya hifadhi hiyo kinyume cha sheria.

Dkt. Nchimbi alisema, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi aliyekuwa anasimamia ajira ya jeshi hilo, Renatus Chalamila, yeye amepewa likizo ya mwezi mmoja ili Ofisi ya Rais ichunguze kwa undani tuhuma ya kujipatia rushwa kwa vijana waliokuwa
wanataka kujiunga na ajira za Jeshi la Polisi nchini.

“Kuruta 95, tumewaondoa katika mafunzo ya ajira za polisi baada ya kubaini wameingia kwa kutumia rushwa hivyo hatuwezi kupokea askari walioingia katika ajira kwa rushwa...hali hii itawafanya waendeleze rushwa kwa kila kitu wanachokitaka wanapokuwa
katika kazi zao na kuleta sifa mbaya kwa jeshi,” alisema.

Aliongeza kuwa, maofisa wengine waliosimamishwa ni Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Elias Mwita, aliyekuwa Mkuu wa Upepelezi mkoani Mbeya, Mrakibu wa Polisi, Jacob Kiango, ambaye alikuwa Msaidizi wa Mkuu wa Upelelezi mkoani humo na Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Charles Kinyongo, aliyekuwa Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), mkoani humo.

“Maofisa hawa wanatuhumiwa kubadili kidhibiti cha dawa za kulevya yaliyokamatwa mjini Tunduma, mkoani Mbeya, ambayo
baada ya kuletwa Dar es Salaam kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi zaidi, majibu yalionesha hazikuwa dawa
halisi za kulevya bali ni chumvi na sukari,” alisema.

Dkt. Nchimbi alifafanua kuwa, watu waliokamata na dawa hizo, walikataa majibu yalitolewa na Mkemia Mkuu na kuomba hiyo sukari na chumvi, virudishwe tunduma na walivyoviona walisema dawa walizokamatwa nazo zimebadilishwa.

Alisema katika uchunguzi wa awali, ilibainika kuwa dawa hizo zilikuwa aina ya Cocain, kilo 1.9 ambapo vitendo viovu ambavyo vinafanywa na maofisa wa jeshi hilo, vinawavunja moyo askari
wa ngazi ya chini ambao watashindwa kazi zao kwa uadilifu.

Katika hatua nyingine, Dkt. Nchimbi alisema Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Peter Matagi, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kagera, naye amesimamishwa kazi na atafunguliwa mashtaka ya kijeshi kwa kuwabambikia kesi watu 13 na kuwaweka mahabusu
miezi miwili akidai ni majambazi sugu waliokamatwa na silaha.

“Kimsingi hawa mahabusu hawakuwa majambazi sugu bali walikuwa walikuja mjini Dodoma kunitafuta mimi ili kutoa malalamiko yao juu ya tajiri mmoja ambaye alikuwa anamiliki shamba lenye ekari 4,000.

“Wanakijiji walimtaka tajiri huyu alirudishe shamba hilo lakini alikataa hivyo wawakilishi wa wananchi hawa waliamua kuja Dodoma ili kunitafuta ni kinieleza kilio chao lakini walikamatwa
na polisi waliodai watu hao ni majambazi sugu waliokuwa
wakitafutwa muda mrefu,” alisema.

Aliongeza kuwa, baaada ya kupata habari za kukamatwa kwa watu hao, mjini Dodoma, alimpigia simu Kamanda wa Polisi mkoani humo na kumwambia, anahitaji kuonana na watuhumiwa ambao inadaiwa walikamatwa na silaha afanye nao mazungumzo
katika Hoteli ya Dodoma.

Alisema Kamanda wa Polisi alitekeleza agizo hilo na aliweza kukutana na watu hao ambao walimweleza malalamiko ambayo walitaka kumueleza kabla hawajakamatwa na kuamua kuunda
tume ambayo yeye aliiongoza kama Mwenyekiti.

Dkt. Nchimbi alisema tume hiyo ilibaini kuwa, watu hao hawakuwa majambazi sugu na hawamiliki silaha,” alisema na kuongeza kuwa, askari yeyote ambaye atakaye fanya vizuri, atalindwa na yule ambaye atakiuka sheria, atachukuliwa hatua stahiki.

Mwingine aliyesimamishwa ni SSP Paul Mng'ong'o, kwa kosa la kuingia katika Hifadhi ya Serengeti na kupanga njama za kuchimba madini ya dhahabu na kusababisha kiongozi huyo ashtakiwe kwenye mahakama ya kiraia huko Serengeti.

2 comments:

  1. Napenda kumpongeza waziri wa mambo ya ndani ya nchi kwa ujasiri anaoanza kuonyesha dhidi ya kukemea maovu na kuangalia usalama wa wananchi na haki zao

    Mbali na pongezi hizo kuna sehemu imenigusa kama mzazi kule kuwafukuza wanafunzi walio kwenye chuo cha polisi pale Moshi inaniuma kidogo

    Ni ukweli usiofichika kuwa wametoa rushwa ili kupata ajira katika soko la ajira ambalo limekuwa gumu mahali pote siyo kwa wazawa watanzania tu hata mataifa mengine wamejazana kwenye nchi yetu kutafuta ajira na juu ya kuishi.

    Kwanza naomba ieleweke wazazi wa wamewasomesha watoto wao hadi labda chuo kikuu na na baadhi wanawaona watoto wao wanaishia kwenye vijiwe kwani hakuna sera kamili ya kuwasaidia vijana hao wanapomaliza shule na kuwapa upendeleo kwenye soko hilo la ajira kama wazawa/watanzania

    Ukienda kwenye mataifa mengine kama ya magharibi kuna kaupendeleo hasa kwa mzawa wa nchi husika na ni vigumu kuona mtu mwingine wa taifa lingine anapata kazi kabla ya mzawa

    Nchi yetu sasa inakwenda mahali kuwa kama huna mtu unayemjua hakuna ajira AJIRA NYINGI HASA SECTA BINAFSI ZIMESHIKWA NA WAGENI MBALI NA WAZAO WENYE ELIMU NZURI YA VYUO VIKUU,aidha ili upate ajira pengine lazima utoe kitu kidogo ndio jina lako lifiriwe kwenye ajira husika.

    Mbali na ajira kuna mambo mengine yamekuwa mabaya zaidi hasa kwenye elimu , mzazi amejidhiki amemsomesha mtoto wake hadi chuo kikuu linakuja swala la cheti , vyuo vinasema/ chuo kinasema hakina/ havina vyeti kweli inaingia akilini hiyo mheshimiwa waziri naomba uchunguze hili

    Hakuna mtu anaweza kuajiriwa bila cheti lakini ukifuatilia cheti chuoni unaambiwa njoo kesho kesho na mwajiri anataka kuona cheti chako mzazi ufanyeje ukitoa rushwa kumpa mkuu wa chuo ni makosa ukikamatwa ni haya ya mheshimiwa Mchimbi je tutafika kweli

    Naomba mheshimiwa Mchimbi kama kweli umeamua kulifanyia kazi hili basi uamue kuoga kabisa kwani kuna mengi yanawakera wananchi.

    Cheo chako ni dhamana kwa taifa lako na uadilifu wa sehemu uliyowekwa ni heshima kwako na kizazi chako kama mawaziri wengine waliofanya kweli
    wanavyheshimika, ikiwa ni pamoja na mawaziri waliouacha ubinafsi na kulihudumia Taifa kama waziri wa uchukuzi mheshimiwa Mwakyembe, waziri wa ujenzi Mheshimiwa Mgufuli nk

    Nakutakia kila la kheri katika kulinda heshima ya Raisi Kikwete na uongozi wote wa chama kwa maana hiyo nawaombea radhi hao wanafunzi walioangukiwa kwenye mtego huo ambao ni sawa na wezi wa elimu, na watakaoangukia kwenye mtego kama huo kwani makosa yako juu,

    Mheshimiwa baba wa Taifa marehemu Julius K Nyerere aliwahi kusema mwizi wa elimu na mbolea siyo wezi ,hadithi hiyo ni sawa na hawa wanafunzi wanaotakuta ajira kwa nguvu zote wakihitaji na elimu ili wawahudumie watanzania na ili wasiwe kupe

    Naomba uwashughulikie hawa viongozi wanaopokea zaidi kwani wana mishahara yao na marupurupu mazuri tu.

    Mungu ibariki Tanzania na watu wake

    ReplyDelete
  2. Mh nchimbi hongera sana kwa ujasiri wako lakini tunawataka mfahamu kwamba Tanzania sasa hivi kazi katika mashirika na hata serikalini si mali ya masikini bali na kwa ajili ya watoto wa vigogo.Hao uliowafukuza ni matunda ya mfumo uliopo sasa ambao kwa kipingi kirefu serikali imekua ikiutazama huku kukiwa na juhudi hafifu kuutokomeza.Umewafukuza watoto wa masikini na wakulima wadogowadogo ambao kiukweli kama wangetaka wafuate taratibu za ajira hakika wasinge pata hizo nafasi.Hao ni watoto wa masikini kwani tunapaswa kujiuliza upolisi una maslah gani hata mtu ahonge?Tanzania inanuka kwa rushwa tena za wazi wazi lakini sababu ni vigogo waliomadarakani wanapeana kazi kindugu,kikabila na kufahamiana.Tunahitaji uwajibikaji,tunahitaji heshima ya Tanzania ya hayati baba wa Taifa erejee ilivyo kua,tumechoka na hawa wanyang'anyi wasio na huruma kwa uma wa watanzia,tunahitaji adhabu kali ichukuliwe dhidi ya hawa wanyanyasaji.

    ReplyDelete