12 March 2013

Serikali iwasaidie wajasiliamali kwa kuwapa mafunzo




KUJIAJIRI ni suala linalopewa kipaumbele na mamlaka
mbalimbali nchini pamoja na mataifa yaliyoendelea.


Mabadiliko makubwa katika mifumo ya uchumi, yamechangia
wananchi wengi kukosa kazi za kuajiriwa ambapo ajira binafsi


ndizo zinazoonekana kushika kasi katika maeneo mengi.



Nchini Tanzania, idadi kubwa ya wananchi wameamua kujiajiri wenyewe wakiwemo wastaafu kwa kufungua vitega uchumi mbalimbali
 pamoja na kufanya biashara ndogondogo ili
waweze kujipatia kipato. Cha kukidhi mahitaji yao.


Kujiajiri katika biashara ni jambo jema lakini sisi tunaona kuwa, tatizo kubwa linalowasibu wadau wengi wanaofanya shughuli hizo ni kukosa mafunzo ambayo yatawawezesha kuendesha biashara pamoja na kukuza mitaji yao.

Wafanyabiashara wengi nchini hawabadiliki kwa sababu shughuli wanazofanya ni zile za mazoea bila kuwa na ujuzi wa namna ya kuziendesha hivyo upo umuhimu wa Serikali, kubeba jukumu
hilo ili kuwawekea msingi mzuri wa maisha.



Baadhi ya wastaafu waliopewa viinua mgongo na kuwekeza kwenye biashara, wanakabiliwa na wakati mgumu wa kutafuna mitaji yao kwa sababu ya kufanya biashara zisizoendelea.

Wanaofanya biashara ya kuuza maandazi na vitumbua, hawana mtazamo wa kutunza ziada wanazopata kwa kufungua akaunti bali wanachokipata kinakwenda tumboni bila kujua senti 50 inayobaki, ilipaswa kuwekwa akiba ili kuendeleza biashara zao.



Hili ni jambo hatari sana, wafanyabiashara kama hawa mbali ya kufanya biashara hizo kila siku, bado wataendelea kubaki maskini bila mafanikio yoyopte kama Serikali haitachukua hatua za haraka kuwasaidia kwa kuwapatia mafunzo ya kuendesha biashara zao.


Ni wajibu wa Serikali na wadau wengine, kutambua kundi hili ni watu wenye vipato vidogo na vile vya kati ambao hawawezi kulipa maelfu ya pesa kugharamia mafunzo ya uendeshaji biashara.


Wito wetu kwa Serikali ibuni mkakati wa kushirikisha wadau wengine na kuandaa mpango maalumu wa kutoa mafunzo ya usimamizi na uendeshaji shughuli za ujasiriamali bure
kwa
wananchi waishio mijini na vijijini.



Kwa kufanya hivyo, italeta mwamko kwa wajasiriamali kujua namna ya kuendesha shughuli zao na kuwapa ubunifu zaidi
wa biashara mpya tofauti na sasa.



Hivi sasa, wajasiriamali wengi wanafanya biashara kwa kumwiga mwenzake, utakuta kila mahali biashara ni saloon, grosari, maduka ya dawa, chakula na nguo. Je, hivi hizi ndio huduma pekee wanazohitaji wananchi?

No comments:

Post a Comment