04 December 2013

...ZANZIBAR HEROES YAAGA MASHINDANO Na Mwandishi Wetu, Nairobi

Wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Chalenji inayoendelea nchini Kenya ya Zanzibar Heroes, jana imetolewa kwenye kinyang'anyiro hicho baada ya kuzabwa na Kenya 'Harambee Stars' mabao 2-0 kwenye mechi iliyochezwa jana mjini Nakuru.


Kwa matokeo hayo, Kenya imeungana na timu za Ethiopia na Jamhuri ya Sudani kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo yanayosimamiwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Mpira ulianza kwa kasi kwa timu zote kushambuliana kwa zamu lakini, Kenya ilipata bao la kwanza dakika ya tatu kupitia kwa Jockins Atudo kwa mkwaju wa penalti, baada Mohamed Faki kumuangusha Francis Kahata katika eneo la hatari ndipo mwamuzi Wish Yabrow toka Somalia akaamuru ipigwe penalti.

Baada ya bao hilo, mpira uliendelea kwa nguvu huku wachezaji wa Kenya wakitumia nguvu nyingi ili kuwachanganya vijana wa Zanzibar . 
Zanzibar Heroes ilifanya shambulizi kali dakika ya nane langoni mwa Kenya na kupata faulo iliyopigwa kwa shuti kali na Chile, lililopanguliwa na kipa wa Kenya na mpira kuokolewa na mabeki.

Dakika ya 18, Jacob Terry aliwapangua mabeki wa Zanzibar na kupiga shuti kali lililopanguliwa kwa ustadi na kipa Abdallah Rashid.

Kipindi cha pili Harambee Stars iliingia kwa nguvu kutaka mabao zaidi ambapo dakika ya 54, Alan Wanga aliipatia timu hiyo bao kwa mkwaju mkali uliomshinda kipa Rashid.

Zanzibar Heroes ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Hamis Mcha 'Vialli' na kumuingiza Ali Ali kwa ajili ya kuongeza nguvu kwa upande wa ushambuliaji.

Hata hivyo mabadiliko hayo hayakuweza kuisaidia Zanzibar kwani Kenya waliendelea kulichachafya lango la wapinzani wao, lakini kipa Rashid alikuwa imara kupangua mashuti ya Mwanga na John Opio, waliokuwa wakiunganishwa vyema na Kahata aliyekuwa akihaha uwanja mzima.

No comments:

Post a Comment