11 March 2013

Hali ya Kibanda sasa yaimarika *Taya, meno vyafungwa waya maalumu


Na Mwandishi Wetu

HALI ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), Bw. Absalom Kibanda, inaendelea kuimarika baada ya kufanyiwa oparesheni ya kuondoa jicho la kushoto na kurekebisha taya.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Katibu wa TEF, Bw.
Neville Meena, ilisema jana Bw. Kibanda alionekana kupata
nafuu kubwa kuliko ilivyokuwa siku za nyuma.

Alisema sura yake imeanza kurejea katika hali ya kawaida na   uvimbe wa damu zilizokuwa zimevilia ndani zimepungua ambapo  kuzungumza kwake kumewapa matumaini wanaomuuguza katika Hospitali ya Millpark, iliyopo Johannesburg nchini Afrika Kusini.

“Katika operesheni aliyofanyiwa, taya ya kushoto na meno ambayo yalibainika kupata mshtuko, yamefungwa waya maalumu ili yaweze kujerea katika hali ya kawaida,” alisema Bw. Meena.

Aliongeza kuwa, baada ya kuondolewa jicho hilo litawekwa la bandia ambalo halitamwezesha kuona ambapo madaktari ambao wanamtibu, walisema jicho hilo litawekwa baada ya kupona
jeraha alilopata.

Bw. Meena alisema, upasuaji aliofanyiwa Bw. Kibanda ni wa kitaalamu zaidi usiotumia kisu kigusa ngozi yake bali madaktari walitumia matundu ya pua kutatua matatizo yanayomkabili hivyo hakuna majereha yoyote yaliyotokana na upasuaji huo.


“Kwa sasa ndugu yetu Kibanda anaendelea na matumizi ya dawa akiwa chini ya uangalizi wa madaktari na wauguzi wa hosipitali
ya Millpark...hiki ni kipindi kigumu katika tasnia yetu ya habari, tuendelee kumuombea aweze kupona haraka,” alisema.

No comments:

Post a Comment