28 February 2013

Ukatili wa aina hii usipewe nafasi



GAZETI moja linalochapishwa kila siku (sio Majira) jana liliripoti habari ya kusikitisha iliyoelezea kwa kina ukatili aliofanyiwa biti wa miaka 16 (jina linahifadhiwa).

Binti huyo alitekwa nyara na vijana watatu waliomfungia ndani kwa miezi mitatu.

Kwa mujibu wa habari hiyo binti vijana hao walimtoa huyo mimba wakitumia majani ya chai. Inadaiwa katika eneo alilofichwa alijengewe mfano wa kaburi ambapo alikuwa analazwa humo, huku juu yake wakiweka godoro ambalo walikuwa wakilitumia kama kitanda.

Kwa ujumla habari hiyo ni ya kusikitisha na kwa lugha nyingine tunaweza kusema ukatili huo ni wa aina yake na tunampa pole binti huyo kwa yaliyomkuta katika kipindi chote.

Lakini inasikitisha kuona kuwa vitendo hivyo vya ukatili vinaendelea kutendeka nchini licha ya elimu ambayo imekuwa ikitolewa na wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu.

Kwa miaka mingi Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) kimekuwa mstari wa mbele kupiga vita vitendo hivyo. Juhudi za chama hicho ndizo zilizosaidia Serikali kutunga ya Sheria kali ya Makosa ya Kujamiia Mwaka 1998.

Pamoja na makali ya adhabu yaliyomo kwenye sheria hiyo, bado Watanzania hawaiogopi na wameendelea kuwafanyia wenzao vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Hii inaonesha wazi kuwa kuna changamoto kubwa mbele yetu ili kuhakikisha vitendo hivyo havitokei.

Hatuwezi kuendelea kujisifia kuwa Tanzania ni kisiwa cha amani wakati watu ndani ya jamii hawana amani. Amani ya nchi haitakiwi kupimwa kwa kuangalia utulivu uliopo kwenye mipaka, bali pia usalama wa watu ndani ya taifa lao.

Kwa hiyo tunatoa mwito kwa Serikali kuwasaka na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale wote wanaojihusisha na vitendo vya kikatili ndani ya taifa letu kwani ni udhalilisha wa utu wa mtu.

Tunataka wanaojihusisha na vitendo hivyo wahukumiwe haraka ili iwe fundisho kwa wingine.  Hatuwezi kukubali kuishi na wahalifu wa aina hiyo kwani ni hatari kwa jamii.

Wakati umefika sasa kwa polisi kuongeza nguvu za kupambana na vitendo hivyo ili kujenga jamii yenye amani na utulivu kwa watu wake.

Pia tunatoa mwito kwa asasi kama vile TAMWA kuongeza kasi ya kutoa elimu kuhusiana na athari za vitendo hivyo kwani bila wao hali ingekuwa mbaya zaidi. Hapo ndipo tunaona umuhimu wa asasi hizo kuongezewa nyenzo.

Tunasema kw akutambua mchango wa chama hicho ndicho kwani ndicho kilichoibua vitendo vya mauaji ya vikongwe mkoani Shinyanga na kusimamia kidete utungwaji wa Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ya Mwaka 1998.

Vyombo vya habari kama wadau wakubwa navyo vina jukumu kubwa vya kuelimisha umma kuhusu madhara ya vitendo hivyo kwani vinaenda kinyume na haki za binadamu. Tanzania bila vitendo vya ukatili inawezekana kinachotakiwa ni kila mtu kutimiza wajibu.

2 comments:

  1. Polisi wa Maeneo hayo hawafai kabisa. Polisi kwa sasa ni 'kimeo' Tanzania. Wanazembea sana na kujinufaisha na kesi za 'mapesa' mengi na kesi za udhalili wa mabinti. UPO USHAHIDI

    ReplyDelete
  2. Serikali yetu ni pambo kama mapambo mengine ya ndani. Vyombo vya dola bora vingeitwa vyombo vya shilingi maana vinazidi kupoteza imani kwa wanainchi kila uchao. Vipo kama geresha tu wala havitimizi majukumu yake. Vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadam zimekuwa zikiongezeka siku hadi siku hii inatupa picha dhahiri kuwa kila mwananchi ajilinde kwa nafsi yake wala asitegemee dola kamwe. Yangu ni hayo tu.

    ReplyDelete