04 March 2013

Bila Serikali kuchukua hatua, vita ya rushwa kamwe haitakomaTATIZO la rushwa nchini lipo katika sekta mbalimbali lakini
hali hiyo haina maana kuwa inakubalika katika jamii.


Ukweli ni kwamba, rushwa haikubaliki kutokana na madhara yake ndio maana Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha vitendo hivyo vinatokomezwa.

Rushwa inaathiri maendeleo ya mtu binafsi, familia, Taifa, kushusha hadhi ya mtoaji, mpokeaji na kuchangia kupindisha kanuni za maadili wakati wa kutekeleza majukumu kwa masilahi ya
umma, mtu au kikundi fulani.

Vitendo hivyo vinajumuisha matumizi mabaya ya madaraka na kusababisha baadhi ya viongozi wa umma na sekta binafsi, kutumia madaraka waliyonayo kinyume cha sheria ili kujinufaisha.

Rushwa imebatizwa majina mengi, wengine huiita mlungula, kitu kidogo, shati la mikono mirefu au zawadi.

Watu wanaojihusisha na vitendo hivyo, wanawanyima wananchi mategemeo ya kuwa na maisha bora, kuwakosesha elimu, huduma bora za afya, chakula, maji na mahitaji mengine ya kibinadamu.

Sisi tunasema kuwa, rushwa ni wizi dhidi ya Taifa na wananchi ambao wanategemea maisha bora, inachochea makosa ya jinai yanayovuka mipaka, kuvunja amani na utulivu.

Rushwa ina madhara makubwa kiuchumi kwa lugha nyepesi ni
uovu unaowavunja moyo Watanzania na wafanyabiashara
ambao wangependa kuwekeza nchini.

Inaongeza ugumu wa maisha kwa wananchi wakati mwingine husababisha kupungua ubora wa bidhaa ambazo huzalishwa viwandani.

Imani yetu ni kwamba, rushwa husababisha mapato ya Serikali Kuu, Serikali za Mitaa kupungua hivyo kupuguza uwezo wa kutoa huduma kwa wananchi ili watekeleze malengo yao pamoja
na kuboresha miundombinu ya nchi.

Uovu wa rushwa unachangia kuongeza umaskini katika jamii, kuathiri ubora wa elimu na sekta nyingine nchini.

Rushwa inaweza kusababisha mgonjwa asipone haraka au kupoteza maisha kama atakataa au kukosa kile alichodaiwa kukitoa.

Tukifikia kiwango cha kuibubali rushwa kama sehemu ya utamaduni wetu katika vyombo vya sheria, waathiriwa wataamua kujilinda wenyewe kwa kuchukua sheria mkononi hivyo kuharibu sifa ya amani na utulivu tulionao.

No comments:

Post a Comment