09 May 2011

Wanachama wadaiwa kuikimbia TABOA

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Wamiliki wa Mabasi yaendayo Mikoani (TABOA) kimesambaratishwa baada ya wanachama wake kujitoa na sasa kubakiwa na mwanachama mmoja tu
, imefahamika.

Mbali ya hatua hiyo, wamiliki hao wa mabasi wamesisitiza msimamo wao wa kukataa kufungwa kwa kifaa cha kuweka kumbukumbu na kufuatilia mwenendo wa magari ‘Car Tracking System’

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa utata kuhusu uongozi wa TABOA ulianza kujitokeza wiki iliyopita kwenye mkutano wa kamati ya ufundi uliokuwa chini ya Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabrani (SACP) Mohamed Mpinga.

Katika mkutano huo uliohusisha viongozi wa TABOA, Chama cha wamiliki wa Mabasi Dar es Salaam (DABOA) na mkandarasi wa mfumo huo, baadhi ya wamiliki walimhoji kiongozi wa TABOA anamwakilisha nani wakati wanachama wote wamejitoa.

Mwakilishi wa TABOA katika mkutano huo alikuwa Katibu Mkuu Wilbert Mtenga ambaye pia anajitambulisha kuwa ni Kaimu Mwenyekiti baada ya kujiuzulu kwa Mohammed Abdullah. Makamu Mwenyekiti alikuwa mmiliki wa mabasi ya Dar Express ambaye kajiengua.

“Mmoja wa wajumbe alimuuliza Mtenga mbele ya Kamanda Mpinga, anawakilisha nani, hakutoa jibu lolote, baadaye alisubiri hadi mkutano ulipomalizika ndipo akazungumza na vyombo vya habari…TABOA kwa sasa haina mwanachama zaidi yake,” kilisema chanzo chetu cha habari.

Alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, Mtenga alisema wanaosema TABOA haina wanachama hawana maana kwa kuwa ina miaka 36 na kuwa anakaimu nafasi hiyo kwa kuwa ameteuliwa na halmashauri kuu ya chama hicho.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa TABOA haina kadi za wanachama na haijawahi kufanya mkutano kujadili mambo yanayowagusa wanachama wote, badala yake ilikuwa ikiendeshwa na kikundi cha watu wachache tu.

Habari zaidi zilisema wamiliki wengi wa mabasi kwa sasa wamejiunga na DABOA ambao watakutana kesho Dar es Salaam kujadili kuhusu ufungaji wa mfumo wa kufuatilia mwenendo wa magari ambao wanadai una harufu ya ufisadi.

Mmoja wa wamiliki hao ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alitoa mfano kuwa basi la kampuni moja linalofanya safari kati ya Dar es Salaam na Mbeya ambalo lilipata ajali juzi maeneo ya Mikumi, mkoani Morogoro licha ya kuwa limefungwa kifaa hicho na kuwa kabla ya hapo lilipigwa 'tochi' na kutozwa sh. 100,000 kutokana na mwendo kasi.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mpinga alisema wameongoza muda wa miezi mitatu ili wamiliki wa mabasi wafunge kifaa hicho na kuwa hadi sasa mabasi 48 ya kampuni 11 tu ndiyo yamefunga wakati lengo lilikuwa mabasi 500.

2 comments:

  1. KAZI YA TRAFIKI IPO WAPI? rushwa ndio tatizo kubwa linalosumbua suala la usafirishaji tz.
    UGONJWA WA AJALI TANZANIA NI UGONJWA MKUBWA SANA KWA TAIFA LETU.
    NANI WA KULITATUA HAKUNA, MAANA WATU WAENDELEE KUFA TU.
    NASHINDWA KUELEWA KAMA KWELI USALAMA BARABARANI UNAFANYA KAZI?
    KWA HIYO NDUGU WANANCHI NAOMBA KUWAKILISHA

    ReplyDelete
  2. Kwa hakika swala la usalama barabarabi bi hasa rushwa na kuwa na sheria ambazo hazimbani mwenye kosa na wanaokufa barabarabi ni kama mnyama mharibifu, hakuna wala fidia wala kesi inayomhusisha mwenye bus, dereva na familia ya marehemu! Sisi tuendelee kufia tu barabarani! Siku serikali itadhubutu kusema imetosha na kuchukua hatua, basi tutapona! zaidi ya hayo barabara zetu ni nyembamba sana kwa idadi ya magari na hakuna njia ya waenda kwa miguu, wala kwa baiskeli! Wote tutajuana njia moja! Tena lazima tuangalie deveva anatoa gari Mbeya hadi Dar peke yake, kwani ni chuma asichoke??? Mwisho ulevi nao unachangia sana! usalama u wapi?

    ReplyDelete