09 May 2011

Madiwani watengua mipaka ya hifadhi

Na Kassian Nyandindi, Mbinga
 
BAADHI ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wametengua mipaka ya Hifadhi ya Liparamba ambayo iliwekwa na Wizara ya Maliasili na
Utalii kwa madai kuwa maeneo wanaoizunguka yaliyokuwa yanataumia kwa kilimo yamechukuliwa.
 
Hatua hiyo ilijitokeza katika kikao cha Baraza la madiwani kilichoketi hivi karibuni katika ukumbi wa Umati mjini humo ambapo mvutano mkubwa
ulijitokeza kati yao na Meneja wa Hifadhi hiyo, Bw. Hashim Sariko ambaye alitoa ufafanuzi wa kisheria kuwa mipaka hiyo isiondolewe.
 
Bw. Sariko alisema mipaka ya hifadhi ya Liparamba iliwekwa kisheria kwa kuzingatia taratibu husika, ikiwemo wananchi wenyewe kushirikishwa na kuridhia wapi iwekwe, hivyo inashangaza kuona madiwani hao wanatilia mkazo kwamba mipaka hiyo inawaumiza wananchi waishio katika kata ya Liparamba.
 
Bw. Sariko alisema madai ya madiwani hao si ya kweli kwani kata hiyo ina maeneo mengi ya wazi, ambayo yanafaa kwa shughuli za kilimo, hivyo viongozi wanapaswa kuwaelimisha wananchi ili waelewe na badala ya
kuendesha migogoro isiyokuwa ya lazima.
 
Alifafanua kuwa madiwani hao wanataka mipaka hiyo iondolewe ili wananchi waingie katika baadhi ya maeneo ya hifadhi na kuendelea na uwindaji haramu kama walivyozoea miaka ya nyuma kabla ya hifadhi hiyo kuwekwa mipaka kisheria.
 
Pamoja na maelezo hayo, bado madiwani walionekana kutoelewa na kufikia maamuzi kwamba mipaka iliyowekwa kisheria na serikali iondolewe
na ufanyike utaratibu mwingine wa kuiweka upya.
 
Hifadhi ya Liparamba iliwekewa mipaka Mei 16, 2000 na kusainiwa na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kwa kuzingatia vigezo maalumu baada ya wananchi wenyewe kuridhia.

1 comment:

  1. Hebu wataalamu tufafanulieni, jee hii inawezekana?

    Kama ni hivyo ina maana mipaka inaweza kutenguliwa tu na misitu kuuzwa bila ya taasisi husika kuhusishwa.

    ReplyDelete