01 February 2011

Dkt. Slaa: Udini ni propaganda ya CCM

*Asema unaibuliwa kufunika udhaifu wa uongozi

Na Tumaini Makene

TATIZO la udini unaodaiwa kuwepo nchini umeelezewa kuwa ni propaganda inayotumika kuficha udhaifu wa kiuongozi ili wananchi waache kujadili
mambo ya msingi ya taifa, ikiwemo chama kilichoko madarakani kushindwa kutekeleza ahadi zake kwa miongo mitano iliyopita.

Imeelezwa kuwa wananchi wa Tanzania wanaendelea kuishi kwa amani, upendo na mshikamano bila kujali tofauti zao za kidini, hivyo viongozi nchini wametakiwa kuacha kuwagawanya Watanzania kwa manufaa yao ya kisiasa.

Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibrod Slaa alipokuwa akisoma tamko la Kamati Kuu (CC) juu ya hali ya siasa nchini na masuala mengine ya kitaifa katika nyanja mbalimbali.

Dkt. Slaa alisema kuwa CC ya CHADEMA imeazimia kuwahimiza viongozi wa dini zote hapa nchini kuendelea kukemea maovu yoyote katika jamii bila woga wala upendeleo kwani hilo ni jukumu lao la msingi.

"Kamati kuu imesikitishwa na propaganda zinazoendelezwa na viongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi, hususan Rais Kikwete, kuhusu kuwepo kwa mfarakano wa kidini hapa nchini. Kamati Kuu imezingatia kuwa wananchi wa Tanzania wameendelea kuishi kwa amani, upendo na mshikamano mkubwa bila kujali tofauti zao za kidini.

"Kamati kuu imezingatia kuwa viongozi wa juu wa CCM na hasa Rais Kikwete, wameamua kuficha udhaifu wake wa kiuongozi chini ya zulia la udini ili wananchi waache kujadili mambo ya msingi ya taifa hili, ikiwemo kushindwa kwa CCM kutekekeza ahadi ambazo imekuwa ikizitoa katika miongo mitano iliyopita," alisema Dkt. Slaa na kuongeza;

"Hivyo basi kamati kuu imewahimiza wananchi wa dini zote hapa nchini kuendelea kuishi kwa amani na mshikamano na kushirikiana katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii, bila kujali tofauti zao za dini, ukabila wala itikadi ya siasa.

"Kamati Kuu imewataka viongozi wa juu wa CCM na hasa Rais Kikwete kuacha kuchochea mgawanyiko wa dini hapa nchini kama njia ya kuficha udhaifu wake wa uongozi...imewahimiza viongozi wa dini zote hapa nchini kuendelea kukemea maovu yeyote nchini bila woga wala upendeleo kwani hilo ni jukumu lao la msingi."

Ushirikiano wa vyama

Kwa mujibu wa Dkt. Slaa aliyesoma tamko hilo katika mkutano wake na waandishi wa habari, alisema kuwa CC ya chama hicho ilitafakari juu ya umuhimu wa ushirikiano wa vyama vya siasa ili kuimarisha nguvu ya upinzani hapa nchini na kumuagiza Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, kuunda baraza kivuli kwa kuhusisha wabunge wa CHADEMA pekee.

"Kamati Kuu imeendelea kuzingatia umuhimu wa vyama vya siasa kushirikiana katika kuimarisha nguvu ya upinzani hapa nchini. Hata hivyo, kamati kuu imezingatia kuwa Chama cha Wananchi (CUF) wamejiunga na CCM kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

"Na kwa kuwa sheria inayoruhusu uwepo wa vyama vya siasa inahusu pande zote za muungano na kwa kuwa vyama vingine vya upinzani vyenye wabunge vimo katika ushirikiano na CUF, Kamati Kuu imeona kuwa CHADEMA haiwezi kuwa na ushirikiano wenye tija na vyama hivyo," alisema Dkt. Slaa.

Akifafanua hatua hiyo, Dkt. Slaa alisema kuwa ni vigumu kwa CHADEMA kuwa na ushirikiano wa CUF, wakati kiko serikalini, kikitimiza majukumu ya kiserikali pamoja na chama kilichoko madarakani sasa, CCM, hivyo ni vigumu kushirikiana na wapinzani ambao tayari ni sehemu ya utawala.

Akizungumza juu ya uwezekano wa CHADEMA kushirikiana na vyama vingine vilivyoungana na CUF katika kile kinachoitwa kamati ya wabunge wa upinzani wasiokuwa katika kambi rasmi, Dkt. Slaa alisema kuwa vyama hivyo navyo vimekuwa sehemu ya watawala kwa sababu vimeungana nao kupitia CUF.

"Sasa kwa mfano tukiazimia kitu kinachopingana na serikali, Katibu Mkuu wa CUF ambaye ndiye Makamu wa kwanza wa Rais huko Zanzibar unategemea atakubaliana nacho ili apingane na serikali, hivi vyama vingine navyo tayari vimeshakuwa sehemu ya watawala maana wameamua kushirikiana na CUF katika kamati yao."

Mchakato wa katiba mpya

Juu ya suala la mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya, CC ya CHADEMA ilipinga utaratibu wa uundwaji wa tume ya rais katika uundaji wa katiba mpya, ikisema si njia sahihi kwa upatikanaji wa katiba mpya yenye utashi, matakwa na mahitaji ya wananchi wa Tanzania, badala yake imeunga mkono utaratibu wa kutumia bunge katika kutengeneza na usimamia mchakato wa kuelekea kupatikana kwa katiba mpya.

Hivyo, mbali ya kuipongeza sekretarieti ya kamati kuu hiyo kwa kumwagiza Bw. John Mnyika (Mbunge wa Ubungo) kuandaa na kuwasilisha hoja binafsi inayolitaka bunge kuandaa sheria kuratibu mchakato wa katiba mpya, imewapongeza pia wadau mbalimbali wa demokrasia nchini kwa kudai mchakato wa nchi kuwa na katiba mpya.

"Kamati Kuu imejadili na kutafakari kwa kina maoni ya wadau mbalimbali juu ya mchakato unaofaa katika kupata katiba mpya na kuzingatia kuwa njia sahihi ni ile itakayowashirikisha wananchi kikamilifu na kwa dhati bila kujali tofauti zao za kisiasa, dini, umri, elimu, kabila wala jinsia zao,' alisema Dkt. Slaa.

Mauaji ya Arusha

Dkt. Slaa alisema kuwa CC ya CHADEMA imeiagiza sekretarieti ya CHADEMA kuendeleza harakati za kudai haki za wananchi wa Jiji wa Arusha kwa njia za kisiasa.

Pia iliwapongeza Bw. Freeman Mbowe, Dkt. Willibrod Slaa na Mbunge wa Arusha Mjini Bw. Godbless Lema kwa juhudi zao za kuepusha shari na kutoa uongozi wa kisiasa "baada ya viongozi wa serikali ya CCM kuwatelekeza wananchi kwa kipindi chote cha matatizo ya Arusha."

"Kamati Kuu imepokea kwa masikitiko taarifa ya vifo vya wananchi watatu wasio na hatia kwa kupigwa risasi na askari wa Jeshi la Polisi kufuatia vurugu zilizosababishwa na jeshi hilo katika harakati za kuzuia maandamano halali na yenye baraka zote za Kamanda wa Jeshi la Polisi wilayani Arusha.

"Kamati kuu imeskitishwa na uvurugwaji wa uchaguzi wa Meya wa Jiji la Arusha kulikofanywa na mkurugenzi wa Jiji la Arusha kwa maelekezo ya Chama Cha Mapinduzi na serikali yake...kamati kuu imewapa pole ndugu wa wafiwa wa vurugu za Arusha, wananchi wa Arusha na Watanzania kwa ujumla.

Mbali ya kutoa pole, pia imewaagiza madiwani wa CHADEMA katika halmashauri ya jiji hilo kuendelea kuingia katika vikao vya baraza la halmashauri kuwawakilisha kikamilifu wananchi waliowachagua, lakini huku wakitumia nafasi yao kufanikisha uchaguzi wa meya.

Umeme, Gesi na malipo ya Dowans

Katika masuala hayo, Dkt. Slaa alisema "kamati kuu imeskitishwa na kupanda holela kwa bei ya nishati muhimu ya umeme na gesi, pamoja na kushindwa kwa serikali ya CCM katika kuwekeza kikamilifu katika sekta ya nishati hapa nchini.

"Kamati kuu imesikitishwa na kufadhaishwa sana na uamuzi wa CCM na serikali yake kuridhia kuilipa kampuni hewa ya Dowans fedha za walipa kodi wa Tanzania zipatazo sh. bilioni 94 pamoja na kwamba kampuni hii ilikwishaharamishwa na bunge kwa niaba ya wananchi...imetambua kuwa sakata la Dowans ni mwendelezo wa vitendo vya kifisadi ndani ya CCM na serikali yake."

Alisema kuwa mbali ya kuwahimiza wana CHADEMA, wabunge na wananchi kwa ujumla kuendelea kupinga kwa nguvu zote malipo ya Dowans, CC ya chama hicho pia imeiagiza sekretarieti yake kuanza maandalizi ya maandamano ya nchi nzima kupinga ongezeko la bei ya umeme, gesi na kuilipa Dowans, yatakayoanzia jijini Mwanza, Februari 24, mwaka huu.

Alisema CC imewaelekeza viongozi wa CHADEMA kuendelea kuwahamasisha wananchi kupinga kwa njia mbalimbali za kisiasa na kisheria malipo ya Dowans na ufisadi mwingine nchini, huku ikiwapongeza wanaharakati wa masuala ya kiraia kwa ujasiri na moyo wa kizalendo wa kufungua kesi kupinga malipo hayo.

"Kamati kuu imeiasa Serikali ya CCM kutokuona aibu kutekeleza sera za CHADEMA zilizofanyiwa utafiti kuhusu namna ya kujenga na kuimarisha sekta ya nishati ya umeme na gesi hapa nchini ili nchi yetu iondokane na tatizo la kudumu la umeme."

Matokeo ya Kidato cha nne

Dkt. Slaa alisema kuwa kutokana na nusu ya watahiniwa wote kutofaulu mitihani, huku asilimia 11.5 pekee kati ya waliotahiniwa wakipata daraja la I,II na III, ambapo karibu asilimia 90 ya wanafunzi hawataweza kuendelea na masomo ya elimu ya juu, CC ya CHADEMA imeyatangaza matokeo hayo kuwa ni janga la kitaifa.

Mbali ya kusema kuwa vijana hao hawataweza pia kupata ajira ya uhakika, kamati kuu ya CHADEMA imesema kuwa matokeo hayo mabaya yamesababishwa na sera dhaifu za Serikali ya CCM zenye kulenga kughilibu wananchi kwa ajili ya mafanikio ya kisiasa kwa kukazia wingi wa majengo ya shule badala ya ubora wa walimu na shule.

"Kamati kuu imeitaka Serikali ya CCM isione aibu kutekeleza sera za elimu za CHADEMA zilizoainishwa katika ilani yake ya mwaka 2010, na imeunda timu maalumu ya wataalam wa elimu kwa ajili ya kutafiti kwa kina sababu za matokeo mabaya ya kidato cha nne na kutoa mapendekezo yake kwa kamati kuu," alisema Dkt. Slaa.

38 comments:

  1. Sawa Mzee tunakusikia nakubaliana na wewe kuwa hata mule makanisani,mikoani na hata Dar waliokuwa wanahimiza na kukupigia debe uchaguliwe kwa nguvu zote ni propaganda ya CCM!
    Unaonyesha una maneno mazuri yenye mvuto na hamasa lakini una kitu nyuma ya pazia poleni sana,tunasubiria hayo maandamano nia yenu nchi isitawalike, lakini hilo haliwezekani kwani watu wapo makini na wanajuwa kinachoendelea

    ReplyDelete
  2. Ukweli utasimama, Chadema tuko nyuma yenu. hongereni kwa kuwa makini sana na hao CUF

    ReplyDelete
  3. Tunisia na Misri hakutawaliki kwa sababu za uzembe wa serikali zilizo madarakani, unategemea Tanzania itatawalika kwa huu uzembe wa JK.Wewe unaleta hoja za kutisha watu eti nchi haitatawalika,hizo ni propaganda za JK kutaka kuwahadaa wa-TZ ili wamuonee huruma kama anaingiliwa ktk kazi.UMECHEMSHA NDUGU MAANDAMANO KAMA KAWA

    ReplyDelete
  4. Kutokuwa ni muungano wa vyama vya upinzani ndani ya bunge ni uhuni wala sio kusema nini kuna zaidi ya ambacho hatujui wananchi,kuhusu suala zima la elimu haitoshi tu maana kuna kundi kubwa la watoto wetu maisha yao yako kwenye balance and high stake.
    Hii ni sababu tosha ya kufanya maandamanonchi nzima kupinga na kushinikiza serikali kuwapa waalimu mazingira mazuri ya kazi na mishahara yenye kueleweka

    ReplyDelete
  5. Nadhani ingekuwa busara kumjibu huyo aliyetoa maoni yake. Lakini siyo kumuingiza JK na kudai hizo ni propaganda zake kwani hii inaonyesha chuki binafsi na udhaifu upande wako.

    ReplyDelete
  6. Wacha upumbavu na ujinga kusupport vitu vya kijinga unadhani watunisia wote watoto watu wazima na wazee wajinga wanatofauti gani na sababu ambazo tunazo sisi dhidi ya serikali yetu hadi aunadhani haifaai kuandamana au wew miundo mbinu yako safi,maji,umeme,huduma za jamii ziko pouwa kwako,matumizi ya nguvu ya polisi ni pouwa kwako,gharama za maisha zinavyopanda kila kukicha kwa baraka za serikali wew pouwa tu,sasa mafuta hayoo 2000 na kitu kwako pouwa bse nchi hii inatawalika unadhani vitu hivyo vinaenda kiudini wacha ujinga uafrika wetu ndio kitu cha kwanza kutoa tofauti zetu na shida na mateso yetu ndio kitu kinachotuunganisha,nadhani elimu duni ambayo ulipata kwa walimu wasiokuwa na vigezo ndio maana hataupeo wako umekuwa mdogo kuweza kuona kipi ni bora unachefua na kutia hasira. . ... kwahiyo kufika walipo wa Tunisia,Egypt,lebanon,jordan,hata bongo linawezekana kufika kwasababu sisi tuna sababu nyingi zaidi ya wao na wao bado wameamua kuandamana.

    ReplyDelete
  7. Asante Dr. Slaa na CC ya Chadema. tunajua kwa hakika Udini ni Propaganda za Kikwete na serikali yake kwa ajili ya kupanga kuleta machafuko na kuzuia demokrasia ya kweli wakati utakapofika...Mungu iepushie Tanzania udini huu uliokita mizizi yake wakati wa utawala wa JK.

    ReplyDelete
  8. CHADEMA muwe makini, hivi sasa mmejiweka kwenye mazingira ya kuwa chama chenge nguvu, kila kitu kiwe cha kiasi, maoni yangu CUF inaweza kutengwa ila vyama vingine jaribuni kuvihusisha kwenye upinzani hii itawapa nafasi hata hao wapinzani kuwasupport 2015. Sasa mkianza kutenga kila chama cha upinzani muelewe mpo wachache bungeni na hamtakuwa na nguvu ya kutuwakilisha WATANZANIA kwani katika kila jambo ambalo litahitaji kupigiwa kura CHADEMA itakuwa na uhakika na kura 44 tu. SASA Mnataka kutuambia kuwa mtaweza kushawishi Bunge kwenye kila jambo ambalo lina maslahi ya Taifa ambalo linakingiwa kifua na CCM? - tujaribu kuangalia vita ya mbele sio ya uongozi na posho ya kambi ya upinzani tu

    ReplyDelete
  9. Tuache kushabikia mambo bila kuyapima, suala hapa ni la aserikali kutekeleza wajibu wake kwa wananchi kwani hakuna kiongozi yeyote atakayeingia madarakani kwa kuchaguliwa na dini yake. Viongozi wetu sasa hawajali wananchi wanaishije, hali ngumu kila mahali kuanzia vyakula, sukari, mafuta, kodi za nyumba, vifaa vya ujenzi n,k. Watu wakihoji wanaambiwa wanaleta udini! kwanini serikali iliyopita iliweza kudhibiti mfumuko wa bei za vitu kwa muda wote wa miaka kumi sukari kwa mfano haikuzidi sh.mia sita kwa kilo, leo hii ni zaidi ya mara tatu ya bei hiyo. Watanzania wanachohitaji ni unafuu wa maisha tu wala hawana makuu, watimizieni muone kama kutakuwa na malalamiko yoyote.

    ReplyDelete
  10. Bila hata kutafakari kwa kina unaweza kuona kuwa uwezo wetu wa kufikiri, kupima hoja zinazotolewa na kuchangia ni tatizo kubwa. Msingi mkubwa ni elimu ndogo tuliyonayo tulio wengi na hatukuweza za kupata nafasi ya kufunzwa kuwa wapembuzi makini. Hebu jaribu kufikiri, wakati kafu wanaandaa mwafaka na ccm waliwapa upinzani kujadili hatima ya Zanzibar kwa mustakabali wa watanzania wote na vyama vyote? Suala la mfumo wa bei je watawala wanasingiziwa ama wameshindwa kutekeleza sera makini ziatakazotubadili, Athari mbalimbali za kielimu, kisiasa na kiuchumi zimetoka wapi? Kwa watu waliosoma yaliyosemwa na Mzee msuya unapata jibu. Waswahili walisema miruzi mingi ilimpoteza mbwa, wapishi wengi huharibu mchuzi, njia za mwongo ni fupi, wa moja havai mbili na wa mbili vivyo hivyo.

    ReplyDelete
  11. SERIKALI YETU NI YA AJABU SANA, UTAMSIKIA RAIS AU WAZIRI MKUU WAKE AKISEMA WAUZA MADAWA YA KULEVYA TUNAYO MAJINA YENU LAKINI TUNAWAPA MUDA MJIREKEBISHE! EBO! HIYO NI KAZI YAO INAYOWAPA ZIRIKI ZAO WATAACHA VIPI KAMA SI KWA KUPEWA KIBANO? MARA OO MAFISADI NI WATU HATARI SANA TUKIWAKAMATA NCHI ITAYUMBA, HUU NI UDHAIFU MKUBWA SANA WA KIUONGOZI KAMA WENYEWE HAWAJUI.
    ILI NCHI IENDELEE TUNAHITAHI MAMBO MANNE: ARDHI, WATU, SIASA SAFI NA UONGOZI BORA. WHAT'S MISSING? JIBU UNALO/

    ReplyDelete
  12. Duh! jamaa yangu umempasha uzuri huyo jamaa anae tetea serikali ya JK.unajua watu wengi hawajui ulaghai wa wanasiasa, nyerere alishasema kuwa viongozi wanaotumia dini, kabila kwenye tawala zao ilikuhalalisha uongozi wao ujue ameanza kufilisika kisiasa. JK na serekali yake ndio walivyo sasa. kutokana na kushindwa kutekeleza ahadi zao na kupelekea mfumuko wa bei,dorwans, umeme, elimu(rejea kidato cha 4), uwizi rasilimali, ufisadi serikalini, na mengine mengi ndio maana wanatumia suala la udini kupata support ya udini. mnahadaiwa wakati mtoto wako na wewe mwenyewe unapigika wao wanakula maisha. watoto wao wanasoma shule bora, wanapata afya bora viongozi wa kidini nao wanapata ofa na serikali wana walaghai wa umini kuwa dini fulani inamchukia JK kwa udini c kweli hebu angalia maisha yako kamili. rejea nilioanisha hapo juu, je? yanahusiana na udini? mtu anaekupa mkate ndio bora kuliko anae kuchorea mkate kwenye karatasi.

    ReplyDelete
  13. mimi nashindwa kumuelewa huyu Dr Slaa.je tatizo ni C.C.M au kikwete? maana anaposema C.C.M imeshindwa kuwakomboa watanzania kwa kipindi cha miaka 50.inaamaanisha kuwa tangu uhuru. kwa hiyo ni tangu utawala wa Nyerere mpaka Kikwete. wakati mwingine anamsifia Nyerere alifanya kazi mzuri. sasa je tatizo ni Kikwete au C.C.M?. kuhusu suala la udini, je DR Slaa wakati wa kampeni za uchaguzi 2010 uliwahi kufika Zanzibar kuomba kura ambako asilimia 80 ya wakazi ni waislamu? je ulienda kuomba kura huko na ulifanya mikutano mingapi ya hadhara ukilinganisha na maeneo ya kwenu Arusha? hivi unaposema nchi hii haitawaliki, je unamalengo mazuri na nchi hii? nchi isipotawalika je akina nani wataathirika zaidi? je ni masikini unaosema unawapigania au matajiri? mzee kama wewe maisha umeshayachoka tuache sisi tuendelee kula ugali wetu na matembele kwa sababu hatujakuja kwako kukuomba ugali hata siku moja.

    ReplyDelete
  14. CHADEMA HONGERENI MAANA ISINGEKUWA BUSARA KUMWEKA CUF AU MREMA WA TLP KWENYE KAMBI YA UPINZANI. ILA NAWASIKITIKIA SANA NA TENA SANA NCCR-MAGEUZI NA UDP ETI KUUNGANA NA CUF AMBAYO IMESHAFULIA BARA.SIJUI HAO WANAOJIITA KAMBI NDOGO YA UPINZANI WAPO KWA MASLAHI YA NANI? KAFULILA TUMIA UBONGO WAKO WACHA KAMASI ZA MBATIA

    ReplyDelete
  15. mzee slaa mimi binafsi mzee ww umezeeka vibaya tafadhali tuache na nchi yetu kwanza mzinzi umepora mke wa watu mimi binafsi ni mkristo na ni wadhebu jingine sikusapoti hata kwa nn na wakristo wanaokushabikia ww ni waroman peke yake ninakushauri sana mfate mzee mwenzio pengo urudi kanisani siasa waachie wasio na chuki sidhani kama kunamskini hata mmoja anakufata umpe chakula

    ReplyDelete
  16. Kwa maoni haya naona kabisa watu wameshachoka, wameshakosa uvumilivu tena. Wanaona lolote likitokea yote ni heri hawana cha kupoteza.

    Binadamu akisha fikia hapo, ni mtu hatari kuliko hata mnyama wa porini. Hivi kweli Watanzania ndipo tulipofikia? Ni nini kimetufikisha hapo? Nani katufikisha hapo? Yote ni maswali yanayohitaji majibu ya kisayansi!

    Mwanafalsafa Karl Marx kwenye karne ya 19 alituonya kuwa, pale ambapo jamii inakuwa na matabaka makubwa kati ya walionacho na wasionacho, wanaokandamizwa dhidi ya wanaokandamiza, Matajiri wachache na masikini walio wengi. jamii ile ya walio wengi kwa maana ya wanyonywaji, wakandamizwaji, na masikini hawawezi kupata haki yao isipokuwa tu kwa umoja wao, kuungana na kuwafurumushia mbali tabaka la wachache ambao ni matajiri, wakandamizaji na wanyonyaji! Hapo ndipo jamii huru isiyo na matabaka, yenye umoja endelevu na taasisi imara itakapochipuwa na kustawi hatimaye kila mtu kufurahia matunda ya uhuru wake kama mwanadamu huru.

    Falsafa hii bado haijaisha, inatawala. Inatawala Tunisia, inatawala Misri, inatawala Ivory Coast, inatawala Sudani. Imetawala Kenya, Imetawala Afrika ya Kusini, imetawala Burma nk kote unakoweza kukutaja.

    Falsafa hii sidhani kama haitatawala Uganda, Haitatawala Kigali, Bunjumbura,na zaidi Tanzania! Nadhani sasa umefika wakati tuanze kutafakari na kufanya maamuzi kabla hatujapita njia hii! Mimi njia hii siipendi lakini ikionekana ni njia pekee ya kuleta ufumbuzi kwenye matatizo yetu ya kiuchumi, kisiasa na kijamii hapa Tanzania basi tushikamane tuliondowe hilo Tabaka la watawala, kwa njia ambazo sisi watanzania hatutakuwa waasisi wake, kwani tayari waasisi wake wapo kina Karl Marx, Che Guevara, Lenin wa Urusi nk.

    Mapinduzi Tanzania yanakaribia! Tuhakikishe damu ya mtanzania hata mmoja haimwagiki lakini lengo kubwa ni kuwaadabisha watawala viburi, wasiosikia vilio vya wananchi, wanaoendekeza ufahari, kujilimbikizia mali kugawana na ndugu na marafiki zao mali za Watanzania wote nk!

    Mungu ibariki Tanzania Mungu tusaidie kifikiri kwa hekima na kutupatia majibu ya sahihi katika hili!

    By Carwin

    ReplyDelete
  17. Sawa Mzee tunakusikia na nakubaliana na wewe kuwa hata kule makanisani,mikoani na hata Dar waliokuwa wanahimiza na kukupigia debe kwa uhakika ili uchaguliwe kwa nguvu zote ni propaganda ya CCM!!!
    Unaonyesha una maneno mazuri yenye mvuto na hamasa lakini una kitu tena kibaya sana nyuma ya pazia, poleni sana,tunasubiria hayo maandamano nia yenu nchi isitawalike, lakini hilo haliwezekani kwani watu wapo makini na wanajuwa kinachoendelea.
    Si hayo tu, una chuki binafsi kwa JK ndiyo maana kila kukicha huachi kumtukana na kumzulia majanga japo analindwa na Wote, Mungu, Mtume Mohamad, Yesu, Malaika Michael, Gabriel na Raphael, Slaa una mihasira ya aibu ya kushindwa Uraisi kama ulivyo ahidiwa na makanisa machache husika. Hata wewe
    ukitawala, wewe sio malaika na siyo mtakatifu kabisa, makosa na mapungufu yatakuwepo tu. Kwani wewe Slaa ulipewa na Mungu yupi fagio la USAFI katika uongozi?? una uchu wa madaraka tu wewe. Kama unataka kutawala, uache kumganda mtu binafsi kwa maneno na kejeli kwa kupitishia kwa watu for confirmation. Sisi tutakuunga mkono iwapo utatumia sera zako kwa kutokana na jinsi unavyo chimbua ubaya katika uongozi lakini unakera unapo wataja watu kila siku. Chuki binafsi zako hizo, uchu wa madaraka na aibu ya kuukosa uongozi uweke pembeni. Maneno yako ndiyo yaliyo chochea watu kufa Arusha. Uliwaona CCM wakiwepo kwenye maandamano yako? Ulimuona JK? JK ni mjinga awatume watu kuua watu wengine? Uwe na busara mzee Slaa. usifikiri wingi wa washangiliaji wengi wao wahuni wa mitaani ndiyo kutupumbaza tukubali kila unacho kifikiri, kukiwaza na kukitenda. Umetuchosha.
    Huna good leadership ethics. Una kitu au vitu vibaya sana chini ya pazia lako la uongozi. (You are weak, bold, upright, no self respect, lack of tolerance, immaturity) hayo ndiyo yako nyuma ya hilo pazia lako. Jisafishe, tulia, acha hasira.

    ReplyDelete
  18. Asante kwa maoni wetu nyote na kwa malalamiko ya ukosefu wa uwongozi serikalini. Kusema kweli kila Binadamu duniani anachoomba ni amani na kuishi bila tafrani ya kumbuliwa na wenzake Binadamu. Ikiwa ipo amani na usalama katika nchi yoyote ile Ulimwenguni hiyo ndiyo nchi ya usalama na amani kwa watu wake.Usalama na amani zinatokana na Uwongozi bora wa nchi bila mapendeleo kwa watu binafsi au vikundi au kabila. Sisi wote ni watoto wa Mungu Dini na Ukabila haya mambo sio ya kufatilia. Kila mtu yuko huru kuchagua hali ya maisha yatakayo mfaa kuendesha yake na yakayo mfaa kesho kwa Mungu wake kama anaamini kuwa yuko Muumba aliyemuumba kuishi hapa Duniani.Kila mtu huona maya au kutamani akiona au akisikia nchi fulani inaishi kwa usalama na amani bila matatizo.Kila mmoja inambidi kujiuliza kwa nini hiyo nchi iko vila? Jibu lake kwamba watu wote wanapendana na wanishi kama familia moja na hawapendi kuudhiana au kuoneana wivu, wote wanaishi kwa kusaidiana na Serikali yao ndiyo wao wenyewe, hawajaleta mtu kuwaongoza toka nje ya nchi yao.Ikiwa kiongozi ana kasoro basi huyo mtu hapendi USALAMA wala AMANI kwa nchi yake ni bora asiwe kiongozi.

    ReplyDelete
  19. Hongereni CDM, mmetuonyesha kuwa mnasikia maoni ya wadau na mnajua nchi inakopaswa kuelekea.

    Nawashangaa hao ambao wanafikiri mpaka sasa nchi inatawalika. Kama nchi inatawalika ni nani anayeamua bei za bidhaa zipande. Ni nani anayeamua Dowans walipwe. Ni nani anayedhibiti ufisadi kwenye mashirika ya umma? ni serikali gani inaona wananchi wake wanahangaika na maisha, bila kutoa mwongozo wowote?
    Nchi haitawaliki hata sasa. Kama inatawalika mbona bei zinapanda kiholela? mbona shule hazina waalimu wala vitendea kazi? mbona polisi hawafuati sheria? mbona kila mtu ni msemaji kwenye serikali ya CCM?

    Hongera CDM, wala msijali kuwa hoja zenu hazitapata kura nyingi bungeni. Wenye moyo na watanzania hawatajali watawapigia kura hata kama ni wa CCM, CUF, NCCR au UDP. wenye kinyongo tutawajua

    ReplyDelete
  20. INASHANGAZA SANA KILA KUKICHA DR,SILAHA ANAZUA NA KUTAFUTA NJIA ZA KULETA UONGO USIO NA TIJA, UZEE WAKE NI MBAYA NA NI WA TAMAA, AMEWEZA KUWAHAMASISHA BAADHI YA WANA MTANDAO NA BAADHI
    YA WASOMI KUMUUNGA MKONO, KWELI NCHI YETU INA MATATIZO MENGI KWA WANANCHI, INA KASORO NYINGI LAKINI TUANGALIE TULIKOTOKA,TULIPO NA TUENDAKO
    HALI YA SASA NI BORA KULIKO HUKO TUTOKAKO, LAKINI KWA KUWA UPINZANI HAPA KWETU NI KUPINGA HATA MEMA HAMTAKUBALIANA NAMI.TUANGALIE SERIKALI ILIKUWA INAKUSANYA KODI KIASI GANI NA SASA TUKO WAPI, TULIKUWA WANANCHI WANGAPI SASA TUKO MILLION NGAPI BARABARA,MAHOSPITALI NK MIKAKATI INAONEKANA WAZI ILA KUNA BAADHI YA WATENDAJI NI WABOVU.UDINI UPO HASA KWA WAKATOLIKI NA NDIO WANAKUWA MSTARI WA MBELE KUKEMEA HILO WAO WALIKUWA WANAMPIGIA DEBE HUYU MZEE MAKANISANI WAZIWAZI HIVI WANAOSALI HUMO WOTE NI CHADEMA? WALIJISAHAU NA WANAKANUSHA MUHIMU NJIA ZA BUNGE VIKAO SEMINA NA MIKUTANO INAWEZA IKAZIDISHA CHACHU YA MAENDELEO SIO MAANADAMANO HATUJAFIKIA HUKO LENGO LENU NI KUTAKA KUVAMIA NA KUHARIBU MALI ZA WATU NA KUPORA NIA YENU NI KUTUVURUGA -HATUVURUGIKI

    ReplyDelete
  21. Ondoka Kikwete, umeishiwa sera! kazi yako kuhuburi udini, unataka kusababisha yalitokea kule Rwanda na Burundi.

    CUF siyo chama cha upinzani tena. Huo ni ukweli usiopingika.

    ReplyDelete
  22. Watu tunapaswa kuelewa historia kabla ya kuzungumza kuna wengine wameanza kushabikia siasa waka jn hebu wanaosema kwama slaa yupo kwa aajili ya upinzania nani watu walikufa pemba na mwembechai mbona hakusema waliumia pale mbagala mbona hakusema na anae sema udini kwakweli tuseme haki k si chadema ni nani na ndo wanaolizungumza sn hebu turudishe historia nyuma kidogo watu waliuwa mwaka 2001 uliona viongoziwa dini ya kikristo kwenda kuzika na kulaaani walinyamaza kmya na mbona hata mwebe chai nao walikaa kimya ila leo wanaleta udini na kuhitaji waislam waongee acheni ujinga someni history na kusema chama cha cuf ni sehemu ya serekali hebu wacheni wale watu wa znz wakae kwa amani slaa acha udini

    ReplyDelete
  23. Tujaribu sana kuijadili mada na siyo kuendeleza chuki. Mwenye macho haambiwi tazama maaana ukweli unajulikana tu hata ukiupindisha. Ushabiki wa kisiasa bila kufuata taratibu na kuusimamia ukweli ni hatari kwa amani ya Taifa letu. Walichosema CC ya CHADEMA siyo ubabaishaji bali ndiyo ukweli wa mambo ulivyo. Ukipingana nao usitumie jazba tumia busara na hekima. Ukimtukama Dr. Kikwete ama Dr. Slaa haitasaidia kubadilisha ukweli wa mambo.

    ReplyDelete
  24. Aisee mbona mmepeleka hayo maandamano mbali sana, bado nitakuwepo kweli duuu!!!!!. Ninatuma pongezi zangu kwa CC YA CHADEMA na wanachama wote kwa ujumla. Mimi ninajua kabisa CHADEMA ni chama kitakachowasha nuru, taa kwa watanzania katika maisha. Yote yaliyopangwa ni safi hakuna kurudi nyuma mbele kwa mbele hakuna kurudi nyuma.


    Nawashangaa hao ambao wanafikiri mpaka sasa nchi inatawalika. Kama nchi inatawalika ni nani anayeamua bei za bidhaa zipande. Ni nani anayeamua Dowans walipwe. Ni nani anayedhibiti ufisadi kwenye mashirika ya umma? ni serikali gani inaona wananchi wake wanahangaika na maisha, bila kutoa mwongozo wowote?


    Nchi haitawaliki hata sasa. Kama inatawalika mbona bei zinapanda kiholela? mbona shule hazina waalimu wala vitendea kazi? mbona polisi hawafuati sheria? mbona kila mtu ni msemaji kwenye serikali ya CCM?

    Hongera CDM, wala msijali kuwa hoja zenu hazitapata kura nyingi bungeni. Wenye moyo na watanzania hawatajali watawapigia kura hata kama ni wa CCM, CUF, NCCR au UDP. wenye kinyongo tutawajua. PEOPLE'S POWERRR!!!!!!!!!. ASANTENI.

    ReplyDelete
  25. eng. mwakapango,E.P.AFebruary 1, 2011 at 7:16 PM

    hivi kuwa mbunge wa upinzani lazima uwepo kwenye baraza kivuli la mawaziri? unaweza kabisa kuwawakilisha wananchi bungeni bila kuingia kwenye baraza kivuli kwani unayo platform ambayo ni nafasi yako ya ubunge. mimi nawapongeza CHADEMA kwa kufaulu kuunda serikali kivuli wao wenyewe kwani kutakuwa na nidhamu ya kutosha. vilevile nawaomba wabunge wengine waungane na CHADEMA kutetea wananchi. tusije tukaanza kusikia mara mimi ndiyo nilikuwa mpinzani zaidi na wa kweli yamepitwa na wakati tugange yajayo.kuhusu katiba naungana na CHADEMA rais kikwete ainusuru nchi isikumbwe na maandamano kama Misri, kwani kuidaka hoja na kung'ang'ania kuunda tume nikutaka kuwatengenezea wananchi leading questions. naamini JK ni mdemokrasia wa kweli ndio maana ni katika kipindi chake tumeshuhudia mabadiliko makubwa ya kisissa ikiwa ni pamoja na serikali ya kitaifa Zanzbar na wapinzania kuzoa kura nyingi ya za wabunge na madiwani. na nimatuimaini yangu kuwa JK ATAMWOGOPA MUNGU NA KUTUONGOZA VIZURI KWENYE ZOEZI HILI LA KATIBA.
    Kuhusu maandamano ya arusha nadhani tatizo si serikali ila IGP Mwema na wenzake nawahakikishia DAMU YA WATANZANIA ILIYOMWAGIKIKA ARUSHA INAWALILIA. Polisi mwogopeni Mungu na kama kuna moto mbinguni basi MOTO MKUBWA KULIKO WOTE UTAWANGUKIA NYINYI kwa kulinda maslahi ya mafisadi kwa kuua watanzania.
    kuhusu mtihani wa formIV wanafunzi wamekosa commitment kutokana na upungufu wa vifaa (maabara, vitabu, pamphlets n.k) walimu kutolipwa vizuri na kusahaulika kwenye vitu vya msingi. unategemea nini mwanafunzi anakaa chini, mwalimu hana nyumba na kama anayo ni pagale wanafunzi waperform. KAMANDA JAKAYA MLISHO KIKWETE JIPANGE SONGA MBELE NCHI BADO INAMAHITAJI MENGI.

    ReplyDelete
  26. Hivi jamani, kati ya CCM na CHADEMA ni chama gani kinachohusudu sana masuala ya udini?

    Katika uchaguzi mkuu wa 2010, CCM kuanzia mwenyekiti wa chama kitaifa (J.K), makamu wa rais (GHALIB BIAL), katibu wa chama (MAKAMBA) na Mratibu wa kampeni za CCM (A. KINANA), Team yote hiyo hakuna hata mmoja mshika rozali, wote ni barghashia tu. Sasa udini wanaodai unafanywa na CHADEMA huko wapi? kama zote hizo sio propaganda za kisiasa.

    Watanzania tuwe macho na maneno yawanasisiemu, wasitufumbe macho kwa kauli zisizokuwa na vichwa wala miguu, Tumewapa miaka mingi sana yakuleta maisha bora kwa watanzania, sasa kamawameshindwa kwa miaka yote hiyo, huko mbele wataweza?

    ReplyDelete
  27. Udini! udini! udini!
    Hii ni mbinu ya ccm tu ya kutaka kupotosha watu. Viongozi wengi wa ccm hasa hasa Jk na wengine wanatumia dhana hii ili kupotosha hoja za msingi kama vile dowans, richmond,IPTL,Mauaji wa raia Arusha na wengineyo.

    Mimi nadhani wananchi awanabudi kuwapuza watu wengine kutumia dhana hii.

    ReplyDelete
  28. kwa matusi, kashfa na dharau ya slaa na washabiki wake, ninajitoa chadema. i think it is okay to insult the president. nafikir CUF wana hekima kuliko chadema. kwanza slaa aoe na atunze familia. Asivyoheshimu imani, mila na tamaduni zetu, ndivyo anavyo mdharau kila mtu. Utaishije na mtoto wa mtu bila kibali cha mzazi? kwani huyo mchumba wa slaa hana wazazi wala walezi? ni heshima iliyoje kupiga goti kwa mzaa chema. if he has no true love with the girl, no wonder he loves no one and insult the president. ni wazi kabisa kuwa watanzania wengi wanampenda kikwete kuliko slaa. matusi ya nini? anatutukania mpendwa wetu kwa nini? slaa, i hate you - sorry to say!

    ReplyDelete
  29. Nenda tena ufike salama na usiangaliye nyuma, ukiangali nyuma utajeka jiwe. Kwanza wewe ni mtu wavurugu ninani akupe kadi. CHADEMA sio chama cha kihuni ni chama cha watu waelewa. Umenielewa.

    ReplyDelete
  30. Wa kwanza unayetakiwa kukemewa ni wewe kwa kupora mke wa mtu na serikali inaogopa kukuchukulia hatua,mnalalamikia katiba mbovu wakati katiba hii ndio inayowafanya mpore wake za watu bila kuadhibiwa,ingekuwa mimi mlalahoi saa hizi naozea jela,na wala Kikwete hajahubiri udini na ziko kila sababu za kuamini hivyo kwani ndani ya CCM wenye nguvu kubwa na wengi ni Wakristo hivyo si rahisi yeye kuhubiri hilo,tunawahakikishia tutamlinda Kikwete hadi amalize muda wake ni Rais halali na ana wabunge zaidi ya asilimia 75% mtakaa hivyo hivyo kudanganyana,hapa sio Misri wala Tunisi ambapo viongozi wao wamekaa kwa miongo mingi madarakani kama alivyokaa Mbowe na wewe Slaa kwenye Uenyekiti na Katibu Mkuu na mkitaka kuondolewa inakuwa balaa,Kikwete keshokutwa hapo 2015 anaondoka kwenye urais na uenyekiti,nyinyi je? mtafia humo kwenye vyeo mlivyo navyo,Tunisia na Misri inafanana na nyie na chadema yenu.

    ReplyDelete
  31. Wewe unayejisema Yassin ni John tunawajua mbinu zenu zenu,umetupa picha ndogo ya kijinga lakini hujaeleza Wakristo wangapi na Waislamu wangapi wenye vyeo na wapi ni wengi zaidi. MBINU ZENU ZIMESHINDWA KUBADILI FIKRA ZA WATU NA WAKATOLIKI MJUE HATA AKIPATA HAKUNA DOMINATION TENA MMETUSTUA WENYEWE NA SASA MKAE TAYARI KUMEZA KIDONGE JAPO KICHUNGU,KATIBA IJAO LAZIMA IWEKE MAMBO HADHARANI HAKUNA WA KUTUZUIA WAISLAMU KUHOJI

    ReplyDelete
  32. chadema hawana jipya,zile ajenda zao za siri tumesha zijua,udini upo siku nyingi ila ulikuwa wa kisirisiri mpaka pengo alikuwa anaingia kwenye baraza la mawaziri na vatican kuwa na ubalozi tanzania makanisa kuhodhi ardhi kubwa nchini kote na mengine mengi ila chadema imeweka udini wao wazi na kuwafumbua macho walio wengi,nawashauri kazi bado ziko nyingi za kufanya tafuteni,mwenzio anapiga disco

    ReplyDelete
  33. Slaa ungekuwa mwanamke Kikwete angekuoa. mdomoni kwako Kikwete habanduki,haikusaidii kKikwete ni mpaka 2015,mnayokusudia na kanisa lako nchi isitawalike mnajidanganya.

    ReplyDelete
  34. Haya Sasa at least kuna watu wameanza kuongea wanachokusudia ambacho ni kuingiza uislam katika katiba.. Mjue tu kitu kama hicho kikitokea reactions au consequences zake zitakuwa ni nini maana haya mambo yanachukua sura mpya au kuibuka kila kipindi nchi hii inapotawaliwa na mwislam. Mungu atusaidie sana watanzania wote na si baadhi katika kuiendeleza nchi yetu na katika kuishi kwa amani na upendo na uwajibikaji. Kila kiongozi ktk serikali hii anasema la kwake hakuna uniformity na hii inaonyesha kama vile rais either yuko weak au hajali ili mradi kapata term ya pili kwa kuiba au halali yeye bora liende. Nchi imeoza na kunuka rushwa.. Kila mtu anataka cha juu!! Hata ma-housegirl wanachakachua! Hii si hatari? itafika wakati tutakuwa kama Misri. Mimi sitashangaa hali kama hiyo ikija Tanzania na naamini ikitokea hapa damu nyingi itamwagika. Tuombe Mungu tu hali hiyo isitokee maana viongozi wenyewe ndo hao na polisi ndo kama hivo... Tuombe sana Mungu atusaidie!!

    ReplyDelete
  35. Slaa sio tu mdini.bali pia ni mkabila nahisi mbowe amefanya kosa kubwa kumuweka huyu jamaa
    mungu ameinusuru Tazania na balaa kubwa kwa kushindwa kuwa rais slaa slay viongozi kama hawa wenye maneno mengi ndio wanakua madikteta si mnakumbuka zambia,mkapa.lazima watanzania muwe makini

    ReplyDelete
  36. Hakuna kuingiza Uislamu kwenye katiba ila tunachosema sisi Waislam ni kuwa haki zetu ziangaliwe kama za wakristo kwenye katiba msijaribu kupotosha mada na ndio maana wataalam wa katiba wanasema katiba ni ya wananchi na si ya wanasiasa,na wananchi ni wakina nani? ni mimi na wewe uwe mkristo,muislamu, pagani,hindu na wengineo hatutakubali katiba iwe ya watu fulani tu,hii hapana kama ni hivyo hamna haja ya kudai katiba mpya,

    ReplyDelete
  37. Nimefurahishwa sana na huyu ndg. Melkiory Matiya ambae ametoa picha yake kwenye kuchangia mada. Hongera sana bwana kwa sababu katika karne ya leo hakuna haja ya kujificha ili mradi katika kutoa mawazo yako huvunji sheria maana yake hutukani mtu au kwenda kinyume kwa namna yoyote. Katika mada hii naomba kwanza niwapongeze viongozi wa Chadema kwa kupunguza jazba na sasa wamekubaliana kudai haki yao kisiasa. Huku ndiko kukomaa kisiasa. Pia issue ya udini mimi niliisikia kwa mara ya kwanza wakati Rais alipohutubia bunge. Inasikitisha sana kuwa wanasiasa wetu hawa uchwara wameanza kuwaghilibu wananchi kwa kuwahusisha wakristo (maaskofu) na kura za Chadema. Huku ni kufilisika kisiasa kama alivyowahi kusema mwalimu Nyerere. Kwa bahati nzuri dini ya kikristo ni dini inayohimiza ustawi wa jamii ya waumini wake katika maendeleo ya elimu, afya, upatikanaji wa maji safi na salama n.k. Hivyo ni wajibu pia kuelimisha wananchi juu ya kupatikana utawala wenye kujali na kuimarisha huduma za jamii. kwa mantiki hiyo maaskofu hawakupiga debe kwa chadema eti kwa kuwa dr. Slaa ni mkristo. Wahafidhina hawa wa agenda ya udini wamesahau kuwa mwaka 2005 maaskofu hao hao ndio waliosema kuwa Kikwete ni chagua la mungu na leo iweje wageuke kuwa si chaguo lao? Watawala mnapozungumza agenda ya udini, ukabila, ujimbo, umkoa, uwilaya mjue mnatuchefua watanzania na ndipo mnazidi kujipalia makaa zaidi. Taaluma ya Dr.Slaa ni upadri ambao ni sawa na taaluma nyingine kwani huyu bwana ana Elimu ya shahada ya uzamivu katika sheria za kanisa (PhD.in canon Laws) ni sawa na mtu mwingine kabisa mwenye shahada kama hiyo katika Islamic studies au Hadith au Sharia n.k. hapa udini uko wapi? hivi hao wote walipogombea hawakuwa na dini isipokuwa ni Slaa, maaskofu na Chadema. Ili Mhe. Rais aendeleze heshima yake aache kushabikia maswala ya dini tutaelekea kubaya itafika mahali huko bungeni, maofisini, n.k kutakuwa na watu wa dini fulani.mijadala ya dini ife kabisa wanasiasa wa namna hii wamefilisika kisisa na waogopwe kama ukoma.

    ReplyDelete
  38. Usitudanganye Bwana mkubwa,maaskofu walisema Kikwete chaguo la Mungu wakati ule kwa sababu ya kuihofia CUF maana wakati huo ilikuwa na nguvu kubwa kisiasa,hawa ni watu wanakwenda kwa kuangalia maslahi ya Kanisa yatakuwaje,unaweza kuniambia ni kwa kwa nini Maaskofu hawakupayuka sana wakati Mkapa na kundi lake walipokuwa wanaimaliza nchi hii? Mimi nikiwa Marekani nilikuwa nasoma uozo wa serikali ya Mkapa kwenye ufisadi uliokithiri,hapa wewe unazungumzia elimu lakini kuwa na elimu ni mpaka uitumie na uwajibike kwa wananchi,tunachosema uchaguzi umekwisha na hakuna wa kumuondoa Kikwete mpaka ufike muda wake wa kuondoka na uzuri anaondoka moja kwa moja kutokana na system nzuri waliojipangia,sasa Slaa na Mbowe watafia katika hizo nafasi maana Misri na Tunisia inafanana na chama chao kwa viongozi kuganda kwenye madaraka kwa miongo,Mubarak ametaka kumuachia mwanae kama vile Mtei alivyomuachia mkwewe Mbowe uongozi na sasa ni zaidi ya miaka kumi ni huyohuyo. Misri na Tunisia iko chadema,Tanzania haipo tumeishabadilisha uongozi mara nyingi,NYERER,MWINYI,MKAPA NA SASA KIKWETE NA HAWEZI KUONGEZWA MUDA AKIMALIZA ANAONDOKA.

    ReplyDelete