09 May 2011

Madiwani wamwita waziri kuona ufisadi

Na Livinus Feruzi, Muleba

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba mkoani Kagera wameazimia kuomba Waziri wa Tawala za MIkoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) katika Ofisi ya
Waziri Mkuu, Bw. George Mkuchika kufika haraka wilayani Muleba kuona ubadhirifu wa zaidi ya milioni 231.9 unaodaiwa kufanywa na watendaji katika halmashauri hiyo.

Aidha wameazimia kuwa ndani ya siku 30 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa  halmashauri hiyo, Bw. Pastory Kajuna awe ameondoa mabati kutoka Uganda yaliyoezekwa katika majengo manne ya serikali, ambayo inadaiwa hayana viwango na ubora.

Madiwani hao walipitisha azimio hilo juzi wakati wa mkutano wa Baraza la Madiwani, ambapo walimwagiza mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Bw. George Katomero kuwasiliana mapema na waziri huyo ili afike kunusuru halmashauri ambayo inadaiwa kuteketea kutokana na matumizi mabaya ya fedha za wananchi.

Madiwani hao walikubaliana kuwa kabla ya baraza lijalo watatakiwa kuwa wameishazungumza na Waziri Mkuchika juu na mstakabali wa halmashauri hiyo na mwenyekiti atatakiwa kutoa majibu ya azimio hilo katika baraza lijalo na kuwapeleka katika Kamati ya Midhamu na Maadili watendaji wanaotuhumiwa kutumia vibaya fedha za umma.

Aidha katika taarifa ya mkaguzi wa ndani wa halmashauri hiyo, Bw. Blasio Paul alisema kuwa katika kipindi cha robo tatu ya mwaka kumekuwepo na utaratibu mbaya wa matumizi ya fedha, ambapo zaidi ya shilingi milioni 231.9 zimetumika vibaya.

Katika taarifa hiyo Bw. Paul alisema katika akaunti za idara mbalimbali za halmashauri fedha zimekuwa zikitumika kinyume, ambapo wakuu wa idara wamekuwa wakilipwa posho zaidi ya mara moja kwa shughuli tofauti na kwa wakati mmoja.

“Kuendelea kuchukua posho kwa ajili ya shughuli nyingi zinazofanyika kwa wakati mmoja ni kinyume na matumizi mabaya ya fedha za halmashauri, hali hii pia inawanyima nafasi ya kushiriki katika kufanya shughuli iliyokusudiwa, hii pia inadhihirisha ubinafsi usio na maana unaofanywa na wakuu wa idara,” alisema.

Alisema kuwa katika malipo hayo hakuna viambatanisho muhimu, malipo hayakuambatana na hati za kukiri kupokea fedha hizo, hakuna orodha ya majina na sahihi za walipwaji, hakuna taarifa za kazi au safari na  hakuna uthibitisho wa kuwa nje ya kituo cha kazi.

Taarifa hiyo ilisema akaunti ya DADPS ndio inaongoza kwa matumizi mabaya, ambapo kati ya sh. milioni 75.5 zilizotumika, zaidi ya sh. milioni  65.3 zililipwa kama posho, milioni 7/- zililipwa katika ununuzi wa mbegu za mihogo na milioni 3.2 zilitumika kulipa bili za umeme, maji na gesi.

Bw. Paul katika taarifa hiyo alishauri wakuu wa idara waliochukua posho zaidi ya mara moja kurudisha posho hizo katika akaunti za idara ikiwa ni pamoja na kutafuta viambatanisho vyote muhimu na kuviambatanisha kwa ajili ya kuhakikiwa.

Hata hivyo baraza hilo mwanzoni liliingia dosari baada ya mwenyekiti wa halmashauri hiyo, kuamua kusitisha mkutano kwa saa moja kutokana na madiwani kushindwa kuelewana baada ya katibu Tawala wa Wilaya, Bw. Erasmus Rutabanzibwa kuwasomewa barua kutoka kwa Katibu Mkuu TAMISEMI ikiwazuia madiwani kutowakataa watendaji wabovu au kumwajibisha Mkurugenzi Mtendaji.

No comments:

Post a Comment