02 May 2011

Taasisi ya kiislamu yadaiwa kuvamia kiwanja

Na Mwandishi Wetu

TAASISI ya African Relief Committee imedaiwa kuvamia kiwanja cha mfanyabiashara Bw. Alex Masama na kufanya ujenzi bila vibali licha ya kuwapo amri ya mahakama
inayozuia shughuli yoyote kuendelea katika eneo hilo.

Akizungumza na Majira hivi karibuni Bw. Msama alisema kwamba kiwanja hicho ni mali yake na anashangazwa ni kwa vipi watu wengine walivamia eneo hilo huku polisi wakiwapa ulinzi, licha ya kuwapo amri ya mahakama ya kuzuia kujengwa kwa kitu chochote mahali hapo.

“Kesi ya kuzuia ujenzi iko mahakamani, sitaki kuingia kwa undani zaidi, lakini ninachojua ni kwamba, kiwanja kile ni mali yangu halali, nina hati zote baada ya kukinunua kwa Benki ya Raslimali Tanzania (TIB), ambacho awali kilikuwa mali ya Benki ya Nyumba,” alisema Msama.

Kwa mujibu wa hati zilizopo, Bw. Msama alinunua kiwanja hicho namba 141/3 na 141/4 Aprili 16, 2003 na kupewa hati miliki yenye namba 84495 Septemba 8, 2009, baada ya kukamilisha taratibu zinazotakiwa.

Baada ya kuibuka kwa taasisi hiyo ya Kiislamu, Bw. Msama alikwenda Manispaa ya Temeke akiwa na hati zake, akipinga zile zilizokuwa zimewasilishwa awali na taasisi hiyo.

Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa iliijibu taasisi hiyo Septemba 4, 2009 ikiitaka kuwasilisha mkataba wa mauziano baina yao na mtu aliyetajwa kwa jina la Farid Ahmed Mbaraka, anayedai kwamba ndiye alikuwa mmiliki wa viwanja hivyo.

Barua hiyo ilisema: “Tumepokea barua kutoka Tanzania Investment Bank Ltd, wakiwa ni warithi wa mali na madeni ya iliyokuwa Benki ya Nyumba Tanzania (THB), wakieleza ya kwamba, hawajawahi kuuza viwanja, hivyo kwa mtu au Taasisi yoyote, isipokuwa ndugu Alex Msama Mwita.”

Pamoja na kuwataka wapeleke haraka vielelezo vyao, taasisi hiyo haikuwahi kufanya hivyo, na taarifa zinasema kila walipoitwa kwenda Manispaa, wao walikimbilia Polisi Mbagala na kupatiwa ulinzi wakati wakiendelea na ujenzi bila hata vibali.

Taarifa zinasema Manispaa iliwahi kumtuma Mhandisi wa Wilaya ya Temeke, Bw. Zacharia kwenda eneo la tukio na alipofika huko, hakuwakuta na vibali vya ujenzi, hivyo kuzuia ujenzi huo usiendelee na kuwataka wahusika wafike ofisini kwake, lakini hawakuwahi kwenda.

Mhandisi Zacharia alipoulizwa kuhusu sakata hilo, alisema hawezi kusema chochote kwa sababu si msemaji, bali atafutwe Ofisa Ardhi wa Wilaya, ambaye hata hivyo hakupatikana.

Taarifa za uchunguzi zinabainisha kwamba, Polisi Wilaya ya Mbagala ndio wanaodaiwa kuwabeba wahusika wa taasisi hiyo na kuwapatia ulinzi huku wakimfukuza mlinzi wa kiwanja hicho aliyewekwa na Bw. Msama.

Habari kutoka ndani ya polisi wilayani hapo zinasema kwamba, askari wadogo wamekuwa wakitoa ulinzi kwa amri ya wakuu wa polisi wa wilaya hiyo ambao wanadaiwa kukaidi amri ya mahakama na manispaa kwa kuruhusu ujenzi uendelee huku wahusika wakiwa hawana vibali.

Juhudi za kumpata wasemaji wa taasisi hiyo kwa siku kadhaa zimegonga mwamba kutokana na simu zao kutokupatikana hewani.

3 comments:

  1. Hii Taasisi mbona inafanya mambo kinyemela? au pesa hizo za misaada hawana uchungu nazo?Wapeleke vibali na hati zao ili wawe na hakki na hicho kiwanja na kama walitapeliwa basi wakae na huyo mmiliki wakubaliane.Wasifikirie wakati wa zamani wa kutoa mlungula mambo yanaishia watapata hasara!! Inakuwaje taasisi ya Kidini inataka kudhulumu na wakati wanajuwa ni dhambi kudhulumu hakki ya mtu?

    ReplyDelete
  2. Hao jamaa ni matapeli wameshakula pesa za African Relief Committee, maana walijenga kibanda pale wakidai ni msikiti wakati eneo ni la viwanda!!Sasa wanatafuta mahali pa kuangukia banda bovu ni matapeli tuu hao

    ReplyDelete
  3. UDINI USIWE NDIO NJIA YA KUHARIBU AMANI KWA WANANCHI.
    kwa nini mahakama isianze kuwachukulia sheria polisi kwanza.
    HAO JAMAA WAMEISHA JIPANGA KWA SHARI LOLOTE LILE KWA HIYO POLISI WASISHANGAE DAMU KUMWAGIKA PASIPO SABABU,heshimuni sheria za mahakama

    ReplyDelete