Na Mwajuma Juma, Zanzibar
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imelitaka Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC) kutowakingia vifua wafanyakazi wasio waadilifu wala
waaminifu.Agizo hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi katika maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi Duniani, yaliyofanyika Bwawani mjini Zanzibar.
Alisema kuwa kufanya hivyo ni kuungana nao katika makosa ya maasi, hasa kwa
vile katika kazi kunahitajika maadili ambayo yatakwenda sambamba na sheria
za kazi.
“Ningependa kuiasa jumuiya kutowakingia kifua wafanyakazi wasio waadilifu,
wabadhirifu, wazembe na wasio waaminifu, pale ambapo waajiri wao
wanapowachukulia hatua na kuwafukuza kazi kwa makosa ya aina hiyo,”
alisema.
Hata hivyo aliwaonya waajiri serikalini na sekta binafsi kuacha
kuwadhalilisha na kuwanyanyasa wafanyakazi wao, hasa makosa ambayo
hawakuyatenda kwa lengo la kuwaachisha kazi.
"Hilo nalo halikubaliki kama hili linatokea jumuiya itakuwa na haki ya
kuwatetea wafanyakazi hao ambao wameonewa, lazima taratibu zifuatwe kwa
mujibu wa sheria zilizowekwa,” alisema Balozi Seif.
Maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi Dunia hufanyika kila ifikapo Mei Mosi ya
kila mwaka ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Ushirikishwaji wa wafanyakazi
katika mambo yanayowahusu ni haki yao sio fursa’.
No comments:
Post a Comment