Na Zahoro Mlanzi
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limesema wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi (Maproo), huenda wakaukosa mchezo wa kirafiki wa kimataifa wa
Taifa Stars dhidi ya Afrika Kusini 'Bafana Bafana'.
Wachezaji hao wataukosa mchezo huo kwasababu haupo kwenye kalenda za Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).
Mchezo huo wa kirafiki unatarajiwa kupigwa mwishoni mwa mwezi huu, ukiwa ni wa kujiandaa na mechi ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, utakaopigwa Juni 4, mwaka huu nchini humo.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura, alisema licha ya mchezo huo kutokuwepo katika kalenda ya FIFA, lakini tayari wachezaji hao wametumiwa barua kupitia klabu zao.
"Sijui kama watapata ruhusa kutoka katika klabu zao, unajua mara nyingi kwa mechi kama hii, timu za Ulaya kumwachia mchezaji wake, inakuwa ngumu, lakini kama TFF tumetuma barua za kuziomba ziwaachie waje kulitumikia taifa lao," alisema Wambura.
Aliwataja wachezaji hao ni Idrissa Rajab (Sofapaka, Kenya), Henry Joseph (Kongsvinger IL, Norway), Abdi Kassim (DT Long An, Vietnam), Dan Mrwanda (DT Long An, Vietnam), Nizar Khalfan (Vancouver Whitecaps, Canada) na Athuman Machupa (Vasalund IF,Sweden).
Alisema kati ya hao, Henry ndiye mwenye nafasi kubwa ya kurudi nchini kwa kuwa ligi ya kwao mpaka sasa bingwa amejulikana na hata timu zinazoshuka daraja, zinajulikana.
Alisema wanaendelea kufanya mawasiliano na Bafana Bafana kujua tarehe ya kucheza nayo, ambapo mchezo huo utapigwa jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wachezaji wanaotarajia kuingia kambini leo ni makipa Juma Kaseja (Simba), Shabani Kado (Mtibwa Sugar) na Shaaban Dihile (JKT Ruvu), mabeki ni Shadrack Nsajigwa, Nadir Haroub 'Canavaro' na Kigi Makasi (Yanga), Aggrey Morris (Azam), Juma Nyoso (Simba), Amir Maftah (Simba).
Wengine ni Nurdin Bakari (Yanga), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Jabir Aziz (Azam), na Mwinyi Kazimoto (JKT Ruvu) na washambuliaji ni Machaku Salum (Mtibwa Sugar), Mrisho Ngasa (Azam), Mohamed Banka na Mohamed Banka (Simba) na John Bocco (Azam).
No comments:
Post a Comment