12 November 2013

VAN PERSIE AIZAMISHA ARSENAL  •   AL AHLY BINGWA AFRIKA
MANCHESTER, Uingereza
  Mholanzi Robin van Persie juzi aliizamisha klabu yake ya zamani, Arsenal akiifungia bao pekee la ushindi Manchester United na kuirejeshea matumaini ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu England.

 Van Persie alifunga bao tamu kwa kichwa akiunganisha kona iliyochongwa kitaalamu na Wayne Rooney dakika ya 27 Uwanja wa Old Trafford.
Kikosi cha Man United kilikuwa; De Gea, Smalling, Vidic/Cleverley dk45, Evans, Evra, Valencia, Jones, Carrick, Kagawa/Giggs dk78, Rooney na Van Persie/ Fellaini dk85.
Arsenal; Szczesny, Sagna, Koscielny, Vermaelen, Gibbs, Arteta/Gnabry dk82, Flamini/Wilshere dk61, Ramsey, Ozil, Cazorla/Bendtner dk78 na Giroud.
CAIRO, Misri
TIMU ya Al Ahly ya Misri, imenyakua taji la Klabu bingwa Afrika baada ya kuicharaza Orlando Pirates ya Afrika Kusini mabao 2-0 katika mechi ya fainali ya pili iliyopigwa juzi katika Uwanja wa Arab Contractors jijini Cairo. Al Ahly, wamejinyakulia kombe hilo kwa mara ya saba.
Hata hivyo, kulikuwa na ripoti za vurugu kuzuka kati ya mamia ya wafuasi wa Al Ahly na polisi nchini Misri, kabla ya mechi kuanza.
Baada ya vurugu kusitishwa mchezaji mkongwe, Mohamed Aboutrika ndiye aliyefunga bao la kwanza dakika ya 54. Dakika ya 78, Ahmed Abdul Zaher aliipatia Al Ahly bao la pili.
Hata hivyo, mabingwa hao wa Misri walipata pigo baada ya beki wake, Sherif Abdel Fadil kutolewa na mwamuzi kwa kadi nyekundu kutokana na kumfanyia dhihaki mchezaji wa Orlando Pirates, Daine Klate.
Pirates, ambao ni mabingwa wa mwaka 1995, walicheza kwa nguvu zote, lakini walikosa nguvu baada ya Al Ahly kupata bao la pili katika mechi hiyo iliyokuwa na mashabiki lukuki.
Hata hivyo, mabingwa hao wa Afrika Kusini walikosa nafasi nyingi za kufunga katika mechi hiyo.
Baada Al Ahly kunyakua kombe hilo walizawadiwa kitita cha dola milioni 1.5 za Marekani, Pia watawakilisha Afrika katika Kombe la Dunia la Klabu Bingwa Duniani litakalofanyika nchini Morocco mwezi ujao.
Kabla ya mechi hiyo mamia ya mashabiki wa Ahly walikabiliana na polisi ambao walilazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya mashabiki waliokuwa wakitupa mawe huku wakilazimisha kuingia uwanjani kwa nguvu.
Ni mechi ya kwanza kubwa, ambako mashabiki waliruhusiwa kuingia uwanjani tangu mashabiki wa Al Ahly, walipouawa katika mechi iliyokumbwa na vurugu mwaka jana.

No comments:

Post a Comment