12 November 2013

CHADEMA KUIBURUZA CDA KORTINI



Na Elizabeth Joseph, Dodoma
  Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimepanga kuiburuza mahakamani Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kwa kosa la kubomoa nyumba za wananchi bila fidia.

Uamuzi huo ulitolewa juzi na Mkurugenzi wa Organizesheni na Mafunzo Taifa (CHADEMA), Benson Kigaila wakati akihutubia wananchi katika mikutano wa hadhara uliyofanywa katika Kata ya Mkonze na Kikuyu Kusini mkoani humo ambapo alisema kuwa hivi karibuni wakazi wa maeneo hayo walitangaziwa kubomolewa nyumba zao na CDA kwa madai kuwa wameyavamia.
Kigaila aliwataka wananchi wanaoishi katika maeneo hayo kujiorodhesha majina yao ili kupitia chama hicho waweze kutafuta wakili kwa ajili ya kuweka pingamizi la kusitisha ubomoaji huo.
Kigaila alisema kuwa CDA ilitakiwa kufanya kazi ya kustawisha mji na kuondoka lakini cha kushangaza hadi leo bado iko Dodoma na kuwanyanyasa wananchi kwa kuwauzia viwanja kwa bei ya kiasi kisichopungua milioni 5 pindi wanapohitaji viwanja na wakati mwingine kufukuzwa katika ardhi ambazo wamezikuta toka enzi za mababu zao jambo ambalo ni kuwanyima haki ya kumiliki ardhi yao.
  Hivyo ili kutetea haki ya wananchi chama hicho kimeona ni vyema kuungana na wananchi katika kuishtaki Mamlaka hiyo ili kujua suluhu ya wakazi wa mkoa huu .
  Aliongeza kuwa hata chama kilichopo madarakani (CCM) kimekuwa kikifumbia macho kero za wananchi wa mkoa huu kuhusiana na Mamlaka hiyo kwani taarifa juu ya CDA inajulikana lakini kimekuwa kikipiga danadana katika kutoa uamuzi wa kuiondoa mamlaka hiyo ili wazawa waweze kujua suluhisho la maisha yao katika kumiliki ardhi ambayo walifukuzwa bila kulipwa fidia.
  Aidha, aliwataka wananchi kwa pamoja kupinga suala la CDA kuvunja maeneo yao bila fidia na kuungana na chama hicho katika kutetea haki yao ili waweze kuishi kwa amani katika ardhi ya nchi yao pamoja na kuwataka wananchi kuondoa ukereketwa wa vyama ili kufanikisha suala hilo.
  Mkazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mussa Ndalu katika Kata ya Mkonze alisema kuwa Chama kilichopo madarakani ndio kinaoongoza kwa kuwagawanya Watanzania kwa kuyafumbia macho malalamiko ya wananchi juu ya umiliki wa ardhi ya nchi yao huku wageni wakipewa kipaumbele katika suala hilo.

No comments:

Post a Comment