07 November 2013

SAKATA LA UJANGILI :CHINA YAJITOSA

  • NI BAADA YA RAIA WAKE WATATU KUNASWA NA KAGASHEKI
  • SASA KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KUPAMBANA NA UHALIFU

 Hussein Makame, MAELEZO na Penina Malundo
  Serikali ya China imesema itashirikiana na Tanzania kufanya uchunguzi wa tuhumu zanazowakabili raia watatu wa nchi hiyo wanaodaiwa kukamatwa wakiwa na meno ya tembo 706 jijini Dar es Salaam hivi karibuni.


Hayo yalisemwa na Naibu Mkuu na Mshauri wa Masuala ya Kisiasa wa Ubalozi wa China nchini Tanzania, Li Xuhang, wakati alipozungumza na waandishi wa habari kwenye ubalozi wa nchi hiyo, jijini Dar es Salaam.

  Alisema Balozi wa China nchini Dkt. Lu Youqing pamoja na ubalozi wake wanalaani vikali kitendo hicho cha mauaji ya tembo na magendo ya meno na kwamba nchi hiyo iko tayari kushirikiana na Tanzania kupambana na wahalifu.

  Aliongeza kuwa Serikali ya China inaunga mkono kwa dhati Serikali ya Tanzania kupingana na magendo ya meno ya tembo na Jeshi la Polisi la nchi yake linapenda kushirikiana na Jeshi la Polisi la Tanzania kupambana na wahalifu.

  Alifafanua kuwa ubalozi huo umestushwa na habari hiyo iliyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini na kwamba sasa upande wa China unafanya uchunguzi kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili kupata uhalisia wa habari hiyo.

  "Jana (juzi) na leo (jana) tumepeleka maofisa wa Ubalozi wetu ku chunguza kwanza kuthibitisha utambulisho wa watu hao na pia tumeliambia Jeshi la Polisi kwamba hawa watu watatu kama ni raia wa China haki zao za msingi lazima zilindwe," alisema Xuhang.

  Aliongeza kuwa; "Tumeamua kufanya uchunguzi wa kina kwa sababu hatuwezi kufanyia kazi taarifa za vyombo vya habari, hivyo lazima tuthibitishe taarifa hizi na ikiwa ni za kweli tutakuwa tayari kuisaidia Serikali ya Tanzania kuwafikisha mahakamani wahusika."

  Alifafanua kuwa kufanya magendo ya meno ya tembo ni kosa kubwa la jinai kwa nchi ya China na adhabu kali inatolewa kwa mtu anayepatikana na kosa hilo ikiwemo kama atakutwa na kilo sita za meno hayo anafungwa jela miaka kumi au zaidi.

 "Ikiwa utapatikana na hatia ya meno ya tembo ya zaidi ya kilo sita unaweza kuhukumiwa jela miaka zaidi ya kumi au kunyongwa kabisa, kwa hiyo Serikali ya China inaongoza duniani kwa kutoa adhabu kali kwa kosa hilo," alisema Xuhang.

  Aliwataka raia wote wa China wanaoishi Tanzania kufuata Sheria za China na za Tanzania na kwamba wasifanye kitendo chochote kinachokwenda kinyume na sheria kama vile kufanya magendo ya meno ya tembo

No comments:

Post a Comment