27 November 2013

HOSEAH AULA SHIRIKISHO LA RUSHWA DUNIANI



Na Mwandi shi Maalumu, Panama
 Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Dkt. Edward Hoseah, amechaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa Duniani (IAACA).


Dkt. Hoseah alichaguliwa na wajumbe 460 wa Mkutano Mkuu wa saba wa shirikisho hilo kutoka nchi mbalimbali uliofanyika Panama, Amerika ya Kati kuanzia Novemba 22-24, mwaka huu.

Wajumbe wa mkutano huo ni pamoja na wakuu wa taasisi 98 za Kuzuia na Kupambana na Rushwa Duniani ambapo kaulimbiu ya mkutano huo inasema, "Utawala wa Sheria na Rushwa: Changamoto na Fursa Zilizopo".

Kabla ya kuchaguliwa katika nafasi hiyo, Dkt. Hoseah alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Utendaji katika shirikisho hilo ambapo kutokana na uteuzi huo, anakuwa Mwafrika wa kwanza kushika wadhifa huo mkubwa katika mapambano dhidi ya rushwa duniani.

Uchaguzi huo ni heshima kubwa kwa Tanzania na Bara la Afrika pia ni fursa nzuri kwa Dkt. Hoseah kuonesha uwezo wake wa kuongoza mapambano dhidi ya rushwa kimataifa. Nyadhifa nyingine za kimataifa ambazo Dkt. Hoseah amewahi kuzishikilia ni pamoja na Rais wa

 Kwanza wa Shirikisho la Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa Afrika Mashariki (2007-2008), Rais wa kwanza wa Jukwaa la Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika nchi za SADC (SAFAC-2010-2011).

Nyingine ni Mwenyekiti wa Bodi ya Umoja wa Afrika ya Ushauri wa Masuala ya Rushwa (AU-ABC 2011-2012).

IAACA linajumuisha taasisi 298 pamoja na wanachama zaidi ya 2,000 kutoka katika asasi mbalimbali zisizo za kiserikali na lilianzishwa Aprili 19, 2006, Makao Makuu yapo Peking, China.

Lengo la kuanzishwa kwa shirikisho hilo ni kuziwezesha nchi wanachama kutekeleza Mkataba wa Umoja wa Mataifa Dhidi ya Rushwa uliopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Desemba 30, 2003.

1 comment:

  1. Hongera sana kwa uteuzi huo , inaonyesha jinsi gani tanzania tulivyo na watu we nye uwezo tunakutakia kila la kheri katika huo uteuzi wako, hiyo iwe changamoto kwetu kuhusu vita dhidi ya rushwa

    ReplyDelete