27 November 2013

TZ KUTUNZA NYARAKA ZA MAUAJI YA KIMBARI Na Penina Malundo
  Tanzania imeingia mkataba na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN), kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kutunzia nyaraka zinazohusiana na kesi za mauaji ya kimbari nchini Rwanda.

  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.
  Alisema jengo hilo litagharimu dola za Marekani milioni tano sawa na sh. bilioni nane za Tanzania na litajengwa mjini Arusha katika eneo la Lakilaki.
  "Jengo hili litaweza kuhifadhi nyaraka hizo muhimu pamoja na vielelezo mbalimbali vya kesi za kimbari...mafaili yote ya kiutendaji na kiufundi yatahifadhiwa humo," alisema.
  Bw. Membe alisema, nchi tatu ambazo ni Tanzania, Kenya na Rwanda, ziliomba ujenzi wa jengo hilo katika nchi zao ambapo baraza hilo, limeridhia jengo hilo kujengwa Tanzania.
  Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Sheria kutoka Umoja wa Mataifa, Miguel de Serpa Soares, alisema baraza hilo limeridhia ujenzi huo ufanyike nchini kutokana na mahusiano mazuri yaliyopo. kati yao na Tanzania.

No comments:

Post a Comment