27 November 2013

WAJASIRIAMALI WAONYWA KUHUSU SIASA





 Na Suleiman Abeid, Shinyanga


Wanachama wa vikundi vya wajasiriamali wadogo katika kata ya Kitangili Manispaa ya Shinyanga wametakiwa kuepuka kuingiza siasa katika vikundi vinginevyo vitasambaratika
.
Tahadhari hiyo ilitolewa juzi na diwani wa viti maalumu (CCM) manispaa ya Shinyanga, Mariamu Nyangaka, alipokuwa akizungumza na viongozi wa vikund imbalimbali vya wajasiriamali waliokutana kwa ajili ya kuanzisha Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS ).
Nyangaka alisema viongozi wa vikundi vya wajasiriamali pamoja na wanachama wao kwa ujumla wanatakiwa kuhakikisha wanaendesha shughuli zao bila kuingiza au kutanguliza itikadi ya vyama vya siasa katika vikundi vyao kitu ambacho kinaweza kusababisha mgawanyiko miongoni mwao.
Alisema wapo baadhi ya wanasiasa wanaotumia wajasiriamali wadogo kufikia malengo yao waliyojipangia huku wengine wakidiriki hata kuwazuia wafuasi wa vyama vyao wasishirikiane na watu ambao si wafuasi wa vyama vyao vya siasa hata kama shughuli zao zinapaswa kuendeshwa kwa ushirikiano wa pamoja.
"Ndugu zangu mkakati ambao mnataka kuuanzisha ni mkakati mzuri utawasaidia kuendesha shughuli zenu kwa ufanisi mkubwa, mtakapokuwa na SACCOS yenu itawasaidia kuweza kupata mitaji ya kuendesha biashara zenu kupitia mikopo mtakayokopa yenye masharti nafuu tofauti na inayotolewa na benki zetu nyingi nchini,"alisema.
"Lakini naomba mjihadhari na siasa katika vikundi vyenu, mkimruhusu mdudu huyu kuwa miongoni mwenu eleweni wazi hamtadumu kwa kipindi kirefu, hakikisheni mnaendesha shughuli zenu bila kuchanganya na itikadi za kisiasa na wakemeeni wale wote watakaoonesha dalili za kuingiza siasa ndani ya vikundi," alisema Nyangaka.
Kwa upande wake ofisa ushirika kutoka manispaa ya Shinyanga, Athumani, alisema serikali kwa kipindi kirefu imekuwa ikihimiza umuhimu wa wananchi kujiundia vyama vyao vya ushirika wa akiba na mikopo (SACCOS) kwa vile ni rahisi zaidi kusaidiwa na asasi mbalimbali za kifedha. Alisema kupitia SACCOS watu wengi wamefanikiwa katika biashara zao na baadhi wameweza kujenga nyumba za makazi huku wengine wakisomesha watoto wao bila matatizo. Alisema jambo la msingi ni uaminifu wa viongozi wa SACCOS zinazoanzishwa kwa kuhakikisha zinakuwa na wanachama waadilifu na wenye kuzingatia sheria za uendeshaji wa ushirika huo.
Katika hatua nyingine, viongozi hao wa vikundi vya wajasiriamali wadogo wameunda uongozi wa muda utakaosimamia taratibu za uanzishwaji wa ushirika wa akiba na mikopo.
Alisema utaundwa na vikundi vyote vilivyopo katika kata ya Kitangili na kuhakikisha SACCOS hiyo inasajiliwa kisheria ili iweze kuanza kazi mara moja.
Viongozi wa muda waliochaguliwa Elias Joseph (Mwenyekiti), Richard Maige (mwenyekiti msaidizi), Patrick Kileo (katibu), Masunga Elias (katibu msaidizi) ambapo Timothy Kakiri, alichaguliwa kuwa mweka hazina.

No comments:

Post a Comment