03 October 2013

VURUGU TENA

Vijana wakinawa uso baada ya polisi kupiga mabomu ya machozi
Wakazi wa Mbeya wakikimbia baada ya polisi kupiga mabomu ya machozi.
  • WAFANYABISHARA WAZIPINGA MASHINE ZA TRA

 Na Esther Macha, Mbeya

  Vurugu kubwa zimeibuka mkoani Mbeya jana baada ya Jeshi la Polisi kulazimika kutumia mabomu ya machozi ili kuwatawanya wafanyabiashara waliokuwa wakipinga agizo la Serikali linalowataka watumie mashine za kieletroniki kutoa risiti kwa wateja wanaonunua bidhaa zao.


Polisi walitumia mabomu hayo na maji ya kuwasha katika mitaa mbalimbali ya eneo la Mwanjelwa hadi Viwanja vya Shule ya Msingi Ruanda Nzovwe. Gari lililokuwa na askari polisi, lilitoa matangazo ya hali ya hatari kuwataka wananchi wasitoke nje katika nyumba zao.

Mabomu mengine yalipigwa katika Uwanja wa Shule ya Msingi Kagera, uliopo eneo la Soweto ambapo hali ya taharuki ilijitokeza baada ya mabomu hayo kuwaathiri wanafunzi waliokuwa darasani wakisoma ambao walianza kukimbia ovyo na wengine kuzimia.

Wafanyabiashara hao wanapinga agizo la Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), kuwataka kununua mashine hizo ili kukatia risiti kwa wateja wanaonunua bidhaa zao.

Vurugu hizo zimetokea siku moja baada ya Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Abbas Kandoro, kukutana na viongozi wa wafanyabiashara wa Soko la Sido ambapo katika kikao hicho aliwataka viongozi hao kuwajulisha wenzao wasiitishe mkutano waliotaka kuufanya jana katika Uwanja wa Shule ya Msingi Runda Nzovwe.

Bw. Kandoro alilazimika kukutana na viongozi hao baada ya gari la matangazo kupita mitaa mbalimbali ya jiji hilo likiwataka wafanyabiashara kufunga maduka yao siku ya jana na kufika katika uwanja huo ili kujadili matumizi ya mashine hizo.

Baada ya Bw. Kandoro kusikia ujumbe huo, ilidaiwa dereva wa gari hilo alikamatwa na Jeshi la Polisi pamoja na Mwenyekiti wa Soko la Sido ambao waliwekwa ndani kwa muda usiojulikana.

Wafanyabiashara hao walikataa kusitisha mkutano huo hivyo kuendelea na maandalizi ambapo jana asubuhi, walikodi gari lingine na kuwatangazia wenzao wajitokeze kwa wingi katika mkutano kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi na Runda Nzovwe.

Kutokana na msimamo huo, polisi walifika eneo hilo ili kuwazuia wafanyabiashara hao wasifanye mkutano huo kwa kupiga mabomu ya machozi na kutumia maji ya kuwasha.

  Akizungumza na Majira, mmoja wa wafanyabiashara hao, Bw. Alex Oswald, alisema waliamua kufunga maduka yao kwa hiari waweze kufanya mkutano ili watoke na msimamo wa kuiomba Serikali itoe mashine hizo bure kwa wafanyabiashara badala ya kuwauzia.

  Mfanyabiashara mwingine wa Soko la Sido, Bw. Peter Tweve, alisema wao hawajagoma kutumia mashine hizo bali wanataka wapewe bure kwani si kila mfanyabiashara anayeweza kununua kwa sh. 800,000 kiasi ambacho ni kikubwa ukilinganisha na mitaji yao.

  Alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo, Bw. Kandoro alisema yupo katika kikao ambapo simu ya Kamanda wa Polisi mkoani humo, Diwani Athumani, ilikuwa ikiita bila kupokelewa.

  Vurugu hizo zimetokea wiki moja tangu Mkurugenzi wa Elimu ya Kodi Makao Makuu ya TRA, Richard Kayombo, kutoa taarifa zinazosema kuwa, mwisho wa kununua mashine hizo ni Oktoba 14, mwaka huu.

  Taarifa zaidi zinaeleza kuwa, masoko yote ya Uyole na Mbalizi, hakuna duka lililokuwa limefunguliwa siku ya jana na polisi waliendelea kupiga mabomu ili kuwatawanya wananchi.

4 comments:

  1. mashine hizi ni mradi tu wa wakubwa mambo ya ten pacent inashangaza vipi nchi zilizoendelea km china india thailand nk hawatumii mashine hizi ila ktk super market na maduka makubwa leo hapa bongo eti ndo tumeendelea hata machinga watumie mashine Pole Rais Kikwete mafisadi wanakuandama katika kila sekta

    ReplyDelete
  2. Hayo maisha bora kwa TRA tu? waache watanzania nao wajikwamue, tafuteni kodi kwenye vyanzo vingine kama madini

    ReplyDelete
  3. muuza duka ni wakala tu wa TRA ni vipi anunue hiyo mashine kwa sh.800,000 badala ya kugawiwa bure. Aafu RC na wewe acha kutoa amri haraka haraka bila hata ya kuwa na mazungumzo na wahusika. huoni kama unaanzisha vurugu ? MOLMOLI BEE.

    ReplyDelete
  4. Hizo mashine mbona zinatofautiana bei na TRA inawalazimisha wafanyabiashara kununua mashine hizo sehemu moja tu wakati mashine hizo zinauzwa sehemu mbalimbali huo ni ufisadi wa viongozi wa TRA.

    ReplyDelete