03 October 2013

MAJAMBAZI WATEKA BASI

  • WAPORA MAMILIONI,WAJERUHI ABIRIA


Na Damiano Mkumbo, Singida
   Majambazi waliokuwa na silaha, wameliteka basi la Kampuni ya Taqwa linalofanya safari zake kati ya Bunjumbura, Burundi na Dar es Salaam. Katika tukio hilo, abiria waliokuwa ndani ya basi hilo waliporwa fedha za Kitanzania zaidi ya sh. milioni tano pamoja na dola za Marekani 160,000.

Tukio hilo limetokea juzi saa 4 usiku katika Kijiji cha Milade, Kata ya Iguguno, Wilaya ya Mkalama, mkoani Singida, Barabara Kuu ya Singida-Shinyanga. Basi hilo lilikuwa na abiria 51 ambapo majambazi hao walitega mawe makubwa katika eneo lenye daraja.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Geofrey Kamwela, alisema licha ya majambazi hao kupora fedha na mali za abiria, pia waliwapiga, kuwajeruhi kwa marungu na mawe.
 “Abiria 19 walijeruhiwa na kupelekwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Singida, basi lililotekwa lina namba T 298 BLD, aina ya Nissan Disel BLD likitokea Bunjumbura kwenda Dar es Salaam, likiendeshwa na Bw. Ahmed Seif (39), akiwa  na abiria kutoka nchi za Rwanda, Burundi na Congo (DRC).
  “Baada ya kufika eneo lililowekwa kizuizi cha mawe makubwa, dereva alijaribu kupita lakini tairi mbili za mbele zilipasuka
hivyo gari liliacha barabara na kuserereka chini umbali wa meta 100 na kusimama,” alisema Kamanda Kamwela.
  Alisema baada ya basi hilo kusimama, watu wapatao sita wakiwa na marungu, mawe walilivamia basi hilo, kuvunja madirisha,kuingia ndani na kuwaamuru abiria wateremke chini.
  Kamanda Kamwela alisema majambazi hao walianza kumpora abiria mmoja mmoja vitu mbalimbali kama fedha, simu, kamera za mnato na mabegi madogo huku wakiwapiga.
“Katika tukio hili, abiria 28 waliporwa kati yao 19 wanaume na wanawake 12, pia kuna abiria ambao walijeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao,” alisema.
  Aliongeza kuwa, mmoja kati ya majambazi hao alikuwa ndani ya basi hilo akiwasiliana na wenzake ambaye ndiye aliyekuwa akiwalazimisha abiria kuteremka chini wakiwemo wanafunzi watano wa Vyuo Vikuu vya Harare na Maputo.
  Alisema polisi walifika eneo la tukio dakika 20 baada ya watu hao kufanya uhalifu huo na kukimbia kusikojulikana. Daktari wa zamu katika hospitali hiyo, Dkt. Banuba Deogratius, alisema wanaume 12 na wanawake saba walipokelewa, kupatiwa matibabu na kuruhusiwa.
  Kamanda Kamwela alisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi ili kuwanasa watu hao hivyo aliwaomba wananchi watoe taarifa polisi zinazohusiana na viashiria vya kuonekana watu hao.
 

No comments:

Post a Comment