04 October 2013

WARUNDI KUWACHEZESHA TANZANIA, MSUMBIJI
Na Fatuma Rashid

    Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limeteua waamuzi kutoka Burundi kuchezesha mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kwa wanawake chini ya miaka 20 kati ya Tanzania na Msumbiji

 .Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema waamuzi watakaochezesha mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya Oktoba 26 na 27 mwaka huu wataongozwa na Ines Niyonsara akisaidiwa na Jacqueline Ndimurukundo na Axelle Shikana.
   Wambura alisema, Irene Namiburu kutoka Uganda ndiye atakayekuwa mwamuzi wa mezani wakati Kamishna wa mechi hiyo atakuwa ni Evelyn Awuor wa Kenya.Alisema mechi ya marudiano itachezwa jijini Maputo, kati ya Novemba 9 na 10, mwaka huu na itachezeshwa na waamuzi kutoka Madagascar.
   Fainali hizo za Kombe la Dunia zitafanyika mwakani nchini Canada, ambapo Tanzania inashiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo ya Kombe la Dunia kwa wasichana.Timu ya Tanzania tayari imepiga kambi mkoani Pwani ikiwa chini ya Kocha wake Rogasian Kaijage.

No comments:

Post a Comment