- KUNDECHA ATANGAZA KUJIUNGA NA WAPINZANI
Na Mariam Mziwanda
Viongozi wa vyama vilivyoingia ushirikiano vya CHADEMA, CUF na
NCCR -Mageuzi, wamesema, mchakato wa kupata katiba mpya lazima
ufanyike kwa maridhiano, vinginevyo vitisho, dharau na kupuuza baadhi ya maoni
hakutasaidia kupatikana kwa mwafaka.
Viongozi wa vyama hivyo wametoa kauli
hiyo ikiwa ni siku moja baada ya Rais Jakaya Kikwete, kuelezea kushangazwa na
uongo wa baadhi ya wanasiasa hasa madai kwamba aliteua wajumbe wa Tume ya
Katiba bila kuongozwa na mapendekezo ya wadau mbalimbali waliopendekeza majina
hayo.
Wakizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana
viongozi hao ambao ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CUF,
Prof. Ibrahim Lipumba na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema
mchakato huo unahitaji maridhiano.
Mbowe alisema ikiwa Rais atachukulia
kwa mzaha suala hilo
na kuamua kusaini mswada huo bila kutafakari kwa mapana yake nchi itaingia
kwenye machafuko.“Tunarudia kumshauri na kumsihi Rais
Kikwete kwamba katiba ni haki ya Watanzania wote, hivyo inahitaji busara,
ushirikiano, uvumilivu, staa, kuangalia maslahi, kuaminiana na vitu vingine kama hivyo,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Kamwe hatuwezi kupiga magoti kwa
kuomba katiba mpya, katiba sio zawadi kwa wanasiasa na hatupiganii kupatikana
kwa katiba nzuri kwa maslahi yetu wenyewe, bali kwa maslahi ya Watanzania
wote.”Kwa upande wake Profesa Lipumba,
alisema Rais Kikwete ameanza kuonesha dharau kwa mambo yenye maslahi makubwa
kwa taifa.
“Kwanza naomba niseme kwamba Rais
Kikwete ndiye hajaeleza ukweli kwa Watanzania wanaoishi California, nchini Marekani,” alisema.Naye Mbatia alisema kama
Rais Kikwete anadai ametumia mapendekezo ya wadau kuteua wajumbe, anapaswa
kuweka wazi anayewakilisha kundi la walemavu.
Mbatia alisema Shirikisho la Watu Wenye
Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) lilipendekeza majina matatu ili achaguliwe
mmojawapo, lakini wote walitupwa nje na kufanya kundi hilo kujiona halina umuhimu ndani ya jamii.“Kama
kweli anajua ameongozwa na mapendekezo hayo atueleze kila kundi limewakilishwa
na nani, yapo mambo mengi tunayolalamikiwa tunataka haki itendeke kwa kila
Mtanzania,” alisema.
Kwa upande wa Amiri Mkuu wa Baraza Kuu
la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Mussa Yusuph Kundecha,
alisema wameungana na upinzani kudai katiba inayokidhi matakwa ya Watanzania.“Tumejadiliana na kuafikiana kuungana
ili katiba ipatikane yenye mawazo ya makundi yote, kwa bahati nzuri malalamiko
yetu waislamu yamekuwa na uwiano sawa na malalamiko ya wapinzani.
“Sasa kama wote
tumekutana na wazo au shida moja lazima tuamue tufanye nini ili tupate jibu,
sasa tunataka mswada urudi bungeni ujadiliwe upya ili kuondoa upungufu uliopo
na vipengele vilichomekwa kinyemela.”
No comments:
Post a Comment