20 September 2013

MSAJILI MPYA AISHUKIA CCM



  • ASEMA NI KINYUME CHA SHERIA, ATOA ONYO KALI
  • NI KWA KUMTUMIA BALOZI WA CHINA KUFANYA SIASA


 Na Leah Daudi
MSAJILI mpya wa Vyama vya Siasa Nchini, jaji Francis Mutungi amekemea vikali kitendo cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumshirikisha balozi wa China nchini, Lu Younqing, katika shughuli za kisiasa.Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam na kusainiwa na Jaji Mtungi, ilisema kuwa amesikitishwa na suala la ushiriki wa raia wa kigeni katika mambo ya kisiasa hapa nchini.

Alisisitiza kuwa jambo hilo lipo kinyume na taratibu za kisheria.“Nimechukizwa na kitendo cha CCM kumruhusu raia wa kigeni kutumia jukwaa lake kufanya siasa, jambo hili si jema na limeweza kuzua hali ya taharuki kwa wananchi,” alisema jaji Mutungi na kuongeza;
“Nachukua fursa hii kama mlezi wa vyama vya siasa kwa ujumla kuzingatia na kufuata sheria na taratibu stahiki katika utekelezaji wa shughuli zao za kisiasa.”Hivi karibuni Katibu Mkuu wa CCM, Abdurahaman Kinana, akiwa mkoani Shinyanga, alimpandisha Balozi huyo wa China, Lu Younqing, akiwa amevaa kofia ya chama hicho na kumtaka aeleze miradi ambayo nchi yake inakusudia kutekeleza kwa Tanzania.
Kitendo hicho tayari kimelalamikiwa vikali na chama kikuu cha upinzani, CHADEMA ambapo kimetishia kuuandikia barua Umoja wa Mataifa (UN) kuhusiana na kitendo hicho kwani kinaenda kinyume na mikataba ya kimataifa.Pia Serikali tayari imeingilia kati suala hilo na kuwataka mabalozi wote wanaowakilisha nchi zao nchini kutambua kuwa wanawajibika kuheshimu mkataba wa kimataifa wa Vienna unaoainisha taratibu za kidiplomasia.
Tayari Serikali imesema kuwa inajiandaa kumwandikia barua balozi huyo ili kumkumbusha wajibu wake baada ya kukusanya taarifa zote za tukio hilo.Hata hivyo, CCM kupitia Katibu wake wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Nape Nnauye, amekuwa akitetea kitendo hicho cha chama hicho kumsimamisha balozi huyo jukwaani.
Katika hatua nyingine, jaji Mutungi, alisema ofisi yake ipo kwenye mchakato wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa kutokana na iliyopo sasa kubainika kuwa na upungufu.Alisema lengo la hatua hiyo ni kukabiliana na changamoto zilizopo. Alisema ofisi yake inaendelea kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwa ni jitihada ya kufanikisha marekebisho hayo ya sheria.

No comments:

Post a Comment