Na John Gagarini, Kibaha
MATUKIO ya uvunjifu wa
maadili kwenye shule mbalimbali hapa nchini yameendelea kushamiri baada ya
wanafunzi wanne wa Shule ya Msingi Lulanzi wilayani Kibaha mkoani Pwani
kutuhumiwa kumbaka mwanafunzi wa darasa la pili na kumsababishia maumivu
yaliyopelekea kulazwa Hospitali ya Tumbi kwa matibabu.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana babu wa mtoto huyo,
Jacob Mrope alisema tukio hilo lilitokea Septemba 2 saa 6 mchana ambapo mjukuu
wake ambaye ni yatima alikuwa akitoka shuleni huku akiwa na wenzake wawili
wakike, walikimbizwa na watuhumiwa hao ambapo yeye alishindwa kukimbia kutokana
na kuumia mguu na kujikuta akibakwa.
Mrope alisema kuwa wanafunzi wenzake aliokuwa nao walisema kuwa
baada ya watuhumiwa hao kumkamata walimziba mdomo kisha wakaanza kumuingilia
kwa zamu ambapo mwanafunzi huyo hakuweza kupata msaada wowote hadi watuhumiwa
hao kutimiza haja zao.
"Wenzake waliokuwa nao walitoa taarifa nyumbani kwa mlezi
wake ambaye ni dada yake ambapo alikwenda na kumkuta akitokwa na damu nyingi na
alipomuuliza alisema kuwa wenzake wamembaka ndipo alimchukua na kumpeleka
shuleni kutoa taarifa," alisema Mrope.
Kwa upande wake dada yake Lwiza alisema kuwa yeye alipata taarifa
kupitia kwa wanafunzi hao ambao alikuwa nao wakati wanatoka shule na kukimbizwa
na watuhumiwa hao, ambapo walisema kuwa ilibidi warudi na kumkuta mwenzao
akitokwa damu, wamkokota mwenzao hadi nyumba iliyojirani na kumjulisha.
"Alikuwa kwenye hali mbaya kwani alikuwa akitokwa na damu
nyingi na nilipomuuliza alisema kuwa amebakwa na mtuhumiwa ambaye alimtambua na
kumtaja jina mwenye umri wa miaka 10 akiwa na wenzake watatu," alisema
Lwiza.
Lwiza alisema kuwa baada ya kuona hali ile walimpeleka shule na
uongozi wa shule ukamwelekeza kufuata taratibu za kisheria ambapo walikwenda
Serikali ya mtaa kisha kwenda polisi na baadaye Hospitali ya Tumbi kwa matibabu
zaidi ambapo hadi juzi mwanafunzi huyo alikuwa bado kalazwa na hali yake
inasemekana kuwa ni mbaya.
Naye Mwalimu mkuu wa shule hiyo ya Lulanzi, Anna Bilali alisema
kuwa wao kama uongozi wa shule hawawezi kusema lolote kwani suala hilo liko
kwenye vyombo vya sheria pamoja na kitabibu na watakuwa tayari kusema mara
taarifa zitakapokamilika.
"Ni kweli tukio hili limetokea lakini bado haijathibitishwa
kama ni kweli au la na pia lilitokea nje ya shule na muda wa shule kwa
wanafunzi wa madarasa ya chini walisharuhusiwa kurudi nyumbani mara baada ya
masomo kwisha," alisema Bilali.
Akizungumzia tukio hilo mjumbe wa mtaa wa Lulanzi, Rasul Shaban
alisema kuwa walipata taarifa hiyo na kushangazwa na kitendo hicho ambapo tukio
hilo ni la mara ya kwanza kutokea katika shule hiyo ambayo iko kwenye mtaa huo
na pia walitoa barua za kuwadhamini wanafunzi wanaotuhumiwa kufanya tukio hilo.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi
mkoani Pwani Ulrich Matei alisema kuwa hadi sasa wanawashikilia wanafunzi wanne
wenye umri kati ya miaka 10 na 13 kuhusiana na tukio hilo.
No comments:
Post a Comment