Na Said Njuki, Arusha
Wakati ujangili wa meno ya tembo na
faru ukiinyima usingizi Serikali, Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA)
limewashtukia baadhi ya watumishi wake kutokana na kujihusisha na mtandao wa
ujangili kwa kushirikiana na baadhi ya watendaji wa vyombo mbalimbali vya dola.
Kutokana na
hali hiyo TANAPA inakusudia kubadili mfumo wake wa kiutendaji kutoka wa kiraia
na kuwa mfumo kamili wa kijeshi kwa watumishi wote ili kujiimarisha katika
kukabiliana na janga la ujangili nchini.
Meneja Uhusiano
wa TANAPA, Pascal Shelutete, aliwaambia waandishi wa habari jana mjini hapa
kuwa Serikali haiwezi kuona maliasili ambazo ni urithi wa Watanzania na dunia
kwa ujumla, zikiteketezwa na majangili na kuikosesha mapato Serikali.
Alisema lazima juhudi za makusudi
zichukuliwe licha ya majangili hao kuwa na mtandao. Alisema ujangili hasa wa
meno ya tembo na faru ni mtandao wa kimataifa unaohusisha watu wa kada
mbalimbali, huku majangili hao wakitumia fedha nyingi na vifaa vya kisasa
zikiwemo silaha za kivita, hali inayokwamisha jitihada za Serikali za kupambana
na uhalifu huo.
Shelutete alisema Shirika kwa kutumia
vyombo vyake vya kiintelejensia vinawachunguza baadhi ya watumishi wake
wanaojihusisha na mtandao huo na watakapogundulika na kujiridhisha watachukuliwa
hatua kali za kisheria.
"Shirika linaendelea kuchunguza na
kuchukua hatua mbalimbali za kinidhamu na kisheria kwa wafanyakazi wanaobainika
kujihusisha na vitendo vya ujangili kwa kushirikiana na vyombo vya
dola...uchunguzi unaendelea kufanyika kwa baadhi ya wafanyakazi na ushahidi wa
kisheria utakapokamilika kwa wanaojihusisha na mtandao huo hatua za kisheria
zitachukuliwa," alisema Shelutete
"Tumepokea tuhuma dhidi ya baadhi
ya watumishi wetu kujihusisha na ujangili, huo ni mwanzo mzuri kwetu katika kuchunguza
tuhuma hizo kwa kutumia vyombo mbalimbali... hatukatai kuwa Shirika linaweza
kuwa na watumishi wa aina hiyo, bali uchunguzi wa kina utafanyika ili
tusimwonee mtu," alisema.
Alisema shirika linajua ukubwa wa
tatizo, hivyo linajiandaa kwa mikakati mbalimbali ili kukabiliana na ujangili
na tayari uimarishaji wa doria za magari, miguu na matumizi ya mbwa hifadhini
kote nchini hali inayodhihirisha kupunguza kwa kiwango cha vitendo hivyo.
Alitoa mfano wa hifadhi za Tarangire na
Ziwa Manyara akieleza kuwa katika kipindi cha miezi sita iliyopita ujangili
ulikuwa umeshika kasi umedhibitiwa kwa asilimia 100 kwa maana hakuna tembo hata
mmoja aliyeuawa.
Alitaja mikakati mingine kuwa ni pamoja
na kuanzishwa kwa kikosi maalumu cha kupambana na ujangili na matukio ya
dharura, kutoa mafunzo maalumu ya awali kwa askari 100 ambao wataingia katika
mafunzo ya awamu ya pili hivi karibuni.
Aliyataja baadhi ya mafanikio kuwa ni pamoja na kunasa
majangili 1,116 ndani ya hifadhi za taifa nchini, wakiwemo majangili 248 walioshikwa
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti pekee katika kipindi cha Aprili hadi Juni mwaka
huu, kukamata silaha za moto 85 na waya zinazotumika kutega wanyama 25,422,
mbao 3,275' mbao 1030 na mifugo 6,650.
No comments:
Post a Comment