23 September 2013

SHUJAA MWINGINE JWTZ KUAGWA LEO LUGALO



 Na Rachel Balama
   Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, leo anatarajiwa kuongoza waombolezaji kuaga mwili wa mwanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Private Hugo Munga, aliyefariki akiwa kwenye matibabu nchini Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa baada ya kujeruhiwa akiwa katika kikosi cha Umoja wa Mataifa cha Kulinda Amani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)
. Akizungumza kwa njia ya simu jana, Msemaji wa JWTZ, Meja Erick Komba, alisema mwili wa marehemu utaagwa leo kuanzia saa tatu asubuhi, Lugalo Jijini Dar es Salaam.Alisema mbali na Balozi Sefue pia shughuli hiyo itahudhuriwa na Jenerali Davis Mwamunyange, pamoja na makamanda wengine wa jeshi hilo.
 Alisema mwili wa marehemu uliwasili Jijini Dar es Salaam Septemba 20, mwaka huu ukitokea Afrika Kusini. Alisema baada ya kuagwa mwili wa marehemu utasafirishwa kwa ajili ya mazishi mkoani Kilimanjaro.
 Taarifa kutoka JWTZ ilieleza kuwa Private Munga,alifariki dunia Septemba, 18, mwaka huu akiwa hospitalini kwenye matibabu ya majeraha aliyopata kutokana na kujeruhiwa baada ya yeye na wenzake wanne kuangukiwa na bomu Agosti 28, mwaka huu.
 Katika tukio hilo mwanajeshi wa Tanzania Meja Khatibu Mshindo, alifariki.Meja Komba, alisema kuwa majeruhi wengine walionusurika katika tukio hilo wanaendelea vizuri.

No comments:

Post a Comment