05 September 2013

USALAMA BARABARANI:HUHITAJI JITIHADA ZA KILA MMOJA



 Mfano wa gari isiyosajiliwa.
MAPAMBANO dhidi ya ajali za barabarani ni suala endelevu. Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani ni miongoni mwa nchi zinazokabiliwa na janga hili la ajali za barabarani. Hadi kufikia Umoja wa Mataifa kuamua kutangaza miaka kumi ya mapambano dhidi ya ajali za barabarani (UN Decade of Action for Road Safety 2011-2020) hii pia inaonyesha dhahiri dunia inalitambua janga hili. Kwa sasa kila nchi duniani ina mipango yake ya kuhakikisha suala hili linapatiwa suluhisho la kudumu.

Tanzania kwa upande wake inaendeleza mapambano dhidi ya ajali za barabarani na mapambano haya yanaongozwa na taasisi mbili za serikali ambazo ni Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA).Kuanzia mwaka 2008 mamlaka hizi mbili zimekuwa zikiwakutanisha watendaji wao waliopo katika mikoa yote hapa nchini kwa lengo la kutathmini hatua zilizofikiwa na kuweka mikakati ya kukabiliana na ajali za barabarani.
Mnamo Juni 26 na 27 mwaka huu, watendaji wa jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani, hususani wakuu wa kikosi cha usalama barabarani wa mikoa yote ya Tanzania bara (RTOs), Maofisa toka makao makuu ya kikosi cha usalama barabarani na maofisa waandamizi wa SUMATRA Mikoa yote ya Tanzania bara pia baadhi ya wadau muhimu wa usafirishaji na usalama barabarani wakiwemo Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Ofisi ya Kamishna wa Bima nchini (TIRA) na waandishi wa habari.
Kama nilivyotangulia kueleza hapo awali, lengo la mkutano huo ni kufanya tathmini ya utendaji kazi wa wadau wa usafirishaji na usalama barabarani hususani katika kupunguza ajali za barabarani kwa kadri itakavyowezekana.Katika kufungua mkutano huo, Mgeni rasmi (Kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi) alipongeza desturi hiyo nzuri ya wadau wa usafirishaji na usalama barabarani kukutana na kujadili mambo muhimu. Zaidi ya hayo alipongeza jitihada zote zinazofanywa na taasisi hizo katika kupunguza ajali nchini.
Itakumbukwa kuwa katika Mkutano kama huo kilichofanyika mwaka jana (2012) washiriki waliazimia kupunguza ajali kwa asilimia tano (5). SUMATRA na Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kushirikiana na wadau mbalimbali tumefanikiwa kupunguza ajali kwa asilimia tatu (3). Pamoja na kwamba hatukufanikiwa kufikia malengo ya maazimio, jitihada hizo zinaridhisha japo ukweli ni kwamba nguvu ya ziada bado inahitajika kuhakikisha kuwa lengo la kuwa na Tanzania bila ajali linafikiwa.
Kwa namna ya pekee leo tutalenga zaidi katika mada iliyotolewa na Kaimu Meneja wa Kitengo cha Usajili wa Magari na Leseni za Udereva Ndugu Julius Mchihiyo kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambayo inahusu usajili wa vyombo vya moto Tanzania bara. Lengo la kujadili mada hii ni kuleta uelewa wa pamoja juu ya madhumuni ya usajili wa vyombo vya moto, sheria zinazosimamia usajili wa vyombo vya moto, utaratibu wa usajili wa vyombo vya moto, ushirikiano na wadau katika kusimamia vyombo vya moto, madhumuni ya ukaguzi wa vyombo vya moto na mwisho tutajadili changamoto mbalimbali zinazokabili usimamizi mzima wa vyombo vya moto katika kuboresha usafirishaji na usalama barabarani nchini.
JE UNAFAHAMU MADHUMUNI YA USAJILI WA VYOMBO VYA MOTO?
Kwa watu wengi, uelewa wao juu ya madhumuni ya usajili wa vyombo vya moto unaishia kwenye kukusanya mapato, ukweli ni kwamba, pamoja na hilo kuwa ni moja kati ya madhumuni ya usajili wa vyombo vya moto, bado kuna madhumuni mengine mengi ya usajili wa vyombo vya moto kama vile; kuonesha uhalali wa umiliki wa chombo husika, ndio maana kadi ya umiliki wa chombo husika hutolewa baada ya usajili.
Lakini pia usajili wa vyombo vya moto una dhumuni la kuonesha matumizi ya chombo kilichosajiliwa kwa maana kwamba kama chombo kimesajiliwa kwa matumizi binafsi ama kwa matumizi ya biashara. Zaidi ya hayo usajili wa vyombo vya moto unadhumuni la kuonesha aina ya chombo, kama ni gari na ni gari la aina gani, ama ni pikipiki, trela, trekta mtambo, nakadhalika.
Dhumuni jingine la usajili wa vyombo vya moto ni kurahisisha uchunguzi wa uhalifu endapo utafanywa kuhusisha chombo cha moto. Lakini pia usajili wa vyombo vya moto hurahisisha utoaji wa taarifa mbalimbali zinazohusu vyombo vya moto kwa taasisi nyingine. (Information/Statistical data), mfano ajali za kugonga na kukimbia (Hit & Run accidents).
Ndio maana Kifungu cha 8 (i) cha Sheria ya Usalama barabarani namba 30/1973 (CAP 168 RE.2002) inaeleza kuwa hairuhusiwi kwa mtu yeyote kuendesha chombo cha moto ambacho hakijasajiliwa. Kipengele (2) cha sura hiyo hiyo kinaeleza adhabu kwa mtu atakayekamatwa akitumia chombo cha moto ambacho hakijasajiliwa kuwa ni pamoja na faini isiyozidi elfu hamsini za kitanzania au kifungo kisichozidi miaka mitano.
Angalizo hapa ni kwamba, kumekuwa na taarifa za mitaani kuwa unaruhusiwa kutumia chombo cha moto kisichosajiliwa mpaka saa 12 jioni na siku za mwisho wa wiki na sikukuu. Taarifa hizo sio sahihi, sheria inasema kwamba hairuhusiwi kwa mtu yeyote kutumia chombo cha moto ambacho hakijasajiliwa.
SHERIA ZINAZOSIMAMIA USAJILI WA VYOMBO VYA MOTO
Hapa juu nimetaja sheria ya usalama barabarani, Sheria ya Usalama Barabarani namba 30/1973 (CAP 168 RE.2002). Lakini si sheria hiyo pekee inayosimamia usajili wa vyombo vya moto. Kuna sheria nyingine kama vile, Sheria ya Usajili na Ubadilishaji wa Umiliki wa gari ya mwaka 1972. (Motor Vehicles Tax on Registration and Transfer Act of 1972). Hivyo kununua chombo cha moto chenye usajili wa mtu mwingine na kukitumia bila kubadilisha umiliki ni kosa kisheria. Hata hivyo kosa hili linaonekana ni la kawaida sana kwa jamii hasa kutokana na ugumu wa maisha na watu wengi kushindwa kununua magari mapya na hivyo kulazimisha kununua magari mikononi mwa watu wengine yakiwa tayari yalisajiliwa kwa matumizi yao. Sheria inamtaka kila mmoja kubadili umiliki mara baada ya kununua.
Pia kuna kanuni mbalimbali za usalama barabarani zilizoundwa chini ya sheria ya usalama barabarani ya mwaka 1973 kama ilivyorekebishwa mwaka 2002. Moja wapo ikiwa ni Road Traffic Motor Vehicle Registration 2001). Sheria zote hizi zina lenga kuhakikisha kuwa kila mmoja anafuata taratibu sahihi za matumizi ya vyombo vya moto.
AINA ZA USAJILI WA VYOMBO VYA MOTO
Baada ya kuangalia sheria mbalimbali zinazosimamia usajili wa vyombo vya moto, sasa tunaangalia aina mbalimbali za usajili wa vyombo vya moto ambazo ni pamoja na;
• Usajili wa mara ya kwanza chombo kinapoingia nchini (Initial Registration). Huu ni usajili ambao wengi tunaujua na tumeuzoea.
• Usajili wa kubadilisha umiliki wa chombo ambacho tayari kilisajiliwa, mfano unaponunua chombo cha moto kwa mtu ambaye tayari alisajili. (Transfer of Owneship).
• Usajili wa kubadilisha baadhi ya taarifa za chombo (Alteration Registration). Mfano unapobadilisha rangi ya chombo husika au matumizi kutoka binafsi mpaka biashara na mabadiliko mengine.
• Usajili wa kufuta chombo kwenye mfumo wa usajili kwa sababu mbalimbali kwa ridhaa ya mmiliki (De-registration)
• Usajili wa chombo kinachosafirishwa kwenda nje ya nchi na mwisho ni
• Kufuta chombo kwenye mfumo wa usajili baada ya kuonekana kuwa hakikidhi sheria za usalama barabarani au kimesajiliwa bila kufuata taratibu zinazotakiwa
UTARATIBU WA USAJILI
• Kwa vyombo vya moto vinavyoingizwa hapa nchini kwa mara ya kwanza huwa vinatozwa ushuru wa forodha pamoja na kodi ya usajili pale vinapoingia bandarini au mipakani. Hata hivyo kwa vyombo vya moto vyenye umri wa zaidi ya miaka kumi (10) ushuru wa forodha wa ziada wa asilimia 20 hutozwa. Kwa vyombo vya moto vinavyotumika kwa usafirishaji wa umma, viwango vyao vya umri ni tofauti, hivyo kabla ya kuagiza chombo cha moto kwa ajili ya huduma ya usafirishaji wamiliki wanashauriwa kuwasiliana na Sumatraili kupata umri sahihi wa chombo kutoa huduma ya usafirishaji kwa umma, ili kuepusha usumbufu katika usajili wa chombo hicho.
• Utaratibu wa kubadilisha umiliki, mwenye chombo cha moto anatakiwa kwenda ofisi yoyote ya usajili akiwa na kadi halisi, mkataba wa mauziano pamoja na kodi zinazotakiwa.
• Utaratibu wa kubadilisha taarifa kwenye mtandao, mwenye chombo cha moto anatakiwa kuwasilisha ripoti ya polisi kuruhusu mabadiliko yafanyike, kadi halisi pamoja na ada husika.
• Kuomba nakala ya kadi iliyopotea au kuharibika (Duplicate) mwenye chombo cha moto anawajibika kuwasilisha kibali cha kutoa kadi kutoka polisi pamoja na ada husika
• Kuendeleza leseni iliyokwisha muda wake (Motor Vehicle Licence) mwenye chombo cha moto anatakiwa kuwasilisha nakala ya leseni iliyokwisha muda wake pamoja na ada husika.
TAARIFA MUHIMU ZA USAJILI
Wamiliki na madereva wengi wamekuwa wakipuuza kubeba kadi zao za usajili wa vyombo vya moto husika. Kila dereva anapaswa kubeba kadi yake aidha halisi au iliyothibitishwa na kutokubeba kadi kwenye chombo husika wakati kikitumika ni kosa kisheria. Taarifa muhimu ambazo zinapaswa kuonekana kwenye kadi ya usajili ambazo askari hukagua ni pamoja na;
• Jina kamili la mmiliki, anuani, mahali anapoishi, namba ya simu na barua pepe
• Aina ya chombo (Make)
• Model ya chombo
• Aina ya body
• Rangi ya chombo
• Muundo (Class) ya chombo (light, heavy)
• Mwaka wa utengenezaji (Year of Make)
• Namba ya Chasis
• Ujazo wa injini (Engine Capacity)
• Aina ya mafuta/nishati (Fuel used)
• Idadi ya Axles
• Urefu wa Axeles
• Idadi ya abiria
• Ujazo wa chombo kikiwa kitupu (Tare weight)
• Ujazo wa chombo kikiwa na mzigo (Gross weight)
• Nchi ilipotoka (Imported from)
• Matumizi (Private, Commercial)
Taarifa hizi zitakazoonekana kwenye kadi ya usajili zinapaswa kulingana na taarifa halisi za chombo husika, mabadiliko yoyote ya moja kati ya taarifa hizi bila utaratibu unaokubalika ni kosa kisheria
KUSHIRIKIANA NA WADAU
Kama ambavyo tumekuwa tukisisitiza kuwa suala la usalama barabarani linahitaji jitihada za kila mmoja wetu. Kwa hiyo ili kulinda usalama wa raia, vyombo vya moto, barabara, mazingira na mapato ya serikali, taasisi zote zilizopewa dhamana, wadau na wananchi wote kwa ujumla tunatakiwa kufanya kazi kwa kushirikiana. Kwa mfano ili kutekeleza majukumu yake, askari anahitaji taarifa ambazo ni sahihi. Hivyo lengo la kushirikana ni kubadilishana taarifa za vyombo hivyo na kuhakikisha kuwa wamiliki wa vyombo vya moto wanatekeleza taratibu na kanuni zilizowekwa kwa mujibu wa sheria. Hii itafanikiwa kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa vyombo vya moto.
MADHUMUNI YA UKAGUZI WA VYOMBO VYA MOTO
Madhumuni ya ukaguzi wa vyombo vya moto ni pamoja na;
• Kuviondoa barabarani vyombo vya moto ambavyo havikidhi viwango.
• Kuzuia uhalifu wa wizi wa vyombo vya moto.
• Kuzuia wamiliki wa vyombo vya moto kufanya marekebisho (Modifications) kiholela.
• Kuthibitisha kama chombo husika kimelipa kodi stahiki.
• Kuzuia ajali pamoja na msongamano barabarani kwa maana kwamba chombo cha moto kinapokuwa kibovu kinaweza kusababisha ajali au msongamano
• Kupunguza uchafuzi wa mazingira hasa kwa vyombo vya moto vinavyotoa moshi mwingi barabarani
• Kurahisisha uchunguzi wa chombo kilichopata ajali kwa ajili ya madai ya Bima. (Confirmation for accident compensation liability insurance).
CHANGAMOTO
Suala zima la usimamizi na ukaguzi wa vyombo vya moto, lina changamoto nyingi sana, baadhi ya changamoto ni kama zifuatazo:-
• Kuanzisha kwa mfumo wa kisasa wa ukaguzi wa magari ili kuondokana na huu uliozoeleka ambao una mapungufu mengi na hivyo kupunguza tija. Vyombo vingi vya kisasa vinaingia kila siku lakini ujuzi wa wakaguzi wetu umebaki palepale.
• Kuanzisha mawasiliano mazuri kati ya taasisi zote zinazosimamia masuala ya usafirishaji na usalama barabarani hapa nchini pamoja na wananchi wote kwa ujumla. Mawasiliano yaliyopo sasa sio ya kutosha.
• Kuongezeka kwa magari yanayoingizwa hapa nchini bila kuwepo ongezeko la miundo mbinu bora. Hali hii inahitaji kuwepo kwa mikakati maadhubuti ya kuboresha miundombinu na mipango miji.
• Utoaji wa elimu kwa umma kuhusu sheria na kanuni zinazohusu usafirishaji na usalama barabarani. Jitihada bado zinahitajika. Na changamoto ya mwisho ni kukosekana kwa mikutano ya mara kwa mara baina ya wadau na ikiwezekana kushirikisha jamii kwenye makongamano katika kukusanya maoni na mapendekezo yao juu ya uboreshaji wa usafirishaji na usalama barabarani

No comments:

Post a Comment