Na Florah Temba, Moshi
KIJIJI cha Chekereni Weruweru Wi l a y
a y a Mo s h i mk o a n i Kilimanjaro, kimetajwa kuongoza kwa wizi wa maji,
hali ambayo imekuwa ikiisababishia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira
Mjini Moshi (MUWSA) kupata hasara
.Hayo yalibainishwa jana na Ofisa
Uhusiano wa MUWSA, Dorah Kilo wakati wa operesheni ya kuwabaini wananchi
wanaojiunganishia maji kinyume cha sheria na taratibu, jambo ambalo limekuwa
likiisababishia mamlaka kupata hasara kubwa.
Kilo alisema kwa siku Mamlaka hiyo
huzalisha mita za ujazo 1,200 za maji katika kijiji hicho lakini asilimia 80 ya
maji hayo hupotea, kutokana na baadhi ya wananchi kujiunganishia maji kinyume
cha Sheria na taratibu.
"Kumekuwepo na upotevu mkubwa wa
maji katika kijiji hiki, kwani kwa siku tumekuwa tukizalisha maji mita za ujazo
1,200, lakini asilimia 80 ya maji hayo hupotea, na upotevu huu husababishwa na
watu kujiunganishia maji kinyume cha sheria," alisema.Alifafanua kuwa Mamlaka hiyo kwa sasa
hupoteza asilimia 28 ya maji yanayozalishwa ambapo asilimia 80 ya upotevu huo
inatoka katika kijiji cha Chekereni Weruweru.
Alisema katika operesheni waliyoifanya
kwenye Kijiji hicho changamoto kubwa waliyokutana nayo ni wananchi
kujiunganishia maji kinyume cha sheria, jambo ambalo limekuwa likisababisha
kuendelea kuwepo kwa upotevu mkubwa wa maji.
"Katika operesheni tuliyoifanya,
tumekutana na changamoto kubwa ya mkazi mmoja kujiunganishia maji isivyo halali
na amechimba kisima, lakini pia amepandisha maji kwenye tanki kwa kutumia mota
jambo ambalo ni kinyume cha sheria, kwa kweli hii ni hujuma kubwa kwa Mamlaka
na serikali kwa ujumla," alisema Kilo.Kutokana na hali hiyo mamlaka hiyo
ilimtaka msimamizi wa eneo hilo
kuhakikisha kiwango cha upotevu wa maji kinapungua ifikapo mwishoni mwa mwezi
Septemba mwaka huu.
Aidha Dorah alitumia pia nafasi hiyo
kuwaasa wakazi wa Kijiji cha Chekereni Weruweru, kuacha mara moja tabia ya
kujiunganishia maji kinyume cha sheria na kwamba kwa yeyote atakayebainika
atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kusitishiwa huduma ya
maji.
"Niwatahadharishe wananchi wa eneo
hili, waache haraka sana kujiunganishia maji kinyume cha sheria, kwani hatua ya
kwanza tutakayoichukua kwa mtu atakayebainika kufanya hivyo, ni kumkatia maji
kwa mujibu wa sheria na kumtaka alipe gharama ambazo zilipotea kutokana na wizi
wa maji aliokuwa akiufanya," alisema.
Akizungumza Mwenyekiti wa Kitongoji cha Katanini Kijiji cha
Chekereni Weruweru, Yahaya Salum aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa
mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira MUWSA, na kuhakikisha wanawafichua
wale wote ambao wamekuwa wakijiunganishia maji kinyume cha Sheria ili hatua
kali za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
No comments:
Post a Comment