24 September 2013

UGAIDI WA AL SHABAAB :MAPYA KENYA

Mwanajeshi wa Kenya akiwa makini huku akiwasogelea wanamgambo wa Al Shabaab nje ya jengo la Westgate.
  • WALIOKUFA WAFIKA 69,MAPAMBANO YAENDELEA
  • AL SHABAAB WAWILI WAUAWA,WATOA TAMKO ZITO


 NAIROBI, Kenya

  Wakati  hali ya taharuki ikiendelea kutanda kutokana na wanamgambo wa Al Shabaab wenye silaha kuliteka jengo la ghorofa nne lenye maduka la Westgate,jijini Nairobi, nchini Kenya, Septemba 21 mwaka huu, idadi ya watu waliokufa katika uvamizi huo imefikia 69 na majeruhi 175.


Tukio hilo la kusikitisha, limekwamisha ghughuli mbalimbali za maendeleo nchini humo ambapo idadi ya magaidi walio ndani ya jengo hilo ni kati ya 10-15.

Milio ya risasi jana imeendelea kusikika katika jengo hilo kutokana na mapambano makali kati ya vikosi vya Ulinzi na Usalama nchini na wanamgambo hao (magaidi) ambao wamewateka watu mbalimbali wasiofahamika idadi yao.Wapiganaji hao wa Al Shabaab, wamewateka raia ambao idadi yao haijulikani waliokuwa ndani ya jengo hilo kwa shughuli mbalimbali.

Ripoti zinasema kuwa, milio ya risasi ndani ya jengo hilo imesikika muda mrefu na milipuko dakika 15 mfululizo, hali ya mateka wanaoshikiliwa inaendelea kudorora.Rais wa Kenya, Bw. Uhuru Kenyatta, amesema vikosi vya Ulinzi na Usalama nchini humo vinajitahidi kuwaokoa mateka na kuhakikisha wanamgambo hao wanakamatwa.

Helikopta za polisi zimeonekana zikizunguka juu ya jengo hilo pamoja na ndege za kijeshi. Jeshi la nchi hiyo limekiri uwepo wa mazingira magumu ili kuwaokoa mateka waliosalia.

Baadhi ya mateka waliookolewa, wametibiwa hospitali na kuruhusiwa kutokana na majeraha ya risasi pamoja na guruneti ambalo Al Shabaab waliwarushia wakiwa ndani ya jengo hilo. Al Shabaab wamekiri kuhusika na ugaidi huo wakidai Kenya ilipeleka majeshi yake nchini Somalia ili kukabiliana nao.

Udhibiti jengo la Westgate

Jana jioni, Waziri wa Usalama nchini Kenya, Bw. Joseph Ole Lenku, alisema wanajeshi nchini humo wameweza kulidhibiti jengo lote la Westgate.Aliongeza kuwa, wanajeshi 10 wamejeruhiwa na wako hospitali wakiendelea na matibabu ambapo mateka karibu wote, tayari wameokolewa na kuua magaidi wawili.

Alisema moshi mzito umetoka juu ya jengo hilo kutokana na moto uliosababishwa na magaidi hao wakijaribu kukwamisha juhudi za wanajeshi wa Kenya ili wasiweze kukamatwa.Mkuu wa Majeshi nchini humo, Meja Jenerali Julius Karangi, alisema magaidi hao wanaweza kujisalimisha kama wanataka kwa sababu jeshi litakabiliana nao vilivyo.

Alisema nchi hiyo inakabiliana na magaidi wa kimataifa na wale waliomo katika jengo hilo wote ni wanaume na taarifa za awali zinasema walikuwa wakiongozwa na mwanamke.Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini humo, David Kimaiyo, alisema vikosi vya Ulinzi na Usalama vimeingia ndani ya jengo hilo ili kuwaokoa mateka waliobaki. Viongozi wa kidini nchini humo, walikusanyika mahali pamoja na kutoa tamko la kulaani ugaidi huo wa Al Shabaab.

Al Shabaab wazungumza

   Katika hatua nyingine, kundi la wanamgambo wa Al Shabaab lililopo Mogadisho, nchini Somalia, limesema mateka wote wanaoshikiliwa nchini Kenya, watauawa kama majeshi ya nchi hiyo yatatumia nguvu.

   Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwenye tovuti inayohusiana na kundi hilo, ilisema “Vikosi vya Israel na Kenya vimejaribu kuingia jengo la Westgate kwa lazima lakini vimeshindwa.“Wapiganaji wa Mujahideen watawaua mateka kama maadui watatumia nguvu,” alisema Shekhe Ali Mohamud Rage, ambaye ni msemaji wa Al Shabaab.

   Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Uingereza (Reuters), washauri wa Israel wanaisaidia Kenya kupanga mikakati ya kumaliza sakata hilo lililoanza Septemba 21 mwaka huu.

Serikali ya Tanzania

  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, imesema tukio hili limeathiri makundi na raia wa nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, Canada, Uingereza, Australia, China, Ghana, Korea na nyinginezo.

Imesema hadi sasa, baadhi ya wajeruhi wanaendelea na matibabu katika Hospitali za Aga Khan, Nairobi na Hospitali ya MP Shah.

   Kutokana na hali hiyo, Chama cha Msalaba Mwekundu nchini humo, kimetoa wito kwa raia wote wa Kenya kujitolea damu iweze kuwasaidia wote walioathirika na tukio hilo.Hadi sasa, Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini humo imepokea taarifa ya Mtanzania, Bw. Vedastus Nsanzungwanko ambaye ni Meneja, Child Protection, UNICEF aliyejeruhiwa kwa risasi katika miguu yake yote miwili.

   Bw. Nsanzugwanko amelazwa katika Hospitali ya Aga Khan akiendelea kupatiwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri.Katika hatua nyingine, Ofisi ya Ubalozi kwa kushirikiana na Uongozi wa Chama cha Watanzania nchini humo (TWA), unaandaa utaratibu maalumu ambao utaiwezesha jumuiya hiyo kuitikia wito wa kujitolea damu ili kuwasaidia wahanga wa tukio hilo. 

1 comment:

  1. Tanzania tusome kwa yanayotokea kwa wenzetu na tusiwe kimbelembele sana inshaakkah MUNGU ATUSAIDIE kudumisha amani yetu

    ReplyDelete