24 September 2013

BALOZI WA CHINA ‘AFUNGUKA’


Na Frank Monyo

   Balozi wa China nchini, Dkt. Lu Youqing, amesema hataacha kushiriki shughuli za maendeleo nchini kama atapewa mwaliko wa kushiriki na taasisi yoyote.Dkt. Youqing aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipoulizwa na waandishi wa habari juu ya msimamo wake kuhusu tuhuma zilizotolewa dhidi yake na CHADEMA akidaiwa kuiingilia masuala ya kisiasa nchini na kushiriki katika kazi za Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

   Bw.Youqing aliyasema hayo Dar es Salaam jana muda mfupi baada ya kushuhudia utiliaji saini kati ya Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) na Chama cha Wafanyabiashara Wachina (CBCT) kilichopo nchini ili kudumisha uhusiano wa nchi hizo.

    Makubaliano hayo yalisainiwa na Mkurugenzi wa TPSF, Bw. Godfrey Simbeye na Mwenyekiti wa CBCT, Bw. Huang Zaisheng, ambapo Balozi Youqing alisema, China ni mwekezaji mkubwa aliyeshikilia nafasi ya pili Tanzania kwa mujibu wa takwimu za Kituo cha Uwekezaji nchini.

    Alisema kuwa uwekezaji wa moja kwa moja umefikia dola za Marekani bilioni 2.17 hadi Juni mwaka huu ambapo kutokana na uwekezaji huo, umeongeza ajira 150,000 na biashara kati ya China na Tanzania, imefikia dola za Marekani bilioni 2.5.

    Aliongeza kuwa, zaidi ya Watanzania 350.000 wanajihusisha na biashara inayotokana na uwekezaji wa Kampuni za China.“Hadi sasa ajira mpya zitokanazo na uwekezaji wa China, zimefikia 500.000 hivyo kufanya nchi yetu iongoze kwa kutengeneza ajira nyingi Tanzania,” alisema.

    Mwenyekiti wa TPSF, Dkt. Reginald Mengi, alisema baada ya kukutana na Dkt. Youqing, walikubaliana na wafanyabiashara wa China kushirikiana kwa kujiunga na taasisi hiyo ili kutatua matatizo ambayo wanakumbana nayo.

No comments:

Post a Comment