Mwanajeshi wa Kenya akiwa makini huku akiwasogelea wanamgambo wa Al Shabaab nje ya jengo la Westgate.
- WALIOKUFA WAFIKA 69,MAPAMBANO YAENDELEA
- AL SHABAAB WAWILI WAUAWA,WATOA TAMKO ZITO
NAIROBI, Kenya
Wakati hali ya taharuki ikiendelea kutanda
kutokana na wanamgambo wa Al Shabaab wenye silaha kuliteka jengo la ghorofa nne
lenye maduka la Westgate,jijini Nairobi, nchini Kenya, Septemba 21 mwaka huu,
idadi ya watu waliokufa katika uvamizi huo imefikia 69 na majeruhi 175.
Tukio hilo la kusikitisha, limekwamisha ghughuli mbalimbali za
maendeleo nchini humo ambapo idadi ya magaidi walio ndani ya jengo hilo ni kati ya 10-15.
Milio ya risasi
jana imeendelea kusikika katika jengo hilo kutokana na mapambano makali kati ya
vikosi vya Ulinzi na Usalama nchini na wanamgambo hao (magaidi) ambao
wamewateka watu mbalimbali wasiofahamika idadi yao.Wapiganaji hao
wa Al Shabaab, wamewateka raia ambao idadi yao haijulikani waliokuwa ndani ya
jengo hilo kwa shughuli mbalimbali.
Ripoti zinasema
kuwa, milio ya risasi ndani ya jengo hilo imesikika muda mrefu na milipuko
dakika 15 mfululizo, hali ya mateka wanaoshikiliwa inaendelea kudorora.Rais wa Kenya,
Bw. Uhuru Kenyatta, amesema vikosi vya Ulinzi na Usalama nchini humo vinajitahidi
kuwaokoa mateka na kuhakikisha wanamgambo hao wanakamatwa.
Helikopta za
polisi zimeonekana zikizunguka juu ya jengo hilo pamoja na ndege za kijeshi.
Jeshi la nchi hiyo limekiri uwepo wa mazingira magumu ili kuwaokoa mateka
waliosalia.
Baadhi ya mateka
waliookolewa, wametibiwa hospitali na kuruhusiwa kutokana na majeraha ya risasi
pamoja na guruneti ambalo Al Shabaab waliwarushia wakiwa ndani ya jengo hilo. Al Shabaab
wamekiri kuhusika na ugaidi huo wakidai Kenya ilipeleka majeshi yake nchini
Somalia ili kukabiliana nao.
Udhibiti jengo
la Westgate
Jana jioni,
Waziri wa Usalama nchini Kenya, Bw. Joseph Ole Lenku, alisema wanajeshi nchini
humo wameweza kulidhibiti jengo lote la Westgate.Aliongeza kuwa,
wanajeshi 10 wamejeruhiwa na wako hospitali wakiendelea na matibabu ambapo
mateka karibu wote, tayari wameokolewa na kuua magaidi wawili.
Alisema moshi mzito umetoka juu ya
jengo hilo kutokana na moto uliosababishwa na magaidi hao wakijaribu kukwamisha
juhudi za wanajeshi wa Kenya ili wasiweze kukamatwa.Mkuu wa Majeshi nchini humo, Meja
Jenerali Julius Karangi, alisema magaidi hao wanaweza kujisalimisha kama
wanataka kwa sababu jeshi litakabiliana nao vilivyo.
Alisema nchi hiyo inakabiliana na
magaidi wa kimataifa na wale waliomo katika jengo hilo wote ni wanaume na
taarifa za awali zinasema walikuwa wakiongozwa na mwanamke.Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini humo,
David Kimaiyo, alisema vikosi vya Ulinzi na Usalama vimeingia ndani ya jengo
hilo ili kuwaokoa mateka waliobaki. Viongozi wa kidini nchini humo,
walikusanyika mahali pamoja na kutoa tamko la kulaani ugaidi huo wa Al Shabaab.
Al Shabaab wazungumza
Katika hatua nyingine, kundi la
wanamgambo wa Al Shabaab lililopo Mogadisho, nchini Somalia, limesema mateka
wote wanaoshikiliwa nchini Kenya, watauawa kama majeshi ya nchi hiyo yatatumia
nguvu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwenye
tovuti inayohusiana na kundi hilo, ilisema “Vikosi vya Israel na Kenya
vimejaribu kuingia jengo la Westgate kwa lazima lakini vimeshindwa.“Wapiganaji wa Mujahideen watawaua
mateka kama maadui watatumia nguvu,” alisema Shekhe Ali Mohamud Rage, ambaye ni
msemaji wa Al Shabaab.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la
Uingereza (Reuters), washauri wa Israel wanaisaidia Kenya kupanga mikakati ya
kumaliza sakata hilo lililoanza Septemba 21 mwaka huu.
Serikali ya Tanzania
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, imesema tukio hili limeathiri makundi na raia wa nchi mbalimbali
ikiwemo Tanzania, Canada, Uingereza, Australia, China, Ghana, Korea na
nyinginezo.
Imesema hadi sasa, baadhi ya wajeruhi
wanaendelea na matibabu katika Hospitali za Aga Khan, Nairobi na Hospitali ya
MP Shah.
Kutokana na hali hiyo, Chama cha
Msalaba Mwekundu nchini humo, kimetoa wito kwa raia wote wa Kenya kujitolea
damu iweze kuwasaidia wote walioathirika na tukio hilo.Hadi sasa, Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania
nchini humo imepokea taarifa ya Mtanzania, Bw. Vedastus Nsanzungwanko ambaye ni
Meneja, Child Protection, UNICEF aliyejeruhiwa kwa risasi katika miguu yake
yote miwili.
Bw. Nsanzugwanko amelazwa katika
Hospitali ya Aga Khan akiendelea kupatiwa matibabu na hali yake inaendelea
vizuri.Katika hatua nyingine, Ofisi ya Ubalozi kwa kushirikiana na
Uongozi wa Chama cha Watanzania nchini humo (TWA), unaandaa utaratibu maalumu ambao
utaiwezesha jumuiya hiyo kuitikia wito wa kujitolea damu ili kuwasaidia wahanga
wa tukio hilo.
Tanzania tusome kwa yanayotokea kwa wenzetu na tusiwe kimbelembele sana inshaakkah MUNGU ATUSAIDIE kudumisha amani yetu
ReplyDelete