03 September 2013

UELEWA MDOGO CHANZO CHA MIGOGORO YA MIRATHI



 Gaston Katindila


Jibu la hoja hii kimsingi ni rahisi, kwani kisheria mtu yoyote anaweza kuteuliwa kuwa msimamizi wa mali za marehemu, kama nilivyosema awali ilimradi apitishwe na wanandugu katika kikao cha ukoo na familia.


TUNAFAHAMU kuwa zipo taratibu mbalimbali za kisheria zinazotoa mwongozo wa mambo fulani. Katika suala la mirathi za marehemu zipo taratibu na mwongozo juu ya namna ya uteuzi wa wasimamizi au msimamizi mkuu wa mali za marehemu
.Marehemu anapoacha mali, madai pamoja na haki zake mbalimbali familia ina haki ya kufuatilia na kupata haki zote stahiki za marehemu. Lakini hili limekuwa tatizo kwa watu wengi kwa kushindwa kufuata taratibu za kisheria.
Familia nyingi zinapotokewa na tatizo la kufiwa na ndugu au jamaa hushindwa kufuata taratibu za kisheria zitakazowawezesha kupata haki mbalimbali ambazo ni stahiki kwa warithi wa mali za marehemu.
Kuna taratibu zinazotakiwa kufanywa na ndugu wa marehemu ili kuweza kupata uhalali wa umiliki au usimamiaji wa mali zilizoachwa na marehemu.
Mara baada ya taratibu za mazishi kukamilika ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu wanatakiwa kufanya kikao kitakachokuwa na ajenda mbalimbali ikiwemo kujadili juu ya mali za marehemu.Pamoja na kujadili mali na mambo mengine ya kifamilia yanayomhusisha marehemu lakini pia kikao hicho kinatakiwa kumteua msimamizi wa mirathi ambaye kama ilivyozoeleka ndiye atakuwa msimamizi mkuu wa mali zote za marehemu kwa niaba ya wale warithi wanaokubalika kisheria.
Kikao pia kinaweza kumchagua msimamizi wa mirathi zaidi ya mmoja ilimradi tu waridhiwe na mkutano huo wa ndugu. Kuna jambo moja linaloshindwa kueleweka vizuri kwa watu wengi nalo ni juu ya nani anapaswa kuteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi?Jibu la hoja hii kimsingi ni rahisi, kwani kisheria mtu yoyote anaweza kuteuliwa kuwa msimamizi wa mali za marehemu, kama nilivyosema awali ilimradi apitishwe na wanandugu katika kikao cha ukoo na familia.
Lakini ni vyema kwa mtu makini na wakaribu katika familia kuchaguliwa kuwa ndiye msimamizi wa mirathi za marehemu.Na hapa mara nyingi familia huchagua mtu mzima na mwenye busara ambaye wanaamini ataweza kusimamia vyema mirathi hiyo.
Mahakamani kumekuwepo na pingamizi nyingi juu ya wasimamizi mbalimbali wa mirathi, moja ya hoja ambazo zimekuwa zikiibuliwa ni juu ya uhusiano baina ya marehemu na msimamizi wa mirathi, lakini si sababu hiyo pekee zipo sababu nyingine zinazotolewa na wanandugu katika kupinga usimamizi wa mirathi.
Mara baada ya uteuzi huo, ni vizuri kwa msimamizi wa mirathi kupata barua ya mwenyekiti au mtendaji wa mtaa kwa ajili ya kuthibitisha uteuzi wake huo.
Msimamizi wa mirathi anaweza kwenda kufungua shauri la mirathi katika mahakama yoyote yenye uwezo wa kusikiliza shauri hilo. Msimamizi anatakiwa kupeleka muhtasari wa kikao cha wanandugu kilichothibitisha uteuzi wake, cheti cha kifo pamoja na barua kutoka kwa kiongozi wa mtaa ikithibitisha pia juu ya uteuzi wake huo.
Shauri linapofika mbele ya mahakama, uamuzi wowote unaweza kutolewa juu ya msimamizi aliyependekezwa kuwa msimamizi wa mali za marehemu.Kabla ya kusikiliza shauri mahakama huzingatia pingamizi kutoka kwa wanandugu kama kuna uwepo wa pingamizi lolote.
Lakini pia mara baada ya kuchambua ushahidi mahakama huweza kuridhia uteuzi wa msimamiaji huyo wa mirathi au inaweza isiridhie juu ya mtu huyo aliyeteuliwa na wana kusimamia mali za marehemu.Katika mjadala wangu nitaeleza zaidi pale inapotokea msimamizi huyo anapopitishwa na mahakama kuwa msimamizi wa mirathi ya mali za marehemu.
Kumekuwepo na migogoro mingi ya wanafamilia na wasimamiaji wa mali za marehemu katika usimamiaji na ugawaji wa mali za marehemu kitu kinachopelekea migongano kwa wanandugu.Wasimamizi wengi wa mirathi hujigeuza kuwa wamiliki wa mali za marehemu na kuwatendea yasiyo mema warithi halali wa mali hizo za marehemu.
Niseme tu kisheria msimamizi wa mirathi hana umiliki wa mali za marehemu, wala hana chochote katika fungu la mali za marehemu. Kazi yake ni kusimamia tu mgawanyo na mali zote za marehemu.Dhana ya msimamizi wa mirathi kuwa ndiye mmiliki wa mali hizo zilizoachwa na marehemu imekuwa ikidhaniwa na wasimamizi wengi wa mirathi hivyo kusababisha migongano baina ya wanandugu.
Hii hutokana na wasimamizi kuwanyima warithi halali haki zao muhimu na za msingi juu ya taarifa mbalimbali za mwenendo wa mali zinazosimamiwa na msimamiaji huyo mkuu wa mirathi.Hili pia hupelekea wanafamilia wengi kufika mahakamani na kutaka kumbadilisha msimamizi huyo ambaye wanaona kwa namna fulani anageuza maana ya familia na mahakama kumteua kama msimamizi na si mmiliki.
Msimamizi wa mirathi huweza kubadilishwa pale kunapokuwa na haja ya kufanya hivyo, wanandugu na familia huweza kueleza sababu mbalimbali za kutengua na kufuta usimamizi huo mbele ya mahakama.Niseme kwa kuzingatia hoja zilizowasilishwa mahakama yaweza kutengua msimamizi yoyote wa mirathi ambaye kwa namna fulani hakubaliki na wanafamilia kwa sababu kama nilizoeleza hapo awali.
I e l ewe k e k uwa wa k a t i wa s imami z i wa mi r a t h i w a n a p o c h a g u l i w a n a kupendekezwa na wanafamilia wasiwe na dhana ya kwamba wao ndiyo wanaokwenda kuwa wamiliki mbadala wa mali zote za marehemu na badala yake wajue kwamba msimamizi wa mirathi ana jukumu moja tu la kusimamia mali zote za marehemu, na si kuwa na miliki dhidi ya warithi wa mali hizo.
Warithi wa mali za marehemu wataendelea kuwa na haki zote juu ya mali zilizoachwa hata kama kati ya warithi hao hakuna aliyechaguliwa kuwa msimamizi wa mirath hiyo ya mali za marehemu.
Mwandishi wa makala haya ni mwanahabari na mwanafunzi wa Stashahada ya Sheria katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama- Lushoto
0716230044
katindilagaston@gmail.com

No comments:

Post a Comment