28 January 2013

Kamati Kuu Chadema kukutana leoNa Stella Aron

KAMATIi Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinatarajia kufanya mkutano maalum wa siku mbili kwa ajili ya kujadili ajenda mbalimbali ikiwemo taarifa ya fedha kwa mwaka 2012.

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi CHADEMA, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika, alisema mkutano utafanyika leo na kesho Jijini Dar es Salaam.

Alisema mkutano huo utajadili ajenda mbalimbali ikiwemo taarifa ya fedha kwa mwaka 2012, mpango kazi na bajeti kwa mwaka 2013, ratiba ya uchaguzi mkuu wa chama na operesheni ya M4C.

"Pia mkutano huo utajadili maudhui na mchakato wa katiba mpya,taarifa ya katibu wa wabunge wa Chadema, maandalizi ya ajenda za baraza kuu la chama na mara ya mwisho, kamati kuu katika mkutano wake wa kawaida kwa siku mbili ulifanya maamuzi mbalimbali, " alisema.

Mnyika alisema kuwa kati ya ajenda ambazo ziliazimiwa ni kwamba Rais Jakaya Kikwete akumbushwe kujibu barua kuhusu haja ya kuundwa kwa tume tume ya kimahakama/kijaji kuchunguza mauaji ya raia kama alivyoahidi na mwendelezo wa Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) utumike kuishinikiza Serikali iwapo hatua stahiki zitakuwa hazijachukuliwa; kwa kuzingatia kwamba 2013 ni mwaka wa 'nguvu ya umma'.

Alisema kuwa pia kamati kuu iliazimia kwamba uongozi wa Chadema katika maeneo ambazo chaguzi za marudio za udiwani, mitaa, vijiji na vitongoji zinacheleweshwa kwa makusudi uunganishe umma kufanya shinikizo la kisiasa kwa mamlaka zinazohusika kutangaza nafasi kuwa wazi na vyombo vinavyosimamia chaguzi katika ngazi hizo ili haki za kikatiba na kisheria za wananchi kupata uwakilishi ziweze kupatikana kwa wakati.

Mnyika alisema kuwa mapendekezi mengine ni kamati Kuu iliazimia kwamba Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na Chadema ichukue hatua za kibunge kuhakikisha kwamba daftari la wapiga kura linaboreshwa mwaka 2013 ikizingatiwa kuwa daftari hilo hilo litatumika kwenye kura za maoni za katiba mpya.

No comments:

Post a Comment