21 August 2012
Waislamu dumisheni amani-Dkt.Bilal *Dkt.Shein awataka washiriki sensa
Na Waandishi Wetu, Dar na mikoani
WITO umetolewa kwa Watanzania kuendelea kudumisha amani iliyopo nchini ili kuepuka machafuko yanayoweza kuifanya Serikali ishindwe kutekeleza mikakati mbalimbali ya maendeleo.
Makamu wa Rais Dkt.Mohamed Gharib Bilal, aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika ibada ya sikukuu ya Idi el fitri ambayo kimkoa ilifanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja.
Alisema Waislamu wanaposherehekea siku hiyo, hawana budi kukumbuka mafundisho ya Mtume Muhamad (SAW), kuwaombea marehemu na kuwakumbuka wagonjwa, yatima na wasio na uwezo.
"Wazazi hakikisheni watoto wenu wapo katika maeneo yenye maadili mema ili waweze kusherehekea siku hii, pia muone umuhimu wa kutembelea ndugu na kuwafariji," alisema Dkt.Bilal.
Kwa upande wake, Shekhe Mkuu wa Mkoa huo, Alhad Musa Salum, aliwataka Waislamu kujitokeza kwa wingi ili kutoa maoni yao kwa Tume inayoratibu maoni ya Katiba Mpya.
"Tujitokeze kwa wingi na kutoa maoni yenye masilahi kwa Uislamu na Taifa ili kuleta heshima ya dini yetu, pia tushirikiane na Serikali kuhakikisha tunashiriki Sensa ya Watu na Makazi iliyopangwa kuanza usiku wa kuamkia Agosti 26, mwaka huu," alisema.
Alisema sensa ina umuhimu mkubwa kwa Taifa ili kuiwezesha Serikali kupanga mikakati yake ya maendeleo na kuwataka waumini wa dini hiyo, kuwapuuza baadhi ya watu wanaotaka kukwamisha mpango huo kwa masilahi yao binafsi.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na waumini mbalimbali na viongozi akiwemo Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Waziri wa Afya, Dkt. Hussen Mwinyi na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba.
Dkt. Shein ashiriki ibada Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Ali Mohamed Shein, amewataka wananchi kutowapa nafasi watu ambao hawaitakii mema Zanzibar na kuona umuhimu wa kushiriki Sensa ya Watu na Makazi ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Dkt.Shein aliyasema hayo Zanzibar jana, katika hotuba aliyoisoma kwenye Baraza la Idi el fitri na kuongeza kuwa, inasikitisha kuona baadhi ya watu wanawashawishi wenzao wasikubali kuhesabiwa na kutoa visingizio visivyo na msingi.
"Mafundisho ya dini zote hayapingi suala la kuhesabiwa ili kupanga mikakati ya maendeleo kwa wananchi, hivi karibuni Zanzibar ilikabiliwa na viashirio vya kuvunjika amani na utulivu ambao kama utapotea, kuirudisha kwake itachukua muda mrefu," alisema.
Dkt.Shein alisisitiza kuwa, watu wanaoshabikia vitendo vya uvunjaji sheria, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa, itaendelea kuchukua hatua za kisheria kwa wahusika wote.
Wakati huo huo, wito umetolewa kwa Waislamu nchini kote kuwa waadilifu na kuzingatia mafundisho ya dini hiyo ili kudumisha amani na usalama kati ya Tanzania na majirani zao.
Ushauri huo umetolewa jana katika swala la Idi el Fitri ambayo kitaifa ilifanyika mjini Songea, mkoani Ruvuma.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na waumini mbalimbali wa dini hiyo akiwemo Shekhe Mkuu, Mufti Issa bin Shaaban Simba na Mkuu wa Mkoa huo, Bw.Said Mwambungu, ambaye alimwakilisha Rais Jakaya Kikwete.
Akizungumza na waumini katika ibada hiyo, Imam wa Msikiti huo, Shekhe Shaaban Mbaya, alisema waumini wa Kiislamu hawatakiwi kubaguana katika maisha ya kila siku.
"Mafundisho ya dini yetu yanasisitiza upendo na amani ili kumuenzi Mwenyezi Mungu ambaye ni mwingi wa rehema, viumbe vyote vya ardhini, majini na hewani ameviumba yeye bila ubaguzi," alisema.
Aliongeza kuwa, Mtume Muhammad (SAW), aliweza kuwatunza mayatima na watu wasio na uwezo kiuchumi ili wapate furaha ya maisha licha ya shida na upweke walionao.
"Haina maana katika sikukuu hii mkajipamba kwa nguo safi pamoja na kula vyakula vizuri wakati mioyo yenu na matendo yenu hayampendezi Mwenyezi Mungu,"alisema Shekhe Mbaya na kuongeza kuwa ni vyema wakazingatia mafundisho waliyopata katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Alisema uchoyo na tamaa za mali, matendo mabaya, uroho wa madaraka na kudhalilisha wengine ndiyo chanzo cha kuvuruga amani iliyopo kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa.
BAKWATA Singida
Katibu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), mkoani Singida, Alhaj Salimu Ngaa, amewataka Waislamu kushiriki Sensa ya Watu na Makazi ili kufanikisha dhamira ya Serikali.
Alhaj Ngaa aliyasema hayo jana katika ibada ya Idi el Fitri ambayo ilifanyika katika Uwanja wa Namfua mjini hapa.
"Waislamu tuna wajibu wa kushiriki sensa ili Serikali iweze kupata takwimu sahihi ambazo zitatumika kupanga mikakati ya maendeleo na kuhudumia wananchi wake," alisema.
Alisema lazima kila Mtanzania atoe shukrani kwa Serikali ambayo imekuwa ikiwasaidia kutekeleza mambo mbalimbali yaliyofanikisha wapige hatua na kuiomba Serikali iwachukulie hatua watu wanaotaka kukwamisha mpango huo.
Katika hatua nyingine, waumini wa Kiislamu mkoani Geita, wametakiwa kumcha Mwenyezi Mungu pamoja na kuwalea watoto wao katika maadili mema ili wawe viongozi waadilifu nchini.
Shekhe wa Msikiti wa Mseto, Mohamed Abdul, aliyasema hayo jana katika ibada ya Idi el Fitri iliyofanyika kwenye Uwanja wa Bomani, wilayani Geita.
Alisema kama Waislamu na Watanzania watakuwa mstari wa mbele kuwalea watoto wao katika maadili mema, nchi itakuwa na viongozi makini ambao watasaidia kuleta maendeleo ya kweli.
Aliongeza kuwa, kumalizika kwa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni suala la kumshukuru Mungu kwa yote aliyowatendea ambapo katika ibada hiyo, waumini walichanga sh. milioni 2.3 kwa ajili ya ujenzi wa msikiti katika kiwanja hicho na madarasa ambayo yatatumika kutoa mafunzo ya dini hiyo.
Ujenzi huo unatarajiwa kugharimu sh. milioni 30 ambapo baadhi ya waumini walitoa ahadi za kufanikisha ujenzi huo.
Imeandaliwa na Darlin Said, Cresensia Kapinga, Damiano Mkumbo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment