Na Suleiman Abeid
MWAKA 1992, ni mwaka muhimu kwa
Watanzania kufuatia mabadiliko makubwa ya mfumo wa siasa yaliyofanyika ambapo
taifa letu lilitoka katika mfumo wa utawala wa chama kimoja na kuanza kutumika
kwa mfumo wa vyama vingi.
Pamoja na
kukubalika kwa mfumo huo nchini kulitokana na busara za uongozi uliokuwepo
madarakani wakati huo kuchukua maamuzi mazito ambayo wananchi wengi
hawakuyategemea.Maamuzi hayo ni
kitendo cha Taifa kukubali kuingia katika mfumo wa vyama vingi wakati wananchi
wake waliukataa mfumo huo kupitia Tume maalumu iliyokuwa imeundwa kukusanya
maoni ili kuweza kubaini iwapo nchi iingie katika mfumo huo au ibaki katika
mfumo wa chama kimoja.
Kwa mujibu wa
matokeo yaliyotangazwa na tume iliyokuwa ikikusanya maoni hayo, asilimia 80 ya
Watanzania waligoma Tanzania kuingia katika mfumo wa vyama vingi, huku hoja ya
msingi ya kuukataa mfumo huo ikiwa ni kuchelea kutokea mapigano ya wenyewe kwa
wenyewe.Busara za Baba
wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere zilisaidia aliposhauri kwamba, pamoja
na Watanzania wengi kuukataa mfumo huo ilikuwa vyema mawazo ya Watanzania
asilimia 20 waliokuwa wamekubali kuanzishwa kwa mfumo huo yakaheshimiwa na
kuchukuliwa.
Kutokana na
ushauri huo, hatimaye mwaka 1992, ilikubali kubadili katiba yake na kikubwa
katika mabadiliko hayo ilikuwa ni kubadilisha kifungu cha katiba kilichokuwa
kikieleza kwamba, Tanzania itakuwa nchi ya chama kimoja na badala yake ikawa,
"Tanzania itakuwa ni nchi ya mfumo wa vyama vingi".
Mfumo wa vyama
vingi ni hali ya kuwa na chama zaidi ya kimoja, katika nchi moja kwa lengo la
kuleta ushindani wa kisiasa, ili kuleta maendeleo ya nchi.
Upinzani wa
kisiasa si uadui kama asilimia 80 ya Watanzania waliokuwa wameukataa mfumo huo
walivyokuwa wakiamini.Ukweli ni
kwamba nchi yoyote ulimwenguni yenye demokrasia ya kweli inatumia mfumo wa
vyama vingi vya siasa kwa lengo la kuongeza wigo wa demokrasia kwa wananchi
wake ambapo chini ya mfumo wa chama kimoja sehemu kubwa ya wasio wanachama wa
chama tawala hawakuwa na eneo la kuchangia mawazo yao katika kuongoza nchi.
Kuanzishwa kwa
mfumo huo, kulifungua milango ya kuanzishwa kwa vyama vipya vya siasa mbali ya
kile kilichokuwepo Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo vyama vya awali
vilivyoanzishwa ni pamoja na Chama cha Wananchi (CUF).Vingine
vilikuwa, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Demokrasia Makini,
Democratic Party (DP), National Convention for Constitution and
Reconstruction-Mageuzi (NCCR-Mageuzi), United Democratic Party (UDP), UMD na
vingine.
Mpaka kufikia
mwishoni mwa mwaka 2011, zaidi ya vyama vya siasa 18 vilikuwa vimeanzishwa
nchini, vyote vikiwa na lengo kuu moja la kupanua demokrasia katika suala zima
la utawala wa nchi na pia kuweza kupata ridhaa ya kuongoza nchi ambapo kwa
kawaida ni chama kimoja tu ndicho hupata ridhaa hiyo.
Chama ambacho
hakikufanikiwa kupata ridhaa ya kukamata dola na kuunda serikali, lakini
kikapata idadi kubwa ya wabunge wanaoingia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, kinapokuwa ndani ya bunge hupewa heshima ya kuongoza kambi ya
upinzani kwa maana nyingine hujulikana kama chama kikuu cha upinzani.
Upinzani hapa
maana yake si kuwa na chama kinachoongoza mapambano yanayolenga kuifanya nchi
isitawalike la hasha, maana halisi ni kule kukosoa muswada ama sheria yoyote
ile inayopelekwa bungeni ikiwa haina masilahi kwa wananchi.
Kutokana na
hali hiyo kambi ya upinzani hupinga mswada au sheria hiyo kwa maslahi ya
watanzania ambapo pia hupaswa kutoa ushauri wa njia mbadala itumike kwa lengo
la kuleta maslahi bora zaidi kwa wananchi.
Ipo mifano
mingi juu ya hili mmojawapo ni wa mabadiliko ya sheria ya ukusanyaji maoni
Katiba Mpya.
Kwa wanaoamini
kwamba, uwepo wa vyama vingi nchini ni kwa ajili ya kuleta machafuko, ni wazi
wamefilisika kifikra, wanapaswa kufuta mawazo hayo na kurejea katika mistari
kwa kuviona vyama vya upinzani vipo kwa ajili ya kukionesha njia ama kukikosoa
chama tawala kilichoko madarakani pale kinapokwenda kinyume na malengo ya nchi.
Iwa p o c h ama
k i l i c h o p o madarakani kitakaa tu katika kiti chake cha enzi na kukosa
mtu wa kukikosoa; ni wazi kwamba utawala wake utakuwa ni wa ki-imla na wananchi
wanaoongozwa na chama hicho watakuwa wako kifungoni daima kutokana na chama
kujisahau kwamba kilichaguliwa ili kiwatumikie wao.
Kutokana na hali hiyo kila Mtanzania
ana wajibu sasa wa kuviona vyama vyote vya siasa hapa nchini vina haki sawa na
tofauti yao ni kwamba, kimoja kati yao ndicho kinachokuwa kimepewa ridhaa ya
kuongoza nchi baada ya kunadi sera na ilani yake kwa wapigakura na pale
waliporidhika wakakipatia ridhaa hiyo ya kukamata dola na kuunda serikali.
Daima tunapaswa kuelewa kuwa vyama vya
siasa ambavyo havikupata ridhaa ya kukamata dola na kuunda serikali si adui au
vina lengo la kutaka kuleta machafuko nchini la hasha bali ni kwamba ili
demokrasia ya vyama vingi vya siasa iweze kuwa na maana ni muhimu nchi ikawa
katika hali ya amani na utulivu wakati wote.
Ili hali ya amani na utulivu iweze
kupatikana daima suala la kuvumiliana kati ya wafuasi wa vyama ni lazima lipewe
kipaumbele, hasa kwa vyama vile vilivyofanikiwa kupata wabunge wanaoingia
bungeni kwa kujenga utamaduni wa kukosoana bila ya kupigana au kuzomeana.
Katika hili chama tawala ndicho
kinachopaswa kuwa mfano kwa kuelewa ipo siku moja kitajikuta kimekaa katika
viti vya upande wa upinzani na kilichokuwa chama cha upinzani ndicho kimekuwa
chama tawala, hivyo kisipoonesha mfano mzuri; ipo hatari ya kulipizana visasi
ambavyo vinaweza kuwa chanzo cha kupotea kwa hali ya amani na utulivu nchini.
Ha t a h i v y o , p amo j a n a
matatizo yaliyowahi kujitokeza nchini na kuhusisha vyama vya upinzania ikiwa
sasa imetimia miaka 21 tangu kuanzishwa kwa mfumo huu, Watanzania wengi
wameanza kuielewa vyema dhana ya demokrasia ya vyama vingi ikilinganishwa na
pale mwanzo.
Uelewa wa Watanzania utasaidia sana
kuifanya nchi kuendelea kuwa ya amani na utulivu na hata kasi ya kuongezeka kwa
uchumi itakuwepo iwapo chama tawala kitasimamia katika kuongoza kwa haki na
kuwatumikia wananchi waliokiweka madarakani badala ya kujali masilahi binafsi,
maana haki ndiyo msingi mwingine wa amani.
Mara kwa mara CCM imekuwa ikikiri
maneno ya hayati wa Baba wa Taifa, aliyowahi kusema enzi ya uhai wake kwamba,
“pasipokuwa na haki hapawezi kuwa na amani,” Kauli hii ni sahihi maana Tanzania
kwa kiasi kikubwa imefanikiwa kuwa nchi yenye amani na utulivu kutokana na sera
zake zinazoweka mbele uhuru, haki, usawa na utu.
Msingi huu uhakikishe hauvunjiki daima
hata kama CCM itaondoka madarakani na kuwepo kwa chama kingine cha siasa, ili
amani iweze kuendelea kudumu hapa nchini ni muhimu kuheshimiana na kuvumiliana.
Kuvumiliana katika suala la siasa ni
kitu muhimu, Tanzania ni yetu sote, hivyo si vyema kwa wanachama wa CCM kujiona
bora kuliko wale wa vyama vingine, au wale wa vyama vingine kujiona wao ndiyo
wanaojua zaidi ya wale wa CCM na kila jambo kinachofanya ni baya.
Utamaduni wa kudharauliana ukipewa
nafasi ni wazi tutafika sehemu nchi haitatawalika kabisa na hivyo amani na
utulivu uliopo hivi sasa vitatoweka kwa kasi ya ajabu baada ya kundi moja
kushindwa kuvumilia manyanyaso na vitendo vya haki za wananchi kukandamizwa kwa
makusudi.
Hivyo kila Mtanzania anapaswa kurejea
katika katiba iliyopo sasa ambayo inatamka wazi kwamba, Tanzania itakuwa ni
nchi ya mfumo wa vyama vingi vya siasa hivyo ili kifungu hicho kitumike vyema
ni vizuri demokrasia ya kuvumiliana ikapewa uhuru ili kuendelea kuilinda amani
iliyopo nchini.
.
SINA UHAKIKA DEMOKRASIA INAYOHAMASISHWA NA NCHI ZA MAGHARIBI NIYA KWELI AU UNAFIKI KWA KUWA UWEZO WA KUFIKIRI WA WAAFRIKA UKO CHINI NDIO SABABU RAIS OBAMA ALIPOFIKA SENEGALI ALIWAAMBIA KUWA DEMOKRASIA KAMILI NI ILE INAYORUHUSU NDOA YA JINSIA MOJA NI VEMA WAAFRIKA TUKAJIANDAA NA JUHUDI ZA DUNIA KUHUSU"MPANGO MPYA WA ULIMWENGUNI WENYE NIA YA KUSUKA ULIMWENGU UPYA ILI UWEZE KUWA TOFAUTI NA WA SASA KIUCHUMI,KISIASA NA KIJAMII KULIKO KUPAMBANA NA MBUZI WA KUCHONGA"
ReplyDelete