18 September 2013

TANZANIA KINARA KUVUTIA MITAJI YA UWEKEZAJI



Na Rehema Maigala
TANZANIA imeendelea kufanya vizuri katika kuvutia mitaji na kuongoza katika nchi za Afrika ya Mashariki.Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya uwekezaji ya Rand Merchant Bank (RMB) ya mwaka 2013 inayotoa mwongozo wa mahali pa kuwekeza kwa kampuni
. Ripoti hiyo inaonesha kuwa kwa mara ya kwanza Tanzania imeishinda Kenya katika kuvutia mitaji ya wawekezaji wa kampuni.Akizungumzia ripoti mbele ya waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Juliet Kairuki, alisema kuwa Tanzania imeshikilia nafasi yake katika kundi la nchi 10 bora zinazovutia uwekezaji wa mitaji ya kampuni kubwa.
Kufanya vizuri kwa Tanzania kunatokana na kuboreshwa kwa mazingira ya uwekezaji ikiwemo jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete.“Ripoti hii ni uthibitisho tosha wa jitihada zinazofanywa na Serikali kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kuvutia mitaji kutoka nje na ndani ya nchi,” alisema Kairuki.
Tanzania, Kenya na Ethiopia ni nchi pekee zilizo katika kundi la nchi 10 zinazofanya vizuri katika eneo hili la Afrika.Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania imepanda nafasi moja na kuwa ya tisa wakati Kenya imeshuka nafasi na kuwa ya kumi.
Pamoja na kwamba Rwanda haikuwa katika nchi 10 bora, bado imeendelea kuwa kivutio na kushika nafasi ya 14. Nchi ya Uganda ni ya 15, Mauritius 16, Angola 20, na Burundi imeshika nafasi ya 41.Nchi ya Afrika Kusini ndiyo inayoongoza kwa kuvutia uwekezaji ikifuatiwa na Nigeria katika nafasi ya pili.
RMB inatumia vigezo vikuu vitatu kuangalia suala zima la kuvutia uwekezaji katika kila nchi kama ifuatavyo: Ukubwa wa soko; ukuaji wa uchumi kwa miaka mitano ijayo na mazingira ya kazi katika nchi husika.Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nchi za Afrika bado zina kazi kubwa ya kufanya kuvutia uwekezaji duniani kulinganisha na nchi nyingine.
Kairuki alisema ripoti hiyo inataka ushirikishwaji zaidi wa sekta binafsi ili kuvutia zaidi mitaji kutoka kampuni na benki kubwa."Kwa mara nyingine tena tunahamasisha ushiriki zaidi wa sekta binafsi katika ujenzi wa nchi yetu," alisema.
Alisema kuwa pamoja na changamoto kubwa iliyopo kuifanya Tanzania kufanya vizuri zaidi, TIC imefurahia ripoti hiyo na kusema kuwa inaonesha juhudi za Serikali katika kujenga mazingira bora ya uwekezaji na biashara.

No comments:

Post a Comment