- KIM AJIPA MATUMAINI AFCON 2015
Na Amina Athumani
WACHEZAJI wa timu ya Taifa,Taifa Stars
wamerejea nyumbani baada ya mechi yao na Gambia iliyochezwa mwishoni mwa wiki,
ambapo walifungwa 2-0 huku matarajio yote sasa yakiwa ni kufuzu kucheza Kombe
la Afrika 2015.
Wachezaji hao
18 pamoja na benchi la ufundi waliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Julius
Nyerere saa nane mchana kwa ndege ya Shirika la Kenya.
Hii ni mechi
ambayo Taifa Stars, inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, ilitakiwa
kushinda lakini ilikosa wachezaji tisa muhimu ambapo baadhi yao hawakuruhusiwa
na klabu zao na wengine walikuwa majeruhi.
Akizungumza
mara baada ya kuwasili nchini, Kocha Mkuu wa Stars, Kim Poulsen alisema
kutokana na hali halisi alilazimika kuwachezesha wachezaji vijana ambao uzoefu
wao si mkubwa sana kama ule wa wachezaji wa kawaida ambao mara nyingi huwa
wanaanza.
"Tumesikitishwa na matokeo haya
lakini kama nilivyosema Gambia waliita wachezaji wao wote wanaocheza nje lakini
sisi tulikosa timu karibu nzima. vijana waliocheza walijitahidi lakini wenzetu waliwazidi
uzoefu," alisema.
Alisema ni muhimu Watanzania watambue
kuwa mechi za kufuzu kucheza kombe la dunia zimekuwa muhimu sana kwa Tanzania,
kwani wachezaji wengi wametambulika na wameitwa nje. "Kuna wachezaji kama
Shomari Kapombe, Mwinyi Kazimoto, ambao kutokana na mechi hizi wamepata nafasi
ya kwenda kucheza nje," alisema.
Kocha huyo alisema yuko makini sana
kutekeleza mpango wa muda mrefu ambao ni kuhakikisha Tanzania inafuzu kucheza
Kombe la Afrika 2015," alisema na kuongeza kuwa timu anayoendelea kujenga
itafanya kazi hiyo."
Alisisitiza kuwa ni lazima TFF
ihakikishe wachezaji wote muhimu wanakuwepo wakati mechi za kufuzu kucheza
Kombe la Afrika zitakapoanza mwakani.
"Kwa sasa wachezaji watarudi
klabuni kwao na baada ya muda mfupi nitawaita tena ili tujiandae na Mashindano
ya CECAFA Senior Challenge yatakayofanyika Nairobi," alisema. Aliwataka
Watanzania wawe na subira kwani ana imani na timu anayoijenga.
Akiunga mkono maneno ya Poulsen, Meneja
wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe, ambaye bia yake inadhamini
Taifa Stars, alisema ni lazima nguvu zote zielekezwe katika AFCON 2015.
"Tungefurahi kama tungefuzu
kucheza Kombe la Dunia lakini ni mapema sana kwa timu yetu ambayo bado
inajengwa tumpe kocha nafasi aweze kutimiza haya malengo na si kumkatisha
tama," alisema.
Alisema
wao kama wadhamini wanafarijika na mabadiliko mbalimbali yaliyofanyika katika
timu ya Taifa tangu waanze kuidhamini timu hiyo mwezi Mei mwaka uliopita.
No comments:
Post a Comment