19 September 2013

MIKE ROSS, JAYDEE KUTUMBUIZA FAINALI REDD’S MISS TANZANIA Na Mwandishi Wetu
WASANII Mike Ross wa Uganda na Judith Wambura ‘Jaydee’, wanatarajia kutumbuiza katika fainali za Redd’s Miss Tanzania 2013, zinazotarajia kufanyika keshokutwa.Wakati wasanii hao wanatarajia kutoa uhondo katika fainali hizo, wadhamini wa mashindano hayo Redd’s Original tayari wametangaza viingilio ambavyo watu watatakiwa kulipia.

  Kiingilio cha juu katika mashindano hayo ambayo yatafanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, uliopo Mwenge, Dar es Salaam ni sh. 100,000 kwa viti maalumu, huku viti vya kawaida vikiwa sh 50,000.Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Meneja, Victoria Kimaro alisema, wanaamini viingilio hivyo ni vya kawaida kutokana na ubora wa mashindano yenyewe.
Victoria alisema, ili kuongeza uhondo katika mashindano hayo wameamua kumleta msanii mahiri kutoka Uganda, Mike Ross atakayeshirikiana na Jaydee' pamoja na kundi la Mama Afrika."Tunaamini kabisa wasanii hawa watakonga nyoyo za mashabiki wa tasnia ya urembo hapa nchini, hivyo napenda kutoa wito kwa mashabiki kujinunulia tiketi mapema ili kuepuka usumbufu," alisema Victoria.
Naye Jaydee alisema, kwa kushirikiana na bendi yake ya Machozi wamejipanga vizuri kuhakikisha wanatoa burudani ya nguvu kwa mashabiki wote watakaohudhuria."Nawaomba mashabiki wangu na wale wa urembo kujitokeza kwa wingi ili kufurahia burudani nzuri kutoka kwangu na bendi yangu ya Machozi, pia wasanii wenzangu waalikwa naamini watafanya vizuri siku hiyo," alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino International Agency, Hashimu Lundenga ambao ni waratibu wa Redd's Miss Tanzania alisema, tiketi za mashindano hayo tayari zimeshaanza kuuzwa katika vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
"Kwa mara nyingine tena napenda kuwashukuru wadhamini wetu wakuu kinywaji cha Redd's Original na wadhamini wenza ambao kwa kweli wamefanya kazi kubwa kuhakikisha shindano la mwaka huu linakuwa zuri na lenye tija kubwa," alisema.
Lundenga alifafanua kuwa, ili kuwapa fursa watu wengi zaidi tiketi itakayonunuliwa katika vituo vilivyopangwa kabla ya mashindano itakuwa ni sh. 80,000 na kutakuwa na ofa kadhaa.Taji la Redd's Miss Tanzania kwa sasa linashikiliwa na Brigitte Alfred, aliyefanikiwa kulitwaa mwishoni mwa mwaka jana.
Redd's Miss Tanzania inadhaminiwa na kinywaji cha Redd's Original kinachozalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), huku wadhamini wenza wakiwa kinywaji cha Zanzi, hoteli ya Giraffe, Star TV, Uchumi Supermarket na Marie Stopes.

No comments:

Post a Comment