- MAHAKAMA YAKATAA OMI LAKE,ARUDI SEGEREA
- AFIKISHWA MAHAKAMANI CHINI YA ULINZI MKALI
Baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu waliofurika kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Morogoro,wakiwa wamekaa chini na wengine kusimama baada ya kuzuiwa kuingia ndani ya chumba cha mahakama. Kulia ni askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), mkoani Morogoro akilinda usalama.
Shekhe Ponda akiwa katika chumba cha Mahakama ya Hakumu Mkazi mkoani Morogoro chini ya ulinzi wa askari Magereza.
Na Ramadhan
Libenanga,Morogoro
Mahakama ya
Hakimu Mkazi mkoani Morogoro, jana imekataa ombi la dhamana ambalo
liliwasilishwa na wakili upande wa utetezi, Bw. Juma Nassoro katika kesi ambayo
inamkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini,Shekhe Ponda Issa
Ponda.
Katika kesi
hiyo, Shekhe Ponda anakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la uchochezi
anayodaiwa kuyafanya Agosti 10 mwaka huu, eneo la Kiwanja cha Ndege, Morogoro.Hakimu Mfawidhi
wa Mahakama hiyo, Bw. Richard Kabate, alisema mahakama haiwezi kumpa dhamana
Shekhe Ponda kutokana na mambo matatu mbali ya kwamba dhamana ni haki ya
mshtakiwa kikatiba.
Mambo hayo ni
pamoja na hati iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), iliyozuia
mahakama hiyo isitoe dhamana kwa mshtakiwa.Bw. Kabate
alisema, pia mshtakiwa amekiuka amri ya kutotenda kosa lolote katika kipindi
cha mwaka mmoja na kutotoka nje ya Dar
es Salaam ambayo ilitolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu.
Msingi wa kesi
Shekhe Ponda
alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Agosti 19 mwaka huu, kwa usafiri
wa helikopta akitokea mahabusu ya Gereza la Segerea, Dar es Salaam.Mahakama hiyo
ilifurika umati wa watu wakiwemo wafuasi wake ambapo Jeshi la Polisi,
liliimarisha ulinzi katika eneo lote la mahakama hadi kesi hiyo ilipoahirishwa.
Baada ya Shekhe
Ponda kutoka mahakamani na kuona umati mkubwa wa watu, aliwapungia mkono na
kujibu salamu hiyo kwa kusema "Takbriir, Allahu Akbar" (Mungu
Mkubwa).Wakili wa
Serikali, Benard Kongola, alisema Shekhe Ponda alialikwa kutoa maelezo machache
kwenye Kongamano la Eid lililoandaliwa na Umoja wa Wahadhiri mkoani humo na
kutamka maneno ambayo ni kosa kisheria.
"Ndugu
Waislamu, msikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti kwani
kamati hizo zimeundwa na Baraza la Waislamu Tanzania
(BAKWATA), ambao ni vibaraka wa CCM na Serikali, kama
watajitokeza kwenu na kujitambulisha, fungeni milango na madirisha
muwapige"
Alidai kwa
maneno hayo, Shekhe Ponda alivunja masharti ya mahakama ya kifungo cha nje
kilichotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya Mei 9 mwaka huu na kutakiwa
ahubiri amani.
Katika shtaka la pili, Shekhe Ponda anadaiwa kuwashawishi
wafuasi wake kutenda kosa la jinai kwa kuwaambia, "Serikali ilipeleka
jeshi mkoani Mtwara ili kushughulikia suala la vurugu iliyotokana na gesi kwa
kuwaua, kuwabaka, kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu.
"Serikali
haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo ambao walikataa Mwarabu asipatiwe
kipande cha ardhi ya uwindaji baada ya kudai ni mali
yao kwa sababu
asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo."Shtaka la tatu
ni kudaiwa kutamka maneno yaliyoumiza imani ya watu wengine kama
yalivyo katika shtaka la pili.
Baada ya kusoma mashtaka hayo, Bw.
Kongola alisema walikuwa na mashahidi 15 na vielelezo vitatu ambavyo ni DVD
mbili na kibali kilichotolewa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Morogoro (OCD),
Agosti mosi mwaka huu cha kongamano hilo na hati ya hukumu iliyotolewa na
Mahakama ya Kisutu, Mei 9 mwaka huu.
Sheikh Ponda aliyakana mashtaka hayo
ambapo Wakili wa utetezi, Bw. Nassor aliwasilisha ombi la dhamana kwa mteja
akisema mashtaka hayo kisheria yana dhamana.Pia Bw. Nassoro aliwasilisha ombi la kupatiwa hati yenye
maelezo ya mlalamikaji ambaye ni Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania
na kudai kuwa, kutokana na upelelezi upande wa mashtaka kukamilika, wanahitaji
maelezo hayo ili waweze kuandaa utetezi.
Bw. Kongola aliiomba Mahakama kutompa
dhamana mshtakiwa kutokana na cheti kilichotolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka
(DPP), kupinga dhamana ya mshtakiwa huyo kwa ajili ya usalama wa nchi.Hakimu
Kabate aliahirisha kesi hiyo na kudai Septemba 17 mwaka huu, Mahakama hiyo
ingetia uamuzi kama mshtakiwa atapewa dhamana
au la.
Aliosema sk,Ponda yote ni sahihi hakuna hata en moja la unfiki, Ila kwa sababu madia zote ni zenu basi fanyeni mtakalo ,lkn mkae mkijua iko cku halali na harmu, ukweli na uongo na hizo fitna zenu zina mwisho wake, ALLAH KARIM
ReplyDelete