02 September 2013

UTAPELI UBUNGO : UAMUZI MGUMU



  •  POLISI WASAFISHA MTANDAO WA MAPALANJA

Na Waandishi Wetu
SAKATA la utapeli mkubwa uliokuwa ukifanywa na watu wanaojifanya waajiriwa wa Idara ya Usalama wa Taifa, Polisi na Uhamiaji, katika Kituo cha Mabasi yaendayo mikoani Ubungo (UBT), Dar es Salaam, sasa limeanza kupatiwa ufumbuzi.

Hali hiyo inatokana na operesheni kubwa iliyofanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni usiku na mchana ndani ya kituo hicho ili kuubaini mtandao unaofanya vitendo hivyo.Chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya kituo hicho, kimesema operesheni hiyo imeanza wiki iliyopita tangu kuripotiwa kwa mtandao huo na gazeti la Majira.
Katika operesheni hiyo, jeshi hilo lilibaini matapeli hao walikuwa wakifahamika kwa jina maarufu ‘MAPALANJA’ wanaodaiwa kushirikiana na baadhi ya askari polisi kufanya uhalifu huo.Chanzo hicho kiliongeza kuwa, matapeli hao walikuwa wakinasa mawasiliano ya redio za polisi kupitia kwa wenzao; hivyo taarifa zilizokuwa zikihusu operesheni ya jeshi hilo ndani ya kituo hicho walikuwa wakizipata na kukimbia.
"Matapeli hawa ni wengi, baadhi yao ni waajiriwa wa Jeshi la Polisi kutoka vituo vingine si Ubungo na polisi wastaafu, hivyo kukamatwa kwao, polisi wamefanya uamuzi mgumu," kilidai chanzo hicho na kulipongeza gazeti la Majira kwa kazi nzuri na kubwa waliyoifanya kuufichua mtandao huo.
"Ukifika Ubungo sasa hivi, hali ni shwari kabisa...matapeli wote hawapo, mtandao huu ulikuwa ukiogopwa na kila mtu hapa stendi, hata taarifa zao zilipofika polisi, walikuwa wakikamatwa na kuachiwa," kiliongeza chanzo hicho.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili ambazo hazijathibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camilius Wambura, zilidai baadhi ya askari polisi Kituo cha Ubungo wamehamishwa vituo vyao vya kazi.Majira lilimtafuta Kamanda Mwambura ili aweze kuthibitisha taarifa hizo na idadi ya polisi waliohamishwa, lakini simu yake ya mkononi ilikuwa imezimwa muda mrefu.
Mkuu wa Kituo cha Polisi Ubungo alipopigiwa simu ili kuthibitisha taarifa hizo hakuwa tayari kuzungumza na kusema yeye si msemaji, hivyo aliwataka waandishi wawasiliane na Kamanda Wambura.
"Ninachofahamu kweli tumefanya operesheni kali sana ndani ya kituo ila siwezi kuzungumza lolote juu ya hilo, mpigie RPC wa Kinondoni," alisema Mkuu wa Kituo hicho.
Kwa upande wake, Chama cha Wamiliki wa Mabasi yaendayo Mikoani (TABOA), kimelipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuwakamata watu wanaofanya vitendo vya utapeli kwa abiria wanaotoka mikoani na nchi jirani.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana akiwa mkoani Kilimanjaro, Katibu Mkuu wa TABOA, Enea Mrutu alisema utapeli ndani ya kituo hicho ulikuwa kero kwa watumiaji wa kituo hicho."Tunampongeza Kamanda Mpya wa Polisi Kinondoni, Camilius Wambura kwa kazi nzuri aliyoifanya katika kituo hicho, tunamuomba asiishie hapo, kazi iendelee usiku na mchana," alisema Mrutu.
Utapeli huo ulikuwa ukifanywa kwa abiria wanaoshuka katika kituo hicho wakitokea mikoa ya mbali kama Kigoma, Bukoba na nchi jirani za Kenya, Uganda, Bunjumbura na Malawi.

1 comment:

  1. Kuwabadilisha Vituo vya kazi kwa Wahalifu sio adhabu kwa Askari alie asi kazi yake.Kwa nini wazifukuzwe kazi mara moja kuwavua magwanda na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kama Raia wengine?. Jeshi hilo la Polisi haliwezi kujisifu kwa kuwahurumia wenzao ,hawa ni wezi na wahalifu wa sheria lazima waadhibiwe kama watu wengine si hivyo Doa kubwa lipo pale pale.

    ReplyDelete