Na Daud Magesa, Misungwi
HALMSHAURI ya Wilaya ya Misungwi Mkoa wa Mwanza inadaiwa kupoteza sh. milioni 27.9 katika kipindi cha miezi kumi, kati ya sh. milioni 41.2 zinazopaswa
kukusanywa kutoka mgodi wa wachimbaji wadogo wa dhahabu wa Ishokela.
Fedha hizo zinadaiwa kutafunwa na baadhi ya maofisa wa wilaya hiyo, wakishirikiana na Ofisa Mtendaji mmoja wa kata ambaye amepewa zabuni ya kukusanya ushuru kutoka katika machimbo ya mgodi huo.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na timu ya waandishi akiwemo mwandishi wa gazeti hili katika mgodi huo umebaini kuwa, pamoja na kiwango kikubwa cha pesa zinazotozwa ushuru kukusanywa katika machimbo hayo, fedha nyingi zinaishia kwenye matumbo ya maofisa hao na kuwasilisha kidogo.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, fedha zinazowasilishwa katika Halmashauri kwa mwezi ni sh. 1,324,000 badala ya sh. 4,120,000, hivyo kiasi cha sh. 2,796,000 kikidaiwa kuchakachuliwa na mmoja wa vigogo wa halmashauri hiyo.
Kutokana na ulaji huo, kiasi cha sh. 27,960,000 zimetafunwa kwa kipindi cha miezi 10 iliyopita kutoka Julai 2010 hadi Aprili mwaka huu na kuwasilishwa kiasi cha sh. 13,240,000 kati ya sh. 41,200,000 zilizokusanywa kwa kipindi hicho.
Misungwi katika mwaka wa fedha wa 2010/2011, ilikadiria kukusanya sh. 545,483,500 kutoka katika vyanzo vyake vya ndani lakini tangu Julai 2010 hadi Machi 201 1mwaka huu, ilikuwa imekusanya sh. 177,918,365, sawa na asilimia 33 badala ya asilimia 75.
Uchunguzi huo ulibaini kuwa makusanyo ya mwezi katika mgodi huo ni ambayo yanajumuisha maduka 20 kila moja hulipa ushuru wa sh. 30,000; badala ya sh 600,000 zinawasilishwa ni sh. 300,000/=.
Mialo 80, kila mmoja sh 20,000 na huwasilishwa sh. 400,000 badala ya sh 1,600,000 na Krasha za kusaga mawe ya dhahabu 90, kila moja sh. 10,000, huwakilishwa sh. 500,000 badala ya sh. 900,000.
Mapato mengine yanayotozwa Ishokela ni vibanda migahawa, baa na maduka 150, kila mmoja hulipia sh 2,000, huwasilishwa sh. 100,000 badala ya sh 240,000.
Mengine ni machinjio ya ng’ombe kila siku sh 2,000 (kwa mwezi sh 600,000) lakini huwasilishwa sh. 24,000 na gulio la kila Jumatatu sh. 120,000 (kwa mwezi 480,000) lakini hazijulikani zinapokwenda.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, ofisa mmoja wa Kata hiyo anayetoza ushuru wa machimbo hayo, anadaiwa kuwasilisha kiasi cha fedha zinazoibwa kwa baadhi ya vigogo wa halmashauri hiyo kabla kugawana. ofisa huyo anadaiwa kukusanya ushuru kwa kutumia stakabadhi bandia zilizochapisha kwa lengo la kujinufaisha wao binafsi na mmoja wa vigogo vya halmashauri.
Akizungumza kwa njia ya simu mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Bw. Xavier Tiluselekwa alikiri kuwepo kwa taarifa za ubadhilifu huo na kudai tayari aliagiza uchunguzi ufanyike upya ikiwa pamoja na kufanya tathmini ya biashara zilizopo Ishokela.
“Kwa sasa mimi sipo Misungwi, niko nje kikazi. Kweli suala hilo lipo na wiki mbili zilizopita niliagiza tathmini na uchunguzi ufanyike ili kubaini kiasi cha mapato kinachopotea. Naomba uwasiliana na Bi. Jane Binamungu anayekaimu atakueleza,” alisema Bw. Tiluselekwa.
Bi. Binamungu alisema kwamba halmashauri hiyo imejizatiti katika mwaka ujao wa fedha kuziba mianya yote ya upotevu wa mapato ikiwa ni pamoja na ya Ishokela, ambayo kama alivyodai bosi wake, wanafanyia uchunguzi kubaini ulaji huo.
No comments:
Post a Comment