03 September 2013

BILIONI 881/- KUSAMBAZA UMEME Na Darlin Said
ZAIDI ya sh. bilioni 881, zitatumika katika mradi wa kusambaza umeme vijijini na kuwanufaisha zaidi ya wateja 250,000.Mwenyekiti wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Balozi Ami Mpungwe, aliyasema hayo Dar es Salaam jana baada ya kusaini mikataba 15 ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini awamu ya pili.

Alisema lengo la mradi huo ni kusambaza umeme katika mikoa 24 ya Tanzania Bara hususan vijijini na kwenye Makao Makuu ya Wilaya 13 zisizo na umeme."Utekelezaji wa miradi katika mikoa 14 iliyopata makandarasi, unaenda sambamba na ujenzi wa vituo sita vya usambazaji umeme ambavyo vitajengwa Tunduru, Mbinga, Ngara, Kigoma, Kasulu na Kibondo," alisema Balozi Mpungwe.
Alitaja mikoa iliyopata makandarasi kuwa ni Ruvuma, Arusha, Dodoma, Mara, Iringa, Kilimanjaro, Singida Mtwara, Mwanza, Tabora, Njombe, Katavi, Shinyanga na Simiyu ambapo mikoa 10 haijapata makandarasi."Katika kutekeleza miradi hii, huduma za kijamii kama shule, zahanati na visima vya maji vitapewa kipaumbele kwa kuunganishiwa umeme," aliongeza.
Wakati huo huo, Balozi Mpungwe aliwataka wakandarasi wote kuhakikisha wanasimamia na kutekeleza wajibu wao kulinganana mikataba na wale ambao watakwenda tofauti hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Alisema asilimia 98 ya vijiji vilivyopo nchini, vina matatizo ya kupata umeme usio na uhakika hivyo kuanzishwa kwa REA, kumesaidia ongezeko la upatikanaji umeme katika maeneo hayo kwa asilimia saba ukilinganisha na awali ambapo asilimia 2.5 ya wananchi waishio vijijini ndio waliokuwa wanapata umeme.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa REA, Bw. George Nchwali, alisema Utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini ni sehemu ya juhudi za Serikali kufanikisha Mipango ya Maendeleo ya Taifa kama ilivyoainishwa katika Dira ya Maenedeleo ya Taifa kufikia asilimia 30 wa wananchi waishio vijijini, wanapata umeme ifikapo mwaka 2015

1 comment:

  1. Balozi Ami Mpungwe anaaminika au amejirudi? Inatia wasiwasi. Sijui kama baa la Tanzanite One linatukumbusha kitu na ni wajibu wetu waTanzania kujifunza kwa yaliyopita ili tuweze kupanga yajayo mbele yetu.

    ReplyDelete